NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko amezindua Mfuko wa Mikopo nafuu kwa ajili ya kubiasharisha bunifu unaotambulika kwa jina la Samia Fund huku akielekeza kufanyika kwa bunifu na tafiti zaidi ili kutatua changamoto changamoto zinazoikabili jamii.
Amesema matatizo yaliyopo yanaweza kutatuliwa kwa tafiti za kisayansi na kwamba serikali itaendea kuwatambua na kuwaendeleza watafiti ili kutoa majibu ya matatizo.
Akifungua kongamano la tisa la sayansi, teknolojia na ubunifu kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Biteko alisema kumekuwa na kasi ya ukuaji wa sayansi na teknolojia hivyo, wanahitaji kuwa na mikakati ya kukuza na kuendeleza watafiti.
Alisema serikali ilitoa zaidi ya Sh bilioni 20 kwa ajili ya miradi ya utafiti katika sekta 20 ikiwemo kilimo.
Pia alisema mwaka 2015 hadi 2022, walitoa zaidi ya Sh bilioni 200 kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali.
"Kuna miradi mbalimbali ikiwemo ya HEET ambayo inaleta mageuzi katika elimu ya juu na utachagiza maendeleo," alisema.
Aliongeza kuwa "Ajenda iliyopewa msukumo mkubwa hapa Tanzania ni sayansi, ubunifu na tafiti kwa lengo la kupata majibu ya matatizo yaliyopo au kukabiliana na matatizo ambayo yatatokea."
Biteko alisema matatizo katika jamii yatatuliwa na sayansi na tafiti za kina na kwa kupitia mfuko huo, itaongeza ubunifu na kukuza soko la ajira.
"Lazima tutumie ubunifu kutatua changamoto, bila tafiti hakuna uendelevu vyote vinategemea sayansi na teknolojia," alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk Amos Nungu alisema changamoto iliyopo ni bado idadi ya watafiti haikidhi mahitaji hivyo, serikali ya Norway imefadhili Sh bilioni 6.3 kwa ajili ya watafiti.
Alisema Costech imetoa vibali 1,000kwa watafiti wa ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia faragha, haki ya wanyama na maadili ya kijamii.
"Norway imefadhili utafiti wa mabadiliko ya tabia nchi. Jitihada mbalimbali zimefanywa na watafiti ikiwemo uhawilishaji teknolojia ya kilimo, kuanzisha maabara ya mawe na kuwa na vifaa vya uhakiki ubora kwa wasindikaji wa zabibu," alieleza Dk Nungu.
Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema wameanzisha mfuko huo ili kubiasharisha bunifu na kuwezesha wabunifu kupata mikopo ya kuendeleza kazi zao za kibunifu.
Alisema serikali ya Norway pia imetoa Sh bilioni 6.3 kwa ajili ya watafiti 19 ambao watafanya utafiti katika maeneo mbalimbali.
No comments:
Post a Comment