JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


WAANDISHI DCPC WANOLEWA, TRA YAENDELEA KUTOA ELIMU YA MLIPA KODI

Share This

Afisa wa Usimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Hamad Mterry akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo ya elimu kwa Mlipa kodi yaliyofanyika leo Juni 6, 2023 katika Chuo Cha Kodi jijini dar es Salaam.Picha ya pamoja.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) leo Juni 6, 2023.



Waandishi wa habari wa chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) wakiwa katika Mafunzo yaliyotolewa na TRA leo Juni 6, 2023.


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA,) imekutana na kutoa Elimu kwa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) ikiwa ni mwendelezo wa kukutana na makundi mbalimbali na kutoa Elimu ya Mlipa kodi ili kuwezesha ukusanyaji wa kodi kwa ujenzi wa Taifa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo ya siku moja iliyofanyika katika chuo cha Kodi jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo amesema, Mamlaka hiyo imeendelea kuelimisha Umma juu ya masuala ya kodi na wataendelea kukutana na makundi mbalimbali ikiwemo wahasibu na wafanyabiashara kutoka nyanja mbalimbali ikiwa ni mkakati wa Mamlaka hiyo wa kuwafikia wananchi kote nchini na kutoa Elimu pamoja na kutatua changamoto.

Kayombo amesema, waandishi wa habari ni daraja kati Mamlaka hiyo na walipa kodi na ni waelimishaji kwa walipa kodi kupitia kalamu zao na wataendelea kukutana na waandishi wa habari katika mikoa mbalimbali nchini na kutoa elimu hiyo.

"Katika nyakati tofauti tunalipa kipaumbele kundi hili la waandishi wa habari kutokana na umuhimu wake katika kuelimisha umma, kupitia mafunzo haya kutakuwa na nafasi ya kujibu maswali na kufafanua masuala mbalimbali ya kikodi yaliyokuwa hayaeleweki pamoja na ufafanuzi wa kina kuhusu wajibu wa Mamlaka katika utekelezaji wa majukumu yake." Amesema.

Kuhusiana na jitihada za Mamlaka hiyo kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi Kayombo amesema, wameendelea kusogeza ofisi za TRA katika maeneo ya mbalimbali ya karibu na wananchi ili kuwafikia wateja wengi zaidi kwa ukaribu na kutoa huduma kwa ufanisi zaidi.

"Tumesogeza huduma katika maeneo mengi ya mbali hali inayorahisisha utoaji na upokeaji huduma na kumaliza wapigaji maarufu kama vishoka na tumeenda mbali zaidi kwa matumizi ya kidigitali katika utoaji huduma na wateja wanapongeza na kutumia njia hizo za kidigitali na tunapokea maoni ya kuboresha." Ameeleza.

Pia, ameeleza kuwa wanaendelea katika kuwekeza katika teknolojia ikiwemo kusajili TIN kwa njia ya mtandao, kufanya malipo na huduma kwa njia ya teknlojia ili kurahisisha na kufanya walipakodi kujihudumia.

"Kupitia mitandao ya kijamii tumekuwa tukipokea maoni na kuwahudumia wateja wetu pamoja na kupokea kero, changamoto na ushauri kwa maboresho zaidi." Amesema.

Aidha amesema malengo ya ukusanyaji kodi ya shilingi Trilioni 23.1 unaendelea vyema na kuwahimiza wananchi kulipa kodi na kujenga Taifa.

"Tulipe kodi kwa ujenzi wa Taifa letu kwa ushirikiano, kujiimarisha na kujitegemea kiuchumi ili kuepukana na masharti mengi kupitia misaada mbalimbali....Tulipe kodi ili Serikali iendelee kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo." Amesema.

Kwa upande wake Afisa wa Usimamizi wa Kodi Hamad Mterry amesema, TRA imeendelea kutoa elimu kwa mlipa kodi na Umma ikihusisha elimu ya haki na wajibu wa mlipakodi.

"Mlipakodi ana haki kufaidika na huduma bora kwa mujibu wa viwango vya huduma vilivyowekwa na TRA, pia mlipakodi ana haki ya kutobughudhiwa, kutishwa wala kuogopeshwa kwa namna yoyote wakati wa usimamizi wa utekelezaji sheria za Kodi, pia ana haki ya faragha na usiri wa taarifa za biashara yake pamoja na haki ya kupinga makadirio ya kodi." Amesema.

Aidha amesema, mlipakodi ana haki ya kuchukuliwa kwamba yeye ni mwaminifu hadi itakapothibitishwa vinginevyo.

Aidha amewakumbusha walipakodi wajibu wao ikiwemo kutoa ushirikiano kwa TRA pindi inapotekeleza majukumu yake, kujitokeza katika mafunzo ya taaluma ya masuala mbalimbali ya kodi na kampeni za kulipa kodi kwa hiari pamoja na kulipa kodi kwa wakati na kutoa risiti za Kodi kila anapouza bidhaa au huduma pamoja na kudai risiti za kodi kila anaponunua bidhaa au kunufaika na huduma iliyotolewa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad