Katika ziara hiyo, Nsekela alipokea taarifa ya kina kuhusu utekelezaji wa shughuli za ofisi tangu ilipoanza kazi rasmi Oktoba 2025, akiongozwa na Mwakilishi wa CRDB Bank Dubai, Jackson Kehengu. Taarifa hiyo ilieleza mafanikio ya awali katika kujenga mahusiano na wawekezaji, wafanyabiashara wakubwa, na washirika wa kifedha, ambao wameonesha kuvutiwa kwa kiwango kikubwa na upanuzi wa Benki ya CRDB katika Mashariki ya Kati.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Nsekela alisema Dubai ni kitovu muhimu cha biashara na uwekezaji duniani, hasa katika kipindi cha baada ya janga la UVIKO-19 na mabadiliko ya kiuchumi yaliyoshuhudiwa katika miaka ya karibuni. Alisema Benki ya CRDB imeona fursa ya kimkakati ya kuunganisha wafanyabiashara na wawekezaji kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Afrika Mashariki.
“Benki ya CRDB kwa miaka mingi imekuwa mdau muhimu katika kuwezesha biashara na uwekezaji Tanzania na Afrika Mashariki, hususan Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,” alisema Bw. Nsekela. “Ofisi ya Dubai inalenga kuimarisha daraja hili la kifedha kati ya Mashariki ya Kati na Afrika Mashariki.”
Nsekela alieleza kuwa Benki inajivunia hatua hii kubwa ambayo inaleta mchango chanya kwa uchumi wa Tanzania na ukanda mzima wa Afrika Mashariki. Alitoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania kwa sera bora zilizowezesha hatua hiyo, na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa sera zake nzuri za diplomasia ya uchumi zilizoimarisha mazingira ya uwekezaji na ushirikiano kimataifa.
Aidha, aliishukuru Ubalozi wa Tanzania UAE, Benki Kuu ya Tanzania, Malamka ya Usimamizi wa Huduma za Fedha Dubai (DFSA), pamoja na Kituo cha Kimataifa cha Huduma za Fedha Dubai (DIFC) ambapo ofisi hizo zipo, kwa ushirikiano wao katika kufanikisha kuanzishwa kwa ofisi hiyo.
Akizungumza kuhusu fursa za kiuchumi, Nsekela alisema thamani ya biashara kati ya Tanzania na UAE sasa imezidi dola za Marekani bilioni 2.2, jambo linaloonesha nafasi kubwa ya kuvutia mitaji na uwekezaji zaidi.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji kutumia Ofisi ya Uwakilishi ya Benki ya CRDB Dubai kama lango la kupata huduma za kifedha, ushauri wa uwekezaji, na kuunganishwa na fursa mbalimbali nchini Tanzania na Afrika Mashariki, pamoja na Falme za Kiarabu.
Nsekela aliongeza kuwa pamoja na kuvuka mipaka hadi nje ya bara la Afrika, Benki hiyo itaendelea na mkakati wake wa kupanua wigo wa huduma zake katika nchi za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, na bara la Afrika kwa ujumla.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa (kulia), na Mkurugenzi Mwakilishi wa Benki ya CRDB Dubai, Jackson Kehengu alipotembelea Ofisi ya Uwakilishi ya Benki ya CRDB Dubai ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uzinduzi rasmi wa ofisi hiyo unaotarajiwa kufanyika mapema mwezi huu.







No comments:
Post a Comment