JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


DIRISHA LA KWANZA LA UDAHILI MWAKA WA MASOMO 2024/2025 LIMEFUNGULIWA RASMI

Share This
Katibu Mtendaji wa Tume ya vyuo vikuu nchini, Profesa Charles Kihampa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Julai 15, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akitangaza kufunguliwa kwa dirisha la udahili kwa waombaji wa shahada ya kwanza katika Taasisi za Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2024/2025

Na Karama Kenyunko Michuzi TV
TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua dirisha la maombi ya udahili kwa waombaji wa shahada ya kwanza wa mwaka wa masomo 2024/2025 kuanzia leo Julai 15, 2024 huku ikianisha sifa zinazohitajika kwa wanafunzi kusoma katika vyuo vikuu mbali mbali nchini.

Katibu Mtendaji wa TCU, Prof.Charles Kihampa amesema dirisha litakuwa wazi hadi Agosti 10 2024 na kuwahimiza waombaji wote wa udahili kuendelea kupata taarifa sahihi kupitia tovuti ya TCU au tovuti za Vyuo mbalimbli vinavyotoa elimu ya juu.

Waombaji wote wa udahili kwa mwaka wa masomo 2024/2025 wanatakiwa kuwa na sifa stahiki za kidato cha sita, sifa stahiki za Stashahada na Cheti cha awali.

"Maombi ya udahili wa kujiunga na Shahada ya kujiunga na shahada ya kwanza utahusu waombaji waliohitimu wa kidato cha sita, wenye Stashahada (Ordinary Diploma), na wenye sifa swahili za cheti cha awali (Foundation Certificate) ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Ili kufahamu sifa stahiki za kujiunga na Chuo Kikuu waombaji wameelekezwa kusoma vigezo vilivyopo kwenye vitabu vya muongozo vya TCU huku pia wakitakiwa kutuma maombi yao moja kwa moja kwenye vyuo ambavyo wamevichagua na kwamba maelekezo ya jinsi ya kutuma maombi yanayotolewa na vyuo vikuu husika.

Aidha Prof. Kihampa amewapa tahadhari waombaji wote wa shahada ya kwanza ikiwa watahitaji kupata ufafanuzi wa suala lolote juu ya udahili kuwasiliana moja kwa moja na vyuo vikuu husika ama TCU.

"Tunawaasa wananchi kuepuka kupotoshwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini" amesema Prof. Kihampa.

Amesema masuala muhimu ambayo waombaji wanapaswa kuzingatia ni pamoja na kusoma kwa makini mwongozo wa udahili uliotolewa na TCU pamoja na maelekezo mahususi ya vyuo kabla ya kuanza kutuma maombi ya udahili.

"Waombaji wenye vyeti vilivyotolewa na mabaraza ya mitihani nje ya nchi wanapaswa kuwasilisha vyeti vyao katika Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA)Ili kuweza kupata ulinganifu na matokeo yao yaweze kupatikana kwenye mfumo.

Mambo mengine muhimu ni kuingia kwenye tovuti za vyuo ili kujua taratibu za kutuma maombi, kupata taarifa za kina kuhusu programu za masomo na kutuma maombi moja kwa moja vyuoni kupitia mifumo ya kielektoniki na kuwasiliana na vyuo ili kupata taarifa huku pia waombaji wenye vyeti vinavyotolewa na NECTA au NACTE wakitakiwa kupata idhibati ya ulinganifu wa sifa zao kabla ya kutuma maombi ya udahili.

Aidha Tume imewahimiza waombaji wote wa udahili kuendelea kupata taarifa sahihi kupitia tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz) na tovuti za vyuo vilivyoruhusiwa kudahili wanafunzi wa shahada ya kwanza.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad