JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


VIJANA WATAKIWA KUWA WABUNIFU, WAJASIRIAMALI

Share This
  Mwanzilishi wa Chuo Kikuu cha Afrika Tanzania, Mchungaji Joshua Lee akisisitiza jambo wakati wa mafunzo ya  ujasiriamali na teknolojia jana jijini Dar es Salaam,  mafunzo hayo yaliyotayarishwa na chuo hicho kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Handong cha Korea na UNESCO.
Mkuu wa wilaya ya Temeke, Bi. Sophia Mjema (katikati) akiwa pamoja na Mwanzilishi wa Chuo Kikuu cha Afrika Tanzania, Mchungaji Joshua Lee (kulia) pamoja na mjumbe wa kamati ya chuo hicho, Bw. Gaudens Kayombo wakati wa mafunzo ya  ujasiriamali na teknolojia jana jijini Dar es Salaam. mafunzo hayo ilitayarishwa na chuo hicho kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Handong cha Korea na UNESCO.

Na Mwandishi wetu.
VIJANA watanzania wametakiwa kuwa na mawazo ya kibunifu na kijasiriamali, kuondokana na mawazo ya kuajiriwa ili kujiongezea kipato na kutoa mchango zaidi kwa taifa.

Akifungua semina ya mafunzo ya  ujasiriamali na teknolojia jana jijini Dar es Salaam, Mkuu wa wilaya ya Temeke, Bi. Sophia Mjema amesema ubunifu wa miradi ya ujasiriamali ni njia muhimu ya kuleta maendeleo endelevu kwa vijana na taifa.

“Mafunzo haya ni muhimu kwa vijana ili kuwapa ujuzi wa kubuni miradi ya kibiashara mahali walipo,” alisema na kuongeza kuwa jambo la msingi ni kujenga nidhamu ya fedha na kuheshimu mikopo.

Mafunzo hayo yalitayarishwa na Chuo Kikuu cha Afrika Tanzania kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Handong cha Korea na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia elimu, Sayansi na utamaduni (UNESCO) na kuhudhuriwa na wanafunzi pamoja na viongozi wa serikali za mitaa na vitongoji katika eneo la Kibada Kigamboni.

Mkuu wa Kitivo cha Uhandisi cha Chuo Kikuu cha Handong Global, Profesa Younsik Han alisema Tanzania imejaaliwa kuwa na ardhi kubwa, maliasili nyingi, amani na utulivu lakini bado ipo nyuma katika masuala ya kijasiriamali.

“Mafunzo ya ujasiriamali yanatakiwa zaidi na vyuo vihusike katika hili,” alisema.

Chuo Kikuu cha Afrika Tanzania kinachotoa programu za uhandisi na utawala kimeanza pia kuwafundisha wanafunzi wake maswala ya ujasiriamali.

Alifafanua kwamba chuo chake na Chuo Kikuu cha Afrika Tanzania wanataka kuwa na kituo kwa ajili ya kutoa maarifa ya teknolojia na ujasirimali.

“Tunataka kuunganisha mawazo ya kibunifu ya kijasiriamali ya wanafunzi na watu wa vijiji vya maeneo ya hapa karibu ili waweze kuanza biashara ndogo ndogo za uzalishaji,” alisema.

Mwanzilishi wa Chuo Kikuu cha Afrika Tanzania, Mchungaji Joshua Lee alisema semina ya mafunzo hayo kwa wanafunzi na viongozi wa vijiji yanalenga kuwapa ujuzi na maarifa ya kuanzisha biashara zao na kuondokana na hali duni ya vipato.

“Wamekuja wataalamu bingwa kutoka Chuo Kikuu cha Handong cha Korea kusaidia wanafunzi na viongozi wa vijiji kuwa na ujuzi wa miradi ya kijasiriamali,” alifafanua na kusema kwa pamoja vyuo hivyo vinalenga kuwezesha miradi itakayoanzishwa kifedha.

Mjumbe wa kamati ya Chuo Kikuu cha Afrika Tanzania, Bw. Gaudens Kayombo alisema hiyo ni fursa kubwa kwa vijana hasa kutoka vyuo vikuu na sekondari ambao wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ajira.

“Semina hii ni shirikishi kwa vile wanasemina wenyewe watasema wanahitaji kufanya biashara gani kutokana na mbinu watakazopewa katika semina hii,”alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad