Mwamvua Mwinyi, Rufiji Aprili 26, 2026
Mwenge wa Uhuru wahimiza na kuhamasisha wananchi kuunga mkono matumizi ya nishati safi ikiwemo gesi ya kupikia, majiko banifu na umeme, hatua inayolenga kulinda mazingira, kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ili kuboresha afya ndani ya jamii.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, alitoa rai hiyo Aprili 26, 2026 wakati wa ukaguzi wa mradi wa nishati safi, uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati salama uliogharimu sh. milioni 38.419 zilizotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ambapo mitungi 40 ya gesi iligawiwa kwa makundi maalum katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Ikwiriri (FDC).
Alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ni kinara wa kampeni ya nishati safi nchini, huku akisisitiza wananchi kumuunga mkono kwa vitendo ili kuhakikisha malengo ya matumizi ya nishati safi yanafikiwa.
Aidha, Mwang’onda aliwaomba Watanzania kuendelea kulinda amani na utulivu na kushikamana, akitolea mfano wa Wilaya ya Rufiji ilivyowasaidia watu wenye mahitaji maalum kwa kuwapatia mitungi ya gesi.
Mradi huo unalenga kupunguza uchafuzi wa mazingira unaotokana na moshi wa kuni na mkaa, kupunguza ukataji miti na hivyo kuhifadhi misitu pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kadhalika, imeelezwa kuwa Wilaya ya Rufiji inaendelea na juhudi za upandaji miti ambapo jumla ya miti 3,430,630 ya aina mbalimbali ikiwemo mikorosho, matunda, kivuli na mbao imepandwa.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Fredrick Komba, alisema jumla ya miradi saba yenye thamani ya shilingi bilioni 4.95 imepitiwa wilayani humo, ambapo miradi mitatu imekaguliwa na minne kuwekwa mawe ya msingi, akipokea Mwenge wa Uhuru katika Uwanja wa Shule ya Msingi Umwe Aprili 26, 2026.
Miongoni mwa miradi hiyo ni,mradi wa barabara ya Chumbi-Kiegele kilometa 8.0 kati ya hizo km 1.1 imejengwa kwa kiwango cha lami kwa wastani wa upana mita 7 kwa gharama ya bilioni 1.499 fedha kutoka Serikali kuu kupitia Wakala wa barabara za vijijini na mijini (TARURA).
Mradi mwingine ni ujenzi wa vyumba sita vya madarasa na ofisi mbili za walimu katika Shule ya Sekondari Bwawani sanjali na ugawaji wa hati kwa wafugaji katika Kata ya Chumbi.
.jpeg)


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


No comments:
Post a Comment