JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


CMSA YATOA HATI ZA UWEKEZAJI KATIKA HATIFUNGANI YA PREMIER SUKUK LIMITED

Share This

 Na Mwandishi Wetu


MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imetoa hati za uwekezaji katika hatifungani ya Premier Sukuk Limited kwa lengo la kupata fedha kwa ajili ya kupata fedha za kutekeleza shughuli za kuboresha miundombinu ya Hospitali ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Premier.

Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa hati za uwekezaji katika hatifungani ya Premier Sukuk Limited,Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo CPA Nicodemus Mkama amesema tukio hilo ni la kihistoria katika ustawi na maendeleo ya sekta ya fedha, hususan masoko ya mitaji hapa nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara.

"Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ina jukumu la kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba shughuli katika masoko ya mitaji zinafanyika kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo ili kuleta uwazi na haki kwa washiriki wote.

"Masoko ya mitaji yanawezesha upatikanaji wa rasilimali fedha za muda mrefu, kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo.Fedha hupatikana kutoka kwa wawekezaji, ambao ni watu binafsi, taasisi na kampuni na hatimaye fedha hizo huwekezwa katika sekta za uzalishaji na hivyo kuchochea ustawi na maendeleo ya uchumi."

CPA Mkama amesema Machi 22 mwaka huu CMSA iliidhinisha maombi ya Kampuni ya Premier Sukuk Limited kuuza hatifungani inayokidhi misingi ya Shariah yaani Premier Corporate Sukuk yenye thamani ya Sh.bilioni 1.2 kwa ajili ya kupata fedha za kutekeleza shughuli za kuboresha miundombinu ya Hospitali ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Premier, ambayo inatoa huduma kwa wanafunzi wa shule, walimu, wafanyakazi na wananchi wanaoishi maeneo ya jirani.

Ameongeza CMSA ilitoa idhini kwa hatifungani hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania; na Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya Utoaji wa Hatifungani za Sukuk kwa Kampuni na Taasisi za Umma.

Hivyo mauzo ya hatifungani ya Premier Sukuk yamekidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Taratibu za uuzaji wa Sukuk katika masoko ya mitaji huku akisisitiza mauzo ya hatifungani hiyo yalifunguliwa Aprili 1, 2024 na kufungwa Mei 30, 2024, ambapo Sh. bilioni 1.94 zimepatikana ikilinganishwa na Sh.bilioni 1.2 zilizotarajiwa kukusanywa, sawa na mafanikio ya asilimia 161.67.

"Mafanikio haya yametokana na imani ya wawekezaji kwa Kampuni ya Premier Sukuk na Imani katika masoko ya mitaji hapa nchini. Pia ni matokeo ya elimu ya uwekezaji inayoendelea kutolewa kwa umma na Serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana kwa kushirikiana na wadau katika sekta ya fedha.

"Mauzo ya hatifungani ya Premier Sukuk yanatoa mchango katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha wa 2020/21 2029/30 wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi ili kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu,"amesema CPA Mkama.

Ameongeza hatifungani hiyo pia, inawezesha utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwani fedha zilizopatikana zitatumika kutekeleza miradi muhimu kwa maendeleo ya jamii. Aidha, wananchi waliowekeza katika hatifungani hii watanufaika na faida itokanayo na miradi, hivyo kuinua vipato vyao.

Amefafanua Hatifungani ya Premier Sukuk imezingatia ubunifu unaojumuisha vipengele vinavyogusa maendeleo katika Sekta ya Elimu; ujenzi wa miundombinu ya huduma za Afya kwa wanafunzi wa shule, walimu, wafanyakazi na wananchi kwa ujumla; na utunzaji wa misingi ya maadili.

Pia inaweka msingi madhubuti wa kuonyesha njia kwa kampuni na taasisi katika sekta ya umma na binafsi namna ya kupata fedha za kugharamia miradi yenye uwezo wa kujiendesha kibiashara, kupitia masoko ya mitaji. 

Amesema utoaji wa hatifungani za Sukuk unafuata misingi ya maadili inayokataza: uwekezaji katika miradi kama vile uzalishaji wa vileo; kamali au michezo ya kubashiri; na shughuli zote zenye viwango vya juu vya vihatarishi. 

Aidha, misingi hiyo inahamasisha maadili mema kwa kuhakikisha kuwa uwekezaji unazingatia uwepo wa mali halisi na kwamba manufaa ya uwekezaji huo yanapaswa kugawanywa katika utaratibu unaotoa fursa linganifu za manufaa kwa wadau wote. 

Amesisitiza utoaji wa hatifungani za Sukuk umekuwa na mvuto mkubwa kwa wawekezaji ulimwenguni na umekuwa ukiongezeka kwa kiwango cha asilimia 15 hadi 20 kwa mwaka, ambapo mali zenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani trilioni 2 ziko katika mfumo huu wa uwekezaji chini ya taasisi za fedha zinazozingatia misingi ya Shariah.

Aidha amesema Hatifungani hizo zimewezesha kupatikana kwa mtaji wa jumla wa Shilingi Bilioni 79.32, ikilinganishwa na Shilingi Bilioni 49.2 zilizotarajiwa kukusanywa, sawa na mafanikio ya asilimia 161. 

"Mafanikio haya yametokana na mazingira wezeshi, shirikishi na endelevu ya kisera, kisheria na kiutendaji ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi madhubuti na maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan."









No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad