JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


MAKAMU WA RAIS AFANYA ZIARA WILAYA YA KASULU KIGOMA

Share This

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Kasulu mjini wakati akiwa ziarani mkoani Kigoma tarehe 12 Julai 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Nyakitonto wakati akiwa ziarani mkoani Kigoma tarehe 12 Julai 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka maafisa biashara kutokuwa kikwazo kwa wafanyabiashara wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Kasulu akiwa ziarani mkoani Kigoma mara baada ya kupokea malalamiko ya matumizi ya nguvu kupita kiasi wakati wa kuhamisha wafanyabiashara katika maeneo waliyokuwa wanatumia Wilayani hapo. Amesema suala la kutumia nguvu ikiwemo mabomu ya machozi kwa wananchi ambao hawana silaha ni kinyume na sheria na utaratibu.

Aidha ameagiza viongozi wa Halmashauri hususani maafisa biashara kuwaelimisha wananchi kuhusu oparesheni mbalimbali zinazotarajiwa kufanyika ili kuondoa taharuki wakati wa utekelezaji wake. Makamu wa Rais amekemea vitendo vya utozaji ushuru kwa mazao chini ya tani moja kwani serikali tayari ilipiga marufuku suala hilo.

Makamu wa Rais amesema serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Kigoma ikiwemo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kuunganisha mkoa huo na mikoa mingine. Amewasihi wananchi wa Kasulu na watumiaji wote wa barabara zinazojengwa kuzingatia matumizi salama ya barabara kwa kufuata sheria ili kuepusha madhara ya ajali ikiwemo vifo na majeruhi.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amezungumza na wananchi wa mji wa Makere ambapo amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kutumia sheria ndogo vema katika kudhibiti uharibifu wa mazingira. Amewahimiza viongozi wa dini na kimila kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na kudhibiti uchomaji moto kwenye misitu.

Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Maji kuhakikisha mita zinapatikana ndani ya miezi miwili ili kuwaunganishia huduma ya maji wananchi wa Makere. Amesema mji huo huduma ya maji ni toshelevu lakini wananchi wengi hawajaunganishwa na huduma hiyo sababu ya ukosefu wa mita.

Pia Makamu Rais amekemea tabia ya kuharibifu wa miundombinu ya maji na kuagiza watendaji kuwatafuta na kuwachukulia hatua wahalifu wote walioharibu miundombinu ya maji Wilayani Kibondo.

Makamu wa Rais amesema Serikali italipa fidia halali kwa waliochukuliwa mashamba ya nyakirigi katika upanuzi wa kambi ya wakimbizi nyarugusu.

Akiwa katika eneo la Nyakitonto, Makamu wa Rais ameagiza askari wa uhifadhi kuacha tabia ya kupiga na kuwanyanyasa raia ikiwemo kuchukua mazao yao pale wanapokutwa na makosa na badala yake wapelekwe katika vyombo vya sheria. Pia amewasihi wananchi wa eneo hilo kufuata sheria na makubaliano yaliyowekwa ikiwemo kutovamia maeneo ya hifadhi.

Ametoa rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kurekebisha sheria ndogo ambazo ni kandamizi kwa wananchi ikiwemo kutoza fedha za kadi za kliniki kwa kina mama pamoja na faini kwa wakina mama wanaojifungua watoto nyumbani.

Vilevile Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Wilaya ya Kasulu kujitokeza katika kutoa maoni yao katika Dira ya Taifa 2050 ili mawazo yao yaweze kutumika katika kuandaa Taifa la mika 25 ijayo.

Halikadhalika amewataka wananchi wa Kigoma kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa baadae mwaka huu kwa amani na utulivu.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi – TAMISEMI Mhe. Zainabu Katimba amewataka watumishi wanaotoa huduma za afya katika vituo vya afya na zahanati kuzingatia maadili na miongozo iliyowekwa. Amesema ni marufuku kwa mtumishi wa huduma za afya kumtoza mama mjamzito malipo ya kadi ya kliniki pamoja na faini kwa mama anayejifungua mtoto wake nyumbani bila kudhamiria.

Katimba amesema ni wajibu kwa watoa huduma za afya na serikali kwa ujumla kuelimisha wananchi faida na umuhimu wa kujifungua watoto katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
12 Julai 2024
Kigoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad