JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


DKT. NCHIMBI: KUNYIMA HAKI WANACHAMA KUNAWEZA KUUA CHAMA CHOCHOTE CHA SIASA.

Share This

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM , Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema kuwa jambo linaloweza kuua chama chochote cha siasa ni kunyima haki wanachama wake, akisisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapaswa kuzingatia Katiba yake kwa kulinda haki ya kuchagua na kuchaguliwa kipindi cha chaguzi mbalimbali.

Dkt. Nchimbi, ambaye pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa Dodoma, ameyasema hayo leo Februari 5, 2026, wakati wa maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika katika viwanja vya VETA, Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma.

Amesema ndani ya CCM ni muhimu kuhukumu wanachama kwa misingi ya haki, akibainisha kuwa maamuzi yanapaswa kufanyika kwa wakati unaostahili pindi kosa linapobainika, badala ya kusubiri miaka mingi na baadaye kumzuia mwanachama kupata fursa ya kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa kiongozi.

Aidha, amesisitiza kuwa mchakato wa uchaguzi wa viongozi ndani ya chama unapaswa kuendeshwa kwa haki, uwazi na bila fitina, ili kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama.

Akizungumzia historia ya CCM, Dkt. Nchimbi amesema chama hicho kilianzishwa tarehe 5 Februari 1977 baada ya kuunganishwa kwa vyama vya TANU na ASP, uamuzi wa busara uliolenga kuimarisha umoja wa kitaifa baada ya kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar.

Ameeleza kuwa kwa heshima ya waasisi wa vyama hivyo, Hayati Julius Nyerere na Hayati Abdu Jumbe,  wanachama wa CCM wanapaswa kuuenzi Muungano wa vyama hivyo viwili kwa kuendelea kuimarisha mshikamano ndani ya chama.

Dkt. Nchimbi amesema CCM ni chama cha wananchi wote na si cha kundi fulani la watu au viongozi, akisisitiza kuwa chama kinapaswa kuendelea kufanya siasa zinazogusa maisha ya wananchi na kuendana na matarajio yao.

Ameongeza kuwa msingi wa chama ni wananchi, hivyo viongozi na wanachama wote wanapaswa kuhakikisha matendo na kauli zao zinalinda hadhi ya chama na kuimarisha imani ya wananchi kwa CCM.

Amesema CCM inapaswa kuendelea kuwa mfano wa kuigwa katika kufanya siasa safi, kwa kuepuka kuchafuana au kupakana matope, na badala yake kujikita katika matendo yanayojenga Taifa la Tanzania.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa, amesema CCM imeendelea kufanya kazi kubwa za maendeleo kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa, akieleza kuwa CCM ni chama cha vitendo na si cha maneno matupu.

Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pili Mbanga, amesema CCM Dodoma inampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais  kwa ushindi walioupata mwaka jana, akiongeza kuwa mahusiano kati ya chama na Serikali yameimarika na yanaendelea kuwa ya ushirikiano mzuri.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na wajumbe wa Kamati za Siasa za wilaya na mkoa, wajumbe wa Sekretarieti,  madiwani, wenyeviti na makatibu wa kata na vijiji pamoja na mabalozi na mabaraza ya wazee CCM kutoka wilaya zote za Mkoa wa Dodoma, Wabunge, Katibu wa UWT Taifa, Waziri wa Maliasili na utalii, pamoja na Naibu waziri wa Elimu Sayansi ya Teknolojia.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad