Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ametangaza mpango wa Serikali wa kupumzisha shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika kwa miezi mitatu ili kuwezesha samaki kuzaliana na kuongeza tija kwa wavuvi wanaofanya shughuli zao ziwani humo.
Waziri Ulega ametoa kauli ya serikali
kwa nyakati tofauti ambapo awali alitoa kauli hiyo akizungumza na wadau
wa uvuvi kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa Kigoma na baadaye kuzungumza na
wananchi na wadau wanaofanya shughuli za uvuvi kwenye Mwalo wa Katonga
Manispaa ya Kigoma Januari 9, 2024.
Akiwa kwenye kikao cha ndani
na wadau wa uvuvi Waziri Ulega alisema kuwa utekelezaji wa mpango huo
utaanza rasmi Mei 15 hadi Agosti 15 mwaka huu na hiyo ikiwa ni
Utekelezaji wa Mkataba wa Kikanda wa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya Ziwa
Tanganyika unaoweka hatua na taratibu za usimamizi endelevu wa shughuli
za uvuvi katika ziwa hilo.
Akieleza sababu ya maamuzi hayo
alisema ni kutokana na utafiti kubainisha kuwa kumekuwepo na upungufu
mkubwa wa samaki na dagaa katika ziwa Tanganyika kunakotokana na
ongezeko kubwa la uvuvi usio endelevu uliopelekea uharibifu wa mazalia
ya samaki.
"Pamoja na kufunga shughuli za uvuvi katika ziwa
Tanganyika, Serikali ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeanza
kutekeleza njia mbadala za kuwawezesha wananchi kujiendeleza kiuchumi
katika ziwa Tanganyika ikiwemo kukopesha vikundi maboti na vizimba kwa
ajili ya miradi ya ufugaji wa samaki na tayari imetenga shilingi milioni
200 kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) kubainisha maeneo
yanayofaa kwa ufugaji huo,' alisema Waziri Ulega
Aliongeza kuwa
Mhe. Rais, Dkt. Samia ametoa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuanzisha
kituo cha uzalishaji wa vifaranga vya samaki bora mkoani humo kwa ajili
ya kuwawezesha wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kuwa na uhakika
wa kupata vifaranga bora wakati wote.
Halikadhalika alifafanua
kuwa hatua hiyo ya kupumzisha ziwa sio jambo geni kwa sababu linafanyika
katika Mikoa ya ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi ambapo wanafunga
miamba kwa ajili ya uvuvi wa pweza na matokeo yameonesha kuwa wakati wa
kufungua tani takriban 100 zimekuwa zikipatikana.
Aidha, alitumia
nafasi hiyo pia kuwahimiza wananchi mkoani humo kuchangamkia fursa hiyo
ya mikopo ya vizimba na maboti ili waweze kujikwamua kiuchumi katika
nyakati hizo za upumzishaji wa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti
alisema kuwa mpango huo una manufaa makubwa kwa wananchi na taifa kwa
ujumla na ni muhimu kuharakisha utekelezaji wake ili kunusuru ziwa hilo
ambalo uzalishaji wake umeshuka sana.
Mnyeti alisema kuwa zipo
nchi duniani zimetekeleza mpango huo na faida kubwa imeonekana kwa
kuongeza mazao ya uvuvi, kuongeza mapato kwa wavuvi na serikali kwa
kiwango kikubwa.
Awali Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uvuvi Wizara
ya Mifugo na Uvuvi, Ambakisye Simtoe akiwasilisha hali ya uvuvi na wingi
wa samaki ziwa Tanganyika alisema kuwa umepungua na kwa sasa hali sio
nzuri.
Ambakisye alisema kuwa mwaka 1995 takwimu zilikuwa
zikionyesha kuwepo kwa wingi wa samaki tani 197,493 zinazoweza kuvuliwa
kwa mwaka ambapo kiwango hicho kimeshuka na kufikia tani 144,690. Pia,
uvuvi umeshuka kutoka tani 104,178 mwaka 2020 na kufikia tani 85,180.
Naye
Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira, Paul
Deogratius alisema kuwa mkataba mdogo wa nchi zinazozunguka ziwa
Tanganyika ibara ya saba wa mwaka 2021 unaitaka Tanzania kutekeleza
ulinzi na utunzaji wa rasilimali za ziwa Tanganyika ikiwemo shughuli za
uvuvi.
Deogratius alisema kuwa nchi za Burundi,Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo na Zambia zilitekeleza mkataba huo mwaka jana
isipokuwa Tanzania jambo ambalo halileti picha nzuri kwenye uhusiano na
ushirikiano wa kimataifa.
Wabunge wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Kilumbe
Ng'enda wa Kigoma Mjini na Mhe. Josephine Genzabuke wakizungumza kwenye
mkutano wa hadhara wa Waziri Ulega uliofanyika katika mwalo wa Katonga
wameunga mkono mpango huo wa serikali na kusema utaleta faida kubwa kwa
sekta ya uvuvi.
Miongoni mwa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya Ziwa
Tanganyika sambamba na Tanzania ni pamoja na Zambia, Burundi na Jamhuri
ya Demokrasia ya Congo ambao wao walishaanza kutekeleza zoezi hilo la
upumzishaji wa ziwa Mwaka jana (2023).


.jpeg)




No comments:
Post a Comment