BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limefuta matokeo ya watahiniwa 77, wakiwemo 30 wa shule na 47 wa kujitegemea, waliobainika kufanya udanganyifu wakati wa Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) 2025 uliofanyika kuanzia Novemba 17 hadi Desemba 5, 2025.Mbali na hao, NECTA pia limefuta matokeo ya watahiniwa wawili wa shule baada ya kubainika kuandika lugha ya matusi katika skripti zao, kinyume na taratibu za mitihani.
Hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Mitihani Sura ya 107 pamoja na Kanuni za Mitihani za mwaka 2016.
Akizungumza wakati wa kutangaza rasmi matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, alisema baraza halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo vinavyokiuka maadili na taratibu za mitihani ili kulinda uadilifu wa mfumo wa elimu nchini.
Katika hatua nyingine, NECTA limezuia kutolewa kwa matokeo ya watahiniwa 435 waliopata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mitihani yote au sehemu kubwa ya masomo. Watahiniwa hao wamepewa fursa ya kufanya mitihani ya masomo husika mwaka 2026.
Hata hivyo, matokeo ya CSEE 2025 yameonesha ongezeko la ufaulu kwa ujumla. Kati ya watahiniwa wa shule 554,458 wenye matokeo, jumla ya 526,620 sawa na asilimia 94.98 wamefaulu kwa kupata madaraja ya I hadi IV, ikilinganishwa na asilimia 92.37 mwaka 2024, ongezeko la asilimia 2.61.
Ufaulu umeonekana kuwa mzuri zaidi kwa wavulana, ambapo asilimia 95.79 wamefaulu, ikilinganishwa na asilimia 94.26 kwa wasichana. Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 62.51 mwaka 2024 hadi asilimia 73.83 mwaka 2025.
Kwa mujibu wa NECTA, ubora wa ufaulu pia umeimarika, huku watahiniwa 255,404 wa shule wakipata madaraja ya I hadi III, sawa na asilimia 46.06, ikilinganishwa na asilimia 42.96 mwaka uliotangulia.
Kwa upande wa shule, kati ya shule 5,843 zenye matokeo, shule 5,839 sawa na asilimia 99.93 zimepata wastani wa madaraja A hadi D, huku idadi ya shule zilizopata wastani wa madaraja A hadi C ikiongezeka kwa zaidi ya asilimia tano.
Profesa Mohamed alizipongeza kamati za uendeshaji mitihani, wakuu wa shule, wasimamizi, wasahihishaji pamoja na watahiniwa waliotii taratibu za mitihani kwa kazi kubwa waliyoifanya.


No comments:
Post a Comment