JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


RAIS WA ZANZIBAR AMEWASISITIZA MABALOZI KUTANGAZA UTALII WA ZANZIBAR KIMATAIFA

Share This

 



RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewasisitiza Mabalozi wa Nchi za Afrika wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania, kuimarisha ushirikiano na fursa za kiuchumi pamoja na kuutangaza Utalii wa Zanzibar Kimataifa.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo alipozungumza na mabalozi hao waliofika Ikulu baada ya kumaliza ziara yao ya siku tatu kuitembelea Zanzibar kuangalia fursa za uwekezaji na maeneo ya ushirikiano ambayo nchi hizo za Afrika zinaweza kufanyakazi kwa pamoja na Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi amesema wakati umefika kwa nchi za Afrika kuungana mkono na kuzitumia rasilimali tulizonazo kuinua Uchumi wetu, kubadilishana uzoefu ili kufikia maendeleo.

Alisema, Zanzibar ina utajiri mkubwa wa viungo na fukwe nyeupe zenye kuvutia na kuwasisistiza kuwa mabalozi wa utali wa Zanzibar na kuitangaza ili watalii kutoka katika nchi zao kuja kutalii Zanzibar.

Dk. Mwinyi amewaeleza mabalozi hao kuangalia fursa za ushirikiano na uwekezaji hasa katika sekta za utalii, Usafiri wa bahari na usafirishaji, Uvuvi na ufugaji wa vifaranga vya Samaki, Mafuta na Gesi na kilimo cha viungo ambacho Zanzibar kina utajiri mkubwa.

Kuhusu sekta ya utalii, Dk. Mwinyi ameuelezea ni tegemeo kwa uchumi wa nchi unaochangia asilimia 30 ya pato la taifa mbali na kutangaza utalii wa fukwe na Urithi lakini pia aliwataka mabalozi hao kuangalia fursa mpya za utalii wa mikutano na uwekezaji ili kuitangaza zaidi Zanzibar iingize watalii wengi kutoka maeneo mengine ya dunia.

Akizungumzia Sekta ya usafiri wa bahari na usafirishaji, amewaeleza mabalozi hao kuangalia fursa zinazopatikana kwenye Sekta hiyo kwa kuziunganisha nchi za Afrika zilizo katika ukanda wa bahari ya Hindi kwani kwa pamoja nchi hizo zinauwezo wa kufanya biashara kubwa iwapo sekta hiyo itaimarishwa.

Kuhusu sekta ya Uvuvi na ufugaji wa Samaki Rais Dk. Mwinyi aliwataka mabalozi hao kuiungamkono Zanzibar na kuipatia uzoefu uliopo kwenye nchi zao ili inufaike na uzalishaji wa bidhaa za baharini.

Akizungumzia suala la Mafuta na Gesi amewaeleza mabalozi hao kwamba Zanzibar imebaini kuwa na kiwango kikubwa cha gesi na tayari imeanza mchakato wa kugawa vitalu kwaajili ya kuvuna rasilimali hiyo.

Amesema, ili kuimarisha sekta ya utalii iendelee kufanya vizuri zaidi, Serikali inaendeleza juhudi za kuendeleza ujenzi wa miundombinu ikiwemo viwanja vya ndege Unguja na Pemba, bandari na barabara za kisasa ili kurahisisha sekta ya usafirishaji na kuwavutia wageni wanaoingia nchini.

Wakizungumza kwenye hafla hiyo mabalozi hao wamesifu mabadiliko makubwa ya maendeleo katika kipindi kifupi cha uongozi wa Rais Dk. Mwinyi, husuasa kwenye ujenzi wa Miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na bandari pamoja na hali ya amani na utulivu uliopo nchini.

Balozi kiongozi wa ujumbe huo, Dk. Ahamada El Badaoui Mohamed amesema wakati umefika kwa balozi za Afrika kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali hasa ya kiuchumi.

Pia, ameielezea Zanzibar kuwa na fursa nyingi zinazoweza kutumiwa na nchi za Afrika kunufaika nazo kiuchumi na kumuhakikisha Rais Dk. Mwinyi wanakwenda kuutangaza utalii wa Zanzibar katika nchi zao na kuwa na ushirikiano wa maslahi ya pande zote.

Naye, Balozi wa Kenya nchini Tanzania Issack Jenga Nchi za Afrika zinaweza kuinuana na kushirikiana zenyewe kiuchumi, hatua itakayosaidia kukwepa misaada yenye masharti magumu kutoka kwenye nchi zilizoendelea.

Amesema watatumia fursa ya uwepo wao Zanzibar na kuutangaza utalii wa Zanzbad na kutimiza ndoto ya kuifanya Zanzibar kuwa kituo kikubwa cha utalii unaovuitia duniani.

Ujumbe huo wa mabalozi kutoka nchi za Burundi, Comoro, Kenya, Malawi, Misri, Morocco, Sudan, Rwanda, Uganda na Zambia, ulifika Ikulu ukiongozwa na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadha Soraga na watendaji wa wizara hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad