JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Waziri Sangu Asifia Mafanikio ya NSSF na Ufanisi wa TEHAMA

Share This

*Ni wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Waziri Sangu katika Ofisi za NSSF, Dodoma

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana tangu Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilipoingia madarakani.

Alisema mafanikio hayo yamepatikana kuanzia Machi 2021 hadi Septemba 2025, ambapo idadi ya wanachama wachangiaji imeongezeka kutoka 849,886 hadi kufikia milioni 1.7, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 100. Idadi ya waajiri pia imeongezeka kutoka 32,073 hadi 49,060, sawa na ongezeko la asilimia 52.9.

Mhe. Sangu alisema pia kuwa makusanyo ya michango yameongezeka kutoka trilioni 1.17 hadi trilioni 2.72, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 130. Mapato yatokanayo na uwekezaji yameongezeka kutoka bilioni 269.68 mwaka 2021 hadi zaidi ya bilioni 500, huku thamani ya jumla ya uwekezaji ikipanda kutoka trilioni 1.4 hadi trilioni 8.3 kufikia Juni 2025.

Aidha, malipo ya mafao kwa mwezi yameongezeka kutoka bilioni 49.53 hadi bilioni 78.51, sawa na ongezeko la asilimia 58.1. Waziri Sangu alitoa pongezi kwa NSSF kwa ufanisi katika matumizi ya TEHAMA, ambayo sasa yamefikia asilimia 98, akisisitiza kuwa teknolojia hii inarahisisha utoaji huduma kwa wanachama na wadau.

Alisema kuwa mipango mbalimbali ya NSSF inazingatia Dira ya 2050 na Ilani ya Uchaguzi ya CCM, huku akihimiza Mfuko kufikia wananchi waliojiajiri ili kujiwekea akiba na kupata huduma za hifadhi ya jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, amesema mafanikio haya yametokana na jitihada za Serikali kuboresha mazingira ya ajira na uwekezaji pamoja na mikakati ya Mfuko kuwafikia waajiri wa sekta binafsi na wananchi waliojiajiri.

Bw. Mshomba aliongeza kuwa thamani ya jumla ya Mfuko imefikia trilioni 10, kutokana na hesabu ambazo hazijakaguliwa, kutoka trilioni 4.8 mwaka 2021, na kwamba mafanikio haya yanaonesha jinsi jitihada za Serikali na mikakati thabiti ya Mfuko zinavyolisaidia taifa, kuimarisha ustawi wa wanachama, na kuhamasisha uwekezaji.

























No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad