Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM, Aprili 10, 2026 — Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imeweka historia baada ya kuwa taasisi ya kwanza nchini kupata cheti cha kimataifa cha ISO 21001:2018, kinachohusu mifumo ya usimamizi wa taasisi za elimu, hatua inayotarajiwa kuinua viwango vya ubora katika utoaji wa elimu ya ufundi na teknolojia nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kukabidhi cheti hicho, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Hussein Mohamed, amesema mafanikio hayo yanaashiria hatua muhimu katika mageuzi ya sekta ya elimu yanayolenga kuimarisha mafunzo yenye ujuzi, ubunifu na tija kwa maendeleo ya taifa.
Amesema mafanikio ya DIT yanaendana na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kujenga mfumo wa elimu unaozalisha wataalamu wenye uwezo wa kushindana katika soko la ajira la ndani na kimataifa.
“Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya viwanda,” amesema Mohamed.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yanaonesha umuhimu wa kuunganisha elimu na sekta ya uzalishaji ili wahitimu waweze kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi unaotegemea sayansi, teknolojia na ubunifu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Ashura Katunzi, amesema utoaji wa cheti hicho unaonesha kuwa DIT imekidhi viwango vya kimataifa katika utoaji wa huduma za elimu.
Amesema mfumo wa usimamizi wa elimu wa taasisi hiyo umehakikiwa na kuthibitishwa kuwa unazingatia viwango vinavyotambulika kimataifa, hali inayotoa uhakika wa ubora wa mafunzo yanayotolewa kwa wanafunzi.
“Cheti hiki ni uthibitisho wa juhudi, nidhamu na dhamira ya taasisi katika kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa na ujuzi unaowawezesha kushindana katika soko la ajira la kimataifa,” amesema Katunzi.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi hiyo, Masika, amesema kupatikana kwa cheti hicho ni matokeo ya mchakato wa maboresho ya mifumo ya uendeshaji ulioanza mwaka wa fedha 2021/22 kwa lengo la kuhakikisha elimu inayotolewa na taasisi hiyo inafikia viwango vya kimataifa.
Ameeleza kuwa cheti hicho kinahusu kampasi zote tatu za taasisi hiyo zilizopo Dar es Salaam, Mwanza na Songwe, na kwamba utekelezaji wake utaongeza uaminifu wa wadau, kuimarisha ubora wa mafunzo pamoja na kuongeza ushindani wa wahitimu katika soko la ajira.
Masika amesema mafanikio hayo pia yanaunga mkono utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2023 pamoja na malengo ya maendeleo ya muda mrefu ya taifa kuelekea Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, hasa katika kuimarisha rasilimali watu wenye ujuzi.
Amesisitiza kuwa taasisi hiyo itaendelea kuboresha mifumo ya ubora, kufanya tathmini za mara kwa mara na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha elimu ya ufundi na teknolojia nchini inaendelea kukidhi viwango vya kimataifa.
DIT Yaweka Historia kwa Kupata Cheti cha Kimataifa cha ISO 21001:2018
Share This
Tags
# HABARI
Share This
Jiachie Blog
HABARI
Labels:
HABARI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Author Details
A Tanzanian blog operating since 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.















No comments:
Post a Comment