Farida Mangube, Morogoro.
Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Ndyamukama ametoa wito kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro, hususani wafanyabiashara, kuacha mara moja tabia ya kutupa taka kwenye mifereji ya maji, akisema kuwa kitendo hicho kinahatarisha usalama wa miundombinu na maisha ya wananchi hasa tunapoelekea kwenye msimu wa mvua.Amesema kutupa taka kwenye mifereji husababisha kuziba kwa njia za maji na kusababisha mafuriko ambayo huharibu barabara, nyumba na mali za watu pia maji yanapotuama huongeza hatari ya magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, homa ya matumbo na malaria.
Katika kipindi cha mvua mifereji iliyoziba pia husababisha maji kujaa barabarani na kuvuruga shughuli za kiuchumi hususani biashara ndogondogo zinazofanywa na wakazi wa maeneo yao
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Morogoro akiwemo Bi Asha Othuma na Robert Johnson wameishukuru TARURA kwa kuboresha mifereji katika mitaa yao, wakisema hatua hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la mafuriko lililokuwa sugu kwa miaka mingi.
“Tunaishukuru TARURA kwa kazi nzuri. Zamani maji yalikuwa yanaingia hadi kwenye nyumba zetu, lakini sasa mifereji imepanuliwa. Sisi kama wakazi tuna wajibu wa kuitunza.”
Kwa upande wake, mfanyabiashara mdogo katika Soko la Chifu Kingalu, Bw. Juma Said amekiri kuwa changamoto ya utupaji wa taka bado ipo, lakini amesema elimu zaidi inahitajika.
“Tukipewa elimu na kusimamiwa vizuri, wafanyabiashara wengi tutafuata sheria,” amesema.


No comments:
Post a Comment