JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


TASAC YAFANYA MAJARIBIO YA BOTI YA UTAFUTAJI NA UOKOAJI MKOANI TANGA

Share This

 

Nahodha Grayson Marwa ni Mkaguzi Mwandamizi wa Meli Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC)akizungumza mara baada ya kufanya ukaguzi na  majaribio ya Boti ya Utafutaji na Uokoaji Mkoani Tanga.
Boti ya Utafutaji na Uokoaji katika majaribio mkoani Tanga
Maafisa wa TASAC na Wazabuni wa Boti ya Utafutaji na Uokoji wakiwa ndani ya Boti mara baada ya kuifanyia majaribio mkoani Tanga.


*Kongole zatolewa kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kufanya matokeo kwa vitendo

Na Mwandishi Wetu,Tanga

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limefanya ukaguzi na majaribio ya kitaalamu ya boti ya utafutaji na uokoaji (SAR) katika Bahari ya Hindi Mkoa wa Tanga, kwa lengo la kuthibitisha ubora, uwezo na utendaji kazi wa chombo hicho kabla ya kuanza kutumika rasmi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Nahodha Gryson Marwa, Afisa Mwandamizi Ukaguzi na Usajili wa Meli kutoka TASAC, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imenunua boti mbili mpya za utafutaji na uokoaji, ambapo moja tayari imepelekwa mkoani Tanga ili kuongeza uwezo wa uokoaji katika maeneo ya bahari ya Hindi mkoani humo.

“Tumeendesha majaribio na ukaguzi wa kina ili kuhakiki uwezo, ubora na vigezo vya kiufundi kama vimezingatiwa ipasavyo, hakika boti hii imethibitisha kuwa ina mwendokasi wa maili 40 kwa saa, ina vifaa vyote muhimu, na uwezo mkubwa wa kutekeleza operesheni za utafutaji na uokoaji majini,” amesema Nahodha Marwa.

Kwa upande wake, Nahodha Christopher Shalua, Afisa Mwandamizi Ukaguzi na Usajili wa Meli ambae pia ni Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Tanga, ameipongeza Serikali kwa uwekezaji huo akisema boti hiyo itarahisisha na kuharakisha shughuli za uokoaji majini pindi dharura zitakapotokea zinafanyika kwa weledi.

Ameongeza kuwa boti hiyo itawanufaisha wavuvi na wasafiri wa maeneo ya Pangani, Kipumbwi na maeneo jirani, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kutumia vifaa vya uokozi licha ya kuimarishwa kwa uwezo wa uokoaji.

Kwa upande wao wavuvi wa mialo ya Sahare na (Deep Sea) wameishukuru Serikali kwa hatua hiyo wakieleza kuwa hapo awali, walipokumbwa na dharura walilazimika kujichangisha na kukodi vyombo ili kufanya uokoaji, jambo lililokuwa likihatarisha maisha yao.

Ujio wa boti hiyo mkoani Tanga ni sehemu ya mkakati wa Serikali kupitia TASAC wa kuimarisha usalama wa usafiri majini, kupunguza ajali na kuhakikisha hakuna mvuvi au msafiri anayepoteza maisha kutokana na kuchelewa kuokolewa.




Matukio mbalimbali ya majaribio ya Boti ya Utafutaji na Ukoaji mkoani Tanga.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad