JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Bilioni 12.8 zatumika Matengenezo ya Km 13.1 za barabara Iringa-Mtera

Share This
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara Mhandisi Rashid Kalimbaga akimuelekeza jambo Meneja wa TANROADS Iringa Mhandisi Yudas Msangi (alieshika karatasi), wakati wa ziara ya ukaguzi wa barabara ya Iringa-Mtera. Kulia kwa Msangi ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Mhandisi Mussa Natty na Kaimu Mkurugenzi Huduma za Matengenezo wa Bodi Mhandisi Jacob Mukasa.

**************

Kiasi cha bilioni 12.8 zimetumika katika kazi za matengenezo ya Kilomita 13.1 za barabara ya Iringa-Mtera, ambayo ni kiunganishi muhimu cha jamii, biashara na huduma za kijamii.

Barabara hiyo imefanyiwa matengenezo hayo makubwa yenye lengo la kuboresha usalama, ufanisi na uimara wake.

Kwa mujibu wa taarifa fupi ya Matengenezo ya Barabara ya Iringa–Mtera, iliyosomwa na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Iringa, Mhandisi Yudas Msangi, amesema mradi huo umehusisha matengenezo ya jumla ya Kilomita 13.1 kwa gharama ya shilingi bilioni 12.8.

Taarifa hiyo imewasilishwa mbele ya wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara(RFB),wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Mussa Natty, pamoja na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mifuko ya Matengenezo ya Barabara Afrika (ARMFA), Mhandisi Rashid Kalimbaga, wakati wa ziara yao ya kukagua utekelezaji wa kazi za matengenezo ya barabara

Mhandisi Msangi amesema kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kuziba mashimo, kuimarisha tabaka la juu la barabara, kuboresha mifumo ya mifereji ya maji na kuweka alama za barabarani kwa lengo la kuongeza usalama kwa watumiaji wa barabara.

Amesema, maboresho hayo yamechangia kupunguza gharama za uendeshaji wa magari, kupunguza muda wa safari na kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya Iringa na Mtera.

“Zaidi ya kuboresha miundombinu, matengenezo haya yanaaksi dhamira ya kuendeleza usimamizi endelevu wa barabara. Mtandao imara wa barabara ni msingi wa ukuaji wa uchumi, unaowaunganisha wakulima na masoko, kusaidia shughuli za utalii na kuwezesha upatikanaji wa huduma za elimu na afya,” amesema Mhandisi Msangi.

Pia amesema kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa Mkoa wa Iringa na Taifa kwa ujumla, kwani inatumika kusafirisha bidhaa kutoka mikoa ya Kusini kuelekea Kaskazini,na ni sehemu ya mtandao mkubwa wa barabara unaounganisha nchi za kusini na kaskazini mwa Afrika hadi Cairo, Misri.

Hata hivyo utekelezaji wa matengenezo ya barabara ya Iringa–Mtera unaonesha dhamira ya Serikali kupitia Mfuko wa Barabara ya kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya miundombinu.

Kutokana na hali bora ya barabara iliyoboreshwa, wananchi wanaoishi kandokando ya barabara hiyo wanatarajia kunufaika na safari salama zaidi pamoja na fursa pana za kiuchumi.
Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Vicent Minja, akielekeza jambo kuhusu mabega ya barabara kwa Meneja wa TANROADS Iringa Mhandisi Yudas Msangi (aliyeshika karatasi), wakati wa ziara ya ukaguzi wa barabara ya Iringa-Mtera. Kushoto kwa Minja ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Mhandisi Mussa Natty na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara Mhandisi Rashid Kalimbaga.

​Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wakimsikiliza Mhandisi Yudas Msangi, Meneja wa TANROADS mkoa wa Iringa (aliyeshika karatasi), wakati wa zira ya Bodi hiyo ya kukagua kazi za matengenezo ya barabara katika mkoa wa Iringa, kipande cha Iringa hadi Mtera km 123.
Muonekano wa Sehemu ya Barabara ya Iringa hadi Mtera km 123 eneo la Mtera. Picha imepigwa wakati wa ziara ya Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara iliyolenga kukagua kazi za matengenezo ya barabara kwenye barabara hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad