
Mwanahabari Kelvin Justine Raphael, maarufu kama Zungu (Matejoo), ameonywa kuwa anaweza kuchukuliwa hatua kali zaidi, zikiwemo kusimamishwa au kufutiwa ithibati yake, endapo ataendelea na uandishi usiozingatia maadili ya taaluma.
Onyo hilo limetolewa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) baada ya kubainika kuwa mwandishi huyo alikiuka maadili ya taaluma kupitia maudhui aliyochapisha kuhusu tukio la uchelewaji wa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) lililotokea Februari 21, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Msomi Patrick Kipangula, mwandishi huyo aliitwa mbele ya bodi na kupewa fursa ya kujieleza. Baada ya kusikilizwa, bodi ilijiridhisha kuwa alitoa kauli zilizokuwa na matusi, kejeli na lugha isiyo ya staha, kinyume na misingi ya taaluma ya uandishi wa habari.
Bw. Zungu amekiri makosa yake na kuomba radhi. JAB imemtaka kuondoa mara moja maudhui hayo katika majukwaa yote aliyoyachapisha na kurejea katika misingi ya weledi, maadili na uwajibikaji wa taaluma.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 14(b) cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, JAB imeonya kuwa haitasita kuchukua hatua kali zaidi iwapo makosa kama hayo yatarudiwa. Bodi pia imewakumbusha waandishi kuzingatia matumizi ya lugha yenye staha wanapotekeleza majukumu yao.


No comments:
Post a Comment