JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


ZAIDI YA WANANCHI 699 WILAYANI NAMTUMBO WAFIKIWA NA HUDUMA ZA UCHUNGUZI WA MAGONJWA YA MOYO NA SHINIKIZO LA DAMU

Share This

 Mbunge wa Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma Vita Kawawa kulia,akimsikiliza Mtakwimu kutoka Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) Loveness Msanga katikati kuhusu idadi ya wananchi waliojitokeza kwenye kambi za uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo zilizofanyika katika kituo cha afya Mputa wilayani Namtumbo,kushoto muuguzi kutoka taasisi hiyo Silvia Millanzi.


Na Mwandishi Wetu, Namtumbo
WATU 496 sawa na asilimia 71 kati ya watu 696 waliofanyiwa uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo kutoka vijiji mbalimbali katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, wamebainika kusumbuliwa na shinikizo la juu ya Damu.

Wagonjwa wenye matatizo ya mfumo wa chakula wenye uhusiano wa moja kwa moja na ugonjwa wa moyo ni asilimia 37na wagonjwa 222 sawa na asilimia 32 wamegundulika kuwa na matatizo ya kisukari.

Hayo yamesemwa jana na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) Dkt Baraka Ndelwa,wakati wa zoezi la awali la uchunguzi wa magonjwa ya moyo na shinikizo la damu lililofanyika katika kijiji cha Luhimbalilo kata ya Mputa wilayani Namtumbo.

Aidha alisema,wametoa rufaa kwa wagonjwa watano kwenda Hospitali ya Jakaya Kikwete kwa uchunguzi zaidi na wagonjwa wengine wamewapa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya mkoa Songea (Homso)na Hospitali ya St Joseph Peramiho.

Dkt Ndelwa alisema,katika zoezi hilo wamegundua watu wengi wanaugua magonjwa ya moyo na sukari, lakini wanashindwa kupata matibabu ya uhakika kutokana na upatikanaji wa matibabu ya kwenye ngazi ya zahanati na vituo vya afya kutokuwa rafiki.

Alisema,ugonjwa wa shinikizo la damu husababisha matatizo mbalimbali ikiwemo kiharusi,na moyo kushindwa kufanya kazi hali inayoweza kusababisha kifo kwa mgonjwa ambaye hajapata matibabu.

Dkt Ndelwa,ameshauri kuanzishwa kliniki maalum za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na shinikizo la damu kwenye vituo vya afya na Hospitali za wilaya, ili kuweza kuwafuatilia kwa karibu wananchi watakaobainika kupata ugonjwa huo,na kuwawezesha watoa huduma vifaa vya kisasa vya kutolea huduma kwa wagonjwa.

Ameiomba serikali,kupeleka dawa za magonjwa ya moyo na kisukari kwenye zahanati ili ziweze kuwasaidia wananchi wengi wenye matatizo hayo,badala ya kuishia kwenye Hospitali za rufaa za mkoa ambako upatikanaji wake ni rahisi.

Ameitaka jamii kuwa na utaratibu wa kupima mara kwa mara ili kufahamu afya zao,kwa sababu mtu akiwa na shinikizo la damu anaweza hasione dalili yeyote na anajihisi yuko vizuri,kwa hiyo kupima ndiyo njia sahihi ya kuweza kujitambua.

Muuguzi kutoka Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) Silvia Millanzi alisema,watu wengi waliojitokeza kwenye kambi za uchunguzi na matibabu katika kituo cha afya Lusewa,Hospitali ya wilaya Namtumbo na kituo cha afya Mputa wanafahamu hali za afya zao.

Hata hivyo,changamoto kubwa ni kutofuatilia matibabu kutokana na hali ya kiuchumi au upatikanaji wa dawa kwenye maeneo yao,jambo ambalo ni hatari kwa sababu mgonjwa asiyepata matibabu anaweza kupata magonjwa mengine hatari ikiwemo figo.

Millanzi,ameiomba jamii hasa watu wanaosumbuliwa na ugonjwa wa shikinikizo la damu,kuhakikisha wanazingatia maelekezo ya wataalam kuhusu umuhimu wa kutumia dawa hizo kila siku katika maisha yao, ili kuzuia madhara zaidi yanayoweza kutokea.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa,ameiomba serikali kuangalia upya mwongozo wake unaotaka dawa za shikinizo la damu(BP) na Kisukari zipatikane kwenye Hospitali za rufaa za mikoa na Hospitali kubwa ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

“hapa wataalam wetu wametuambia kuwa BP ikiwa juu inaweza kusababisha matatizo ya figo na watu wengi wa vijijini hawana uwezo wa kulipigia gharama ya kusafisha damu kila baada ya wiki moja,kwa hiyo njia pekee ni kuhakikisha dawa hizi zinapelekwa hadi kwenye ngazi ya zahanati,hatua hii itasaidia wagonjwa kuzipata kirahisi”alisema Kawawa.

Kawawa alisema,ni vema serikali ichukue hatua ya kufikisha dawa hizo kwenye zahanati,badala ya kuwaacha wananchi wakiteseka na kutumia gharama kubwa kwenda kufuata matibabu na wengine kupoteza maisha kwa kukosa huduma za haraka.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad