Balozi wa Tanzania nchini Uswidi, Mhe. Mobhare Matinyi (wa nne kutoka kushoto mstari wa mbele), akiwa pamoja na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Raddy Energy ya Tanzania, Ramadhani Mlanzi (kulia kwake), katika picha ya pamoja na wawakilishi wa taasisi za fedha za Serikali ya Uswidi, kampuni ya Siemens Energy, Benki ya CRDB, Ubalozi na Raddy Energy, jijini Stockholm, mara baada ya kikao kilichofanyika siku chache zilizopita kukamilisha mchakato wa ununuzi wa mitambo minne ya kuzalisha umeme wa gesi itakayoletwa nchini ili kuimarisha uzalishaji wa umeme nchini.
Kikao cha pamoja baina ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uswidi, kampuni ya Raddy Energy, Benki ya CRDB na wawakilishi wa taasisi za fedha za Serikali ya Uswidi wakiendelea na kikao jijini Stockholm, hivi karibuni.BALOZI wa Tanzania nchini Uswidi, Mhe. Mobhare Matinyi (wa nne kutoka kushoto mstari wa mbele), akiwa pamoja na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Raddy Energy ya Tanzania, Ramadhani Mlanzi (kulia kwake), katika picha ya pamoja na wawakilishi wa taasisi za fedha za Serikali ya Uswidi, kampuni ya Siemens Energy, Benki ya CRDB, Ubalozi na Raddy Energy, jijini Stockholm, mara baada ya kikao kilichofanyika siku chache zilizopita kukamilisha mchakato wa ununuzi wa mitambo minne ya kuzalisha umeme wa gesi itakayoletwa nchini ili kuimarisha uzalishaji wa umeme nchini.
Kikao cha pamoja baina ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uswidi, kampuni ya Raddy Energy, Benki ya CRDB na wawakilishi wa taasisi za fedha za Serikali ya Uswidi wakiendelea na kikao jijini Stockholm, hivi karibuni.
Stockholm, Sweden Desemba 19, 2025: Kampuni ya Raddy Energy Solution Limited ya Tanzania imeingia makubaliano ya kununua mitambo minne ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia yenye jumla ya megawati 177 (MW) kutoka kampuni ya Siemens Energy ya Sweden kwa thamani ya dola za Marekani milioni 320, hatua inayotarajiwa kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, mitambo hiyo inatarajiwa kuwasili na kufungwa nchini Tanzania ifikapo mwishoni mwa mwaka 2027. Ununuzi huo umewezeshwa na Benki ya CRDB kama mshirika wa ndani katika uratibu na ufadhili wa mradi. Raddy Energy ni kampuni dada na Kiwanda cha Raddy Fibers kilichopo Mkuranga, mkoani Pwani.
Katika utekelezaji wa mradi, CRDB itashirikiana na taasisi za fedha za Serikali ya Sweden zikiwemo Wakala wa Mikopo ya Mauzo ya Nje wa Sweden (EKN), Shirika la Mikopo ya Mauzo ya Nje (SEK), Taasisi ya Fedha za Maendeleo ya Sweden (Swedfund), Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Sweden (SIDA) pamoja na Business Sweden. Taasisi hizi zote ni za serikali ya Sweden.
Aidha, Baraza la Kimataifa la Viwanda la Sweden (NIR) litakuwa sehemu ya timu ya ushauri wa kimataifa itakayouendesha mradi huo. Raddy Energy imesema mpango huu ni mwanzo wa safari kubwa, ambapo kampuni inalenga kufikisha uzalishaji wa umeme hadi MW 1,000 ifikapo mwaka 2030, ili kukidhi mahitaji ya ndani na kuwezesha uuzaji wa umeme nje ya nchi.
Katika kuimarisha makubaliano hayo, watendaji wa Raddy Energy walifanya ziara ya kimkakati nchini Sweden kuanzia Desemba 10–13, 2025, chini ya uratibu wa Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden. Ujumbe huo ulikutana na watendaji wa Siemens Energy na taasisi za fedha za serikali ya Sweden katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje, Stockholm, kabla ya kuzuru makao makuu ya Siemens mjini Finspäng.
Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, huku Raddy Energy ikiwakilishwa na Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Ramadhan Hassan Mlanzi, pamoja na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara na Miradi, Bw. Ediphine Masase. Timu ya CRDB iliongozwa na Bw. Musa Lwila, ikijumuisha Bw. Saidi Salehe na Bw. Andrew Mbunda.
Kwa upande wa Siemens Energy, kikao hicho kilihusisha Mkurugenzi wa Ufadhili wa Miradi, Bw. Joakim Tornberg, na Meneja Mwandamizi wa Mauzo, Bi. Christiane Carlsson, huku timu ya Serikali ya Sweden ikiongozwa na Mshauri Mwandamizi wa Biashara na Uendelezaji kwa Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Bi. Pia Roed. Wawakilishi wengine walitoka Business Sweden, SIDA, Swedfund, EKN, SEK na NIR.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Balozi Matinyi alieleza mwelekeo wa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Sweden, akisisitiza kuwa Tanzania ina fursa kubwa katika sekta za nishati, madini, viwanda, kilimo cha biashara, usafirishaji, utalii, teknolojia na ubunifu.
Mradi huo unatajwa kuwa miongoni mwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati, unaotarajiwa kuongeza uzalishaji wa umeme, kuchochea viwanda, kuimarisha ajira na kuisogeza Tanzania katika lengo la kuwa kitovu cha nishati ya uhakika katika ukanda.
Imetolewa na:
Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Sweden
Stockholm, 19 Desemba 2025



No comments:
Post a Comment