WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
MAADHIMISHO YA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA JUNI 16, 2106
Tarehe 16 Juni ya kila mwaka, ni kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika. Katika siku hii, Tanzania inaungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Afrika kuadhimisha Siku hii kwa mujibu wa Azimio lililopitishwa na nchi 51 za Umoja huo mnamo mwaka 1990.
Azimio hili lilipitishwa kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya watoto wa shule yaliyofanyika katika kitongoji cha Soweto, Afrika ya Kusini tarehe 16 Juni, 1976. Katika tukio hilo la kusikitisha, inakadiriwa kuwa watoto wapatao 2,000 waliuawa kikatili na utawala ulioundwa na Serikali ya Makaburu. Watoto hawa walikuwa kwenye harakati za kudai haki yao ya msingi ya kutokubaguliwa kutokana na rangi yao.
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka 2016 yataadhimishwa katika ngazi ya Mikoa kwa kuzingatia taratibu za mikoa husika.
Lengo kuu la Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika tarehe 16 Juni, 2016, ni kuwa na siku maalum ya kuelimisha na kuwakumbusha wazazi, walezi na wadau mbalimbali kuitikia utekelezaji wa wajibu na majukumu yetu katika kuwapatia watoto haki zao za msingi. Haki hizi ni pamoja na haki ya kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kushiriki na kutobaguliwa. Katika siku hii watoto hupata nafasi maalum ya kujieleza, kusikilizwa, kushiriki na kuonyesha vipaji vyao mbele ya wazazi, walezi na jamii kwa ujumla.
Maadhimisho haya, huambatana na kaulimbiu ambayo inalenga kuhamasisha jamii kutatua changamoto wanazokabiliana nazo watoto wa Tanzania. Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika 2016 ni “Ubakaji na Ulawiti kwa Watoto Vinaepukika: Chukua Hatua Kumlinda Mtoto”.
Ni matarajio yangu kuwa kila mwananchi atashiriki maadhimisho haya kwa kuchukua hatua thabiti za kuwalinda watoto katika jamii zetu.
S. Nkinga
KATIBU MKUU
10/6/2016.
No comments:
Post a Comment