

Na Khadija Kalili, Kibaha
MSTAHIKI MEYA wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Nicas, ametoa amri ya kufungwa kwa viwanda viwili kwa kosa la kutiririsha maji taka yenye sumu na kinyesi yanayoathiri wananchi katika eneo hilo.
Viwanda vilivyofungiwa ni Radiant kinachotengeneza vinywaji na vipodozi, na Kiwanda cha Fortune Paper Group Limited, vyote vipo katika Kata ya Misugusugu, Manispaa ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.
“Nimefikia uamuzi wa kuvifungia viwanda hivi baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba wanatiririsha maji machafu yanayotoka kiwandani pamoja na maji machafu ya chooni, jambo linalopelekea kuathiri afya za wananchi wanaoishi katika eneo husika,” amesema Dkt. Nicas.
Hatua ya kukifungia kiwanda hicho imechukuliwa jana tarehe 31 Desemba 2025, ambapo wananchi walitoa kero hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Shule ya Miomboni, Kata ya Misugusugu, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Wananchi hao walitoa malalamiko kwa kusema kuwa maji hayo yanayotiririshwa kutoka kiwanda cha Radiant yanaathiri afya zao, huku baadhi wakionesha kupasuka nyayo na kuvimba miguu baada ya kukanyaga maji hayo, ambayo pia imedaiwa yanakausha mazao yanayolimwa na wananchi katika eneo husika, wakitaja baadhi ya mazao kuwa ni mahindi, mbogamboga za majani na matango.
Dkt. Nicas, baada ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi, aliamuru jopo la wataalam kwenda kuona hali halisi katika eneo linalolalamikiwa na wananchi, na mara baada ya kufika walishuhudia maji machafu yenye harufu kali yakitiririka kutoka kiwandani.
Dkt. Nicas alishuhudia ujenzi holela wa mfereji unaolalamikiwa unaotiririsha maji hayo machafu na kuathiri afya za wananchi, ndipo akaamuru kiwanda kifungwe hadi watakapotekeleza kwa kufuata miongozo ya mazingira.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Mlela, amekiri kwa kusema hali waliyoishuhudia si rafiki kwa wananchi, na amesisitiza Mkurugenzi wa Kiwanda cha Radiant kufuata maelekezo aliyokuwa amepewa mara kadhaa na Baraza la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC). Amesema inasikitisha kuona kiwanda kimepewa maonyo mara tatu bila utekelezaji.
“Wameonywa mara tatu na yeye Mahesh anakubali hilo, lakini bado hakuna utekelezaji wa aina yoyote. Malalamiko ya wananchi yamekuwa mengi, hivyo wanahitaji na sisi viongozi tuje hapa kulalamika. Hii haiwezekani,” amesema Mheshimiwa Meya Dkt. Nicas.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Mrisho Mlela, ameongeza kwa kusema kuwa kwa kuwa hawajatii sheria za usimamizi wa mazingira, hivyo wamesimamisha shughuli za uzalishaji hadi pale watakapotekeleza ujenzi wa mabwawa ya maji taka kama walivyoelekezwa, ambayo hayataleta madhara kwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutolewa amri hiyo, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Radiant, aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Mahesh na kugoma kutaja jina lake la pili, amesema hakuna lazima. Amekiri udhaifu huo na kwamba wamepewa onyo mara tatu bila utekelezaji, na ameahidi kuwa ndani ya muda wa miezi mitatu watajenga na kurekebisha mifumo ya maji taka pamoja na mabwawa ya kutiririsha majitaka kutoka kwenye kiwanda cha Radiant, kwa kufuata taratibu na sheria za mazingira kwa kuweka mifumo ya kisasa ya kuchuja maji taka yenye kemikali.
Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kwa kushirikiana na Maofisa Mazingira wa Manispaa ya Kibaha, wamefika kwenye viwanda hivyo na kutoa ufumbuzi wa haraka wa kudhibiti uchafuzi huo wa mazingira.
Raheli Ulaya, Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Kibaha, amekiri kutoa onyo zaidi ya mara tatu lakini wamiliki hao hawajaonesha kutii, hivyo amevifungia kwa muda hadi hapo hali itakaporidhisha.
Diwani wa Kata ya Misugusugu, Ally Simba, pamoja na baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa, wamekiri kuwepo kwa uchafuzi huo wa mazingira.

.jpeg)
.jpeg)


No comments:
Post a Comment