JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Benki ya Absa Tanzania Yazindua Ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika 2025, ikionesha Maendeleo ya Tanzania na Vipaumbele vya Mageuzi ya Kiuchumi.

Share This


Benki ya Absa Tanzania Tanzania imezindua rasmi ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika 2025 kwa Tanzania katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam Leo.

 Hafla hiyo imewakutanisha watunga sera wakuu, wasimamizi wa sekta ya fedha, viongozi wa taasisi za kifedha pamoja na wakurugenzi wa mashirika ya umma na binafsi kujadili hali ya masoko ya fedha barani Afrika na nafasi ya Tanzania katika taswira hiyo.
 Mgeni Rasmi katika hafla hiyo alikuwa Bw. Emmanuel Akaro, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), aliyemwakilisha Mheshimiwa Emmanuel Tutuba, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.

 Uzinduzi wa ripoti hiyo pia ulihudhuriwa na wadau kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Wizara ya Fedha, Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), viongozi wa sekta ya umma na binafsi, Bodi na Wakurugenzi na Menejimenti ya Juu ya Absa Bank Tanzania pamoja na wawakilishi wa vyombo vya habari.

 Sasa ikiwa katika mwaka wake wa tisa, Ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika, hutumika kama kipimo cha maendeleo ya masoko ya fedha katika nchi 29 za Afrika, zinazowakilisha takribani asilimia 80 ya idadi ya watu na Pato la Taifa (GDP) la bara la Afrika. Ripoti hiyo huandaliwa kwa ushirikiano na Official Monetary and Financial Institutions Forum (OMFIF) na kuungwa mkono na Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA).

 Tathmini hufanywa kwa kuzingatia nguzo sita kuu zikiwemo kina cha soko, upatikanaji wa fedha za kigeni, uwazi wa soko, maendeleo ya mifuko ya pensheni, mazingira ya uchumi jumla na utekelezwaji wa mifumo ya kisheria.

 Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser, alisisitiza umuhimu wa masoko ya fedha imara na yenye uwazi katika kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi.

 “Ripoti ya Afrika ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika ilianzishwa ili kutoa tathmini huru na ya kitaalamu kuhusu mwelekeo wa masoko ya fedha barani Afrika,” alisema Bw. Laiser.

  “Kadri uchumi wa Afrika unavyoendelea kukua na kubadilika, masoko ya fedha yaliyo na kina, uwazi na ufanisi ni muhimu katika kukusanya mitaji, kusaidia biashara na kuwezesha maendeleo endelevu.”

 Wakati wa uwasilishaji wa matokeo ya Ripoti ya 2025, wasemaji wakuu kutoka Absa Group walibainisha kuwa, licha ya changamoto za uchumi wa dunia, masoko mengi ya fedha barani Afrika yameonesha maendeleo ya kutia moyo. Mageuzi katika uwazi, mifumo ya udhibiti, utofauti wa bidhaa za kifedha na ubunifu wa kidijitali yalitajwa kuwa nguzo muhimu za kuimarisha ustahimilivu wa masoko.

 Akizindua ripoti hiyo, Bw. Emmanuel Akaro aliipongeza ripoti hiyo kama chombo muhimu cha kutathmini sera na kupima maendeleo, huku akirejea nafasi ya Tanzania kama ilivyoainishwa kwenye ripoti hiyo.

 “Ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika, inatoa mwanga muhimu kuhusu hatua ambazo Tanzania imepiga katika kuimarisha masoko yake ya fedha,” alisema Bw. Akaro.

 “Ripoti inaonesha maeneo ambayo tumefanya vizuri, hususan katika uthabiti wa uchumi jumla na uwazi, lakini pia inaainisha wazi maeneo yanayohitaji maboresho zaidi, ikiwemo kuongeza ushiriki wa wawekezaji wa ndani, kuendeleza mifuko ya pensheni, na kuimarisha mifumo ya kisheria na taasisi.”

 Bw. Akaro alisisitiza dhamira ya Serikali, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendelea kutekeleza mageuzi yatakayoongeza kina cha masoko, kupanua wigo wa vyombo vya kifedha na kuifanya mifumo ya fedha ya Tanzania kuendana na viwango vya kimataifa.

 Kwa upande wake, Mkurugenzi Bi. Lulu Ngwanakilala, akimwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Absa Tanzania, Bw. Paul Makanza, aliipongeza mijadala yenye tija na ushiriki mkubwa wa wadau.

 “Mijadala ya leo inaonesha kukomaa kwa mazungumzo kuhusu maendeleo ya masoko ya fedha nchini Tanzania,” alisema Bi. Ngwanakilala.

  “Ingawa Ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika 2025 inaonesha kuwa hatua zimepigwa, pia inatukumbusha umuhimu wa ushirikiano endelevu kati ya serikali, wasimamizi, taasisi za kifedha na sekta binafsi ili kuziba pengo lililobaki na kujenga masoko ya fedha jumuishi zaidi.”

 Alithibitisha dhamira ya Benki ya Absa Tanzania ya kuendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wote katika kusaidia mageuzi yanayokuza uwazi, uimara na uwekezaji wa muda mrefu katika sekta ya fedha.

 Hafla hiyo ilihitimishwa kwa mjadala wa jopo uliosimamiwa vyema, ukiwahusisha wawakilishi kutoka Absa Group, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) pamoja na Jubilee Life Insurance. Jopo hilo lilijadili njia za vitendo za kuharakisha maendeleo ya masoko ya fedha nchini Tanzania kwa kuzingatia mapendekezo ya Ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika.
Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Akaro (wa tatu kushoto), na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser (wa nne kushoto), wakiwa pamoja na viongozi wakuu wa Absa, wakionesha ripoti ya Absa ya Viashiria vya  Masoko ya Fedha Afrika 2025,iliyozinduliwa jijini Dar es Salaam leo. Kutoka kushoto: Mchumi Mkuu wa Absa Group, Bw. Geff Gable; Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Absa Tanzania, Bi. Lulu Ng’wanakilala; Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Irene Rwegalulira; na Mkuu wa Kanda wa Uendeshaji wa Masoko wa Absa Africa, Bw. Anthony Kivui.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Africa 2025 uliofanyika jijini Dar es Salaam leo
Mchumi Mkuu wa Absa Group, Bw. Geff Gable, akihutubia washiriki wakati  wa uzinduzi rasmi wa ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Africka 2025 uliofanyika jijini Dar es Salaam leo
Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Akaro, akitoa hotuba ya uzinduzi rasmi wa ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika 2025 jijini Dar es Salaam leoPicha ya siku: Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Akaro, akipiga picha ya kumbukumbu pamoja na viongozi wa Benki ya Absa na wageni waalikwa baada ya uzinduzi rasmi wa ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika 2025 uliofanyika jijini Dar es Salaam leo. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad