JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Majibu ya upotoshaji kuhusu maendeleo ya Tanzania

Share This

 Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uswidi, Benjamin Dousa, tarehe 5 Desemba, alitangaza uamuzi wa Serikali ya Uswidi kufuta misaada kwa nchi tano za Tanzania, Msumbiji, Zimbabwe, Liberia na Bolivia baada ya kupitia vipaumbele vya kisera na changamoto za kiusalama.

Hata hivyo, wakati akitoa tangazo hilo, alizisakama nchi hizo kwamba zimekwama katika ujamaa na kushindwa kuendelea. Balozi wa Tanzania nchini Uswidi, Mhe. Mobhare Matinyi, anajibu kwa kuelezea mafanikio ambayo Tanzania imefikia katika maendeleo ya uchumi kwa miaka 60 iliyopita.

Hii ni tafsiri ya makala hii iliyochapishwa tarehe 16 Desemba, 2025, kwenye gazeti la Aftonbladet kwa lugha ya Kiswidi.




Na Balozi Mobhare Matinyi

Serikali ya Uswidi tarehe 5 Desemba, baada ya kupitia vipaumbele vyake vya sera za mambo ya nje na changamoto za kiusalama, ilitangaza uamuzi wa kufuta misaada yake ya ushirikiano wa maendeleo na nchi tano kabla ya mwisho wa mwaka 2026, na hivyo kuhitimisha misaada iliyodumu kwa miongo kadhaa.

Moja ya nchi zilizoathiriwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nchi ambayo imedumisha uhusiano mzuri na Uswidi tangia miaka 62 iliyopita. Kufanana katika itikadi ya demokrasia ya kijamii kati ya nchi hizi mbili ndiko kulikozaa uhusiano huu wa kipekee. Waumini wa demokrasia ya kijamii huamini katika haki ya kijamii, uhuru, usawa, utu wa binadamu na mshikamano ndani ya mfumo wa demokrasia unaoruhusu serikali kuingilia ubepari ili kuwezesha ustawi wa jamii.

Hata hivyo, wakati Uswidi ikiwa na demokrasia ya vyama vingi na kujali ustawi katikati ya ubepari, Tanzania ilichagua kufuata mfumo wa demokrasia ya chama kimoja kinachofuata Ujamaa wa Kiafrika ambayo ilisisitiza kujitegemea. Uswidi hivyo basi, ikachukua jukumu la kuwa mkufunzi wa harakati za vyama vya ushirika kwa Tanzania wakati huo.

Nchi hizo mbili zilikuwa zikitofautiana katika maendeleo ya kiuchumi kwa kiasi kikubwa kwani Uswidi iliyokuwa na watu milioni 7.5, ilikuwa na Pato la Taifa la dola za Marekani bilioni 17.33 mwaka 1961, huku ikiendesha uchumi imara wa viwanda wakati Tanzania iliyokuwa na watu milioni 10.3 ilikuwa na Pato la Taifa la dola za Marekani bilioni 2.83 huku ikitegemea zaidi uchumi wa kilimo.

Kwa hiyo Uswidi, mwaka 1963, iliona umuhimu wa kuiunga mkono Tanzania, wakati huo Tanganyika kabla ya kuungana na Zanzibar mwaka 1964 na kuunda Tanzania, kwa sababu nchi hiyo mpya ilikuwa imeonyesha dira makini ya maendeleo chini ya Rais Julius Nyerere.

Tangazo la hivi majuzi la Serikali ya Uswidi, bila kukusudia, liliibua simulizi iliyoipotosha taswira ya Tanzania na mafanikio yote ya ushirikiano huu wa fahari. Ilidaiwa kuwa nchi zilizotajwa "zimekuwa zikifuata Ujamaa mno" kwa miongo mingi na matokeo yake "hazijaendelea".

Niseme wazi vizuri kabisa: Kauli hiyo haiendani na Tanzania kwa namna yoyote ile, hata kwa fikra tu.

Hebu tuangalie ukweli: Mwanzoni mwa miaka ya 1960 Tanzania ilikuwa na chuo kikuu kishiriki kimoja tu, lakini leo ina vyuo vikuu 36 vilivyosajiliwa na vyuo vikuu vishiriki 16. Uswidi, kwa upande wake, leo ina vyuo vikuu 18 vilivyosajiliwa na vyuo vikuu vishiriki 12. Kwa hakika, ikiwa na takribani watu milioni 70, Tanzania bado inahitaji vyuo vikuu zaidi ikilinganishwa na Uswidi yenye milioni 10.7.

Wakati huo Tanzania ilikuwa na vituo kutolea huduma za afya 1,343 zikiwemo hospitali 96 na vituo vya afya 22. Leo Tanzania ina vituo vya aina zote vya kutolea huduma za afya 13,606 zikiwemo hospitali 473 na vituo vya afya 1,348. Tunashukuru kwa ushirikiano kati ya Hospitali ya Chuo Kikuu cha Karolinska ya jijini Stockholm na Hospitali ya Taifa Muhimbili iliyo pamoja na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili.

Tanzania ilianza na uwanja wa ndege wa kimataifa mmoja jijini Dar es Salaam lakini imeongeza viwanja viwili Kilimanjaro na Zanzibar na vingine viwili Dodoma na Mwanza vikiendelea kujengwa. Nayo Uswidi ina viwanja vya ndege vya kimataifa vikubwa zaidi huko Stockholm, Gothenburg na kidogo cha Malmo.

Ikiwa katika ukanda wa kimkakati wa mwambao wa Afrika Mashariki, Tanzania inahudumia nchi kadhaa zisizo na bandari kupitia bandari zake kuu nne za Dar es Salaam, Mtwara, Tanga na Zanzibar, na hivi karibuni itaanza ujenzi wa bandari kubwa ya Bagamoyo. Pia kuna bandari kadhaa kwenye maziwa makuu matatu ya Afrika, Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Mtandao mkubwa wa barabara na reli wa Tanzania ni miongoni mwa mitandao yenye ufanisi mkubwa barani Afrika na unaendelea kukua. Tunaipongeza Serikali ya Uswidi kwa kuunga mkono kwa njia mbalimbali mradi wetu wa reli ya kisasa (SGR), reli ya kwanza inayotumia umeme Afrika Mashariki na Kati. Kwa sasa reli hiyo inafanya kazi kati ya Dar es Salaam na mji mkuu Dodoma. Miradi zaidi ya reli katika maeneo ya kaskazini na kusini mwa nchi, ambayo kimsingi itaunganisha nchi zaidi na bahari ya Hindi, iko mbioni.

Baada ya miaka michache, Tanzania itakuwa kitovu kikubwa cha nishati baada ya kukamilisha mradi wa gesi asilia na kampuni ya Norway, Equinor, wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 42. Aidha, mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki linaloanzia Uganda hadi bandari ya Tanga unakaribia kukamilika.

Vilevile, Tanzania, ambayo inazalisha maelfu ya megawati za umeme kwa kutumia mitambo ya nguvu za maji, imejiandaa vizuri kutumia vyanzo vingine vya nishati mbadala kama jotoardhi, upepo na jua. Kadhalika, Tanzania ina akiba kubwa ya makaa ya mawe inayokadiriwa kufikia tani bilioni 1.9.

Mtazamo wa uchumi wa Tanzania pia ni wa kuvutia. Ingawa Pato lake la Taifa linakaribia dola bilioni 90, ukuaji wa uchumi kama inavyoshuhudiwa na Benki ya Dunia na Shirika la Mikopo ya Mauzo ya Nje la Uswidi (EKN) umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 5-7 kila mwaka tangu mwaka 2000. Nchi zingine zenye uchumi imara kama Uswidi, yenye Pato la Taifa la dola bilioni 630, imepata ukuaji hasi mara mbili ndani ya miaka mitano iliyopita.

Mnamo Julai 2020, Tanzania ilihitimu kutoka nchi za kipato cha chini na kuingia kwenye kundi la nchi za kipato cha kati, ambayo kwa mujibu wa Benki ya Dunia inaashiria maendeleo makubwa ya uchumi na utulivu kwa miongo miwili. Haya ni matunda ya mageuzi ya mwanzoni mwa miaka ya 1990 ambayo yaliipeleka nchi katika uchumi mchanganyiko, na mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, mchakato unaohitaji miongo kadhaa kukomaa.

Tanzania ilipokea korona za Uswidi milioni 560 mwaka 2024, takriban dola milioni 60 za Marekani, kama msaada kutoka Uswidi. Lakini Tanzania sasa inahama kutoka kwenye misaada kwenda kwenye biashara na uwekezaji; hivyo, inakaribisha wawekezaji wa Uswidi katika sekta muhimu kama viwanda, huduma, madini, utalii, kilimo na teknolojia.

Ni dhahiri kuwa, katika mwaka unaoishia Septemba 2025, Tanzania ilikusanya dola bilioni 4.43 kutokana na dhahabu, bidhaa inayoongoza kwa mauzo ya nje nchi, huku ikitarajia utalii utaleta dola bilioni 6.0 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025. Tanzania kwa sasa ndiyo nchi inayoongoza duniani kwa utalii wa mbugani kwa mwaka wa tatu mfululizo, ikijivunia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hifadhi ya Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na fuko maridadi za Zanzibar.

Tanzania ina hifadhi kubwa ya madini muhimu ikishika nafasi ya tatu barani Afrika na ya sita duniani. Ufini inatusaidia katika utafutaji na utafiti wa utajiri huu wa kipekee, ambao kwa hakika utainua uchumi wetu. Uswidi inahimizwa kutumia fursa za kujenga mitambo ya kuchenjua madini nchini.

Mwaka 2024 pekee, Tanzania ilivutia uwekezaji wa moja kwa moja wenye thamani ya dola bilioni 9.31 kutokana na miradi 901 iliyosajiliwa, na nchi hii inajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 140.

Pamoja na mafanikio haya, serikali ya sasa chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mikakati zaidi ili kuwaletea Watanzania maendeleo thabiti na endelevu.

Hivyo basi, kwa dhati kabisa, kwa uchumi wenye sekta nyingi na unaofuata soko huria huku ukionesha ukuaji stahimilivu wa kuvutia, kuibagaza Tanzania kwamba "imelowea kwenye Ujamaa usio na maendeleo" si sahihi na ni upotoshaji.

Mwandishi ni Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nchi za Nordic, Baltic na Ukraine, mwenye makazi yake Stockholm.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad