Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-Utumishi Bw. HAB Mkwizu (wa pili kutoka kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu namna Serikali inavyoshughulikia madai ya watumishi walio katika Serikali za Mitaa wasio walimu.
Na Magreth Kinabo-maelezo
SERIKALI imetenga kiasi cha fedha cha Sh. bilioni tano ( 5.93) ikiwa ni madeni ya mishahara ya Watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa(TALGWU) na Sh. bilioni nne(4) kwa ajili ya kulipa madeni ya yasiyohusu mishahara, fedha ambazo zitalipwa Oktoba mwaka huu.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa leo na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, HAB Mkwizu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu madai na madeni ya watumishi hao kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dares Salaam.
Aidha Serikali imefafanua kwamba madai ya watumishi hao yanayohusu mishahara mpaka kufikia Oktoba Mosi,mwaka huu,ambao si walimu malimbikizo yake yalikuwa takribani Sh. bilioni 6.147, na idadi ya watumishi wanaodai ni 5,695 katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2015/2016.
Hivyo hadi kufikia Oktoba , mwaka huu Serikali ilikuwa imewalipa watumishi 1,551 wakiwemo wa Serikali za Mitaa jumla ya Sh. bilioni 1.6 na malipo hayo hayajumuishi yale yaliyofanyika kwa walimu.
“Aidha Watumishi wa Serikali za Mitaa wapatao 455 wenye madai ya Sh. milioni 593.2 watalipwa mwezi Oktoba, mwaka huu. Madai yaliyosalia yataendelea kulipwa kila mwezi kadri uhakiki unavyokamilika,” alisema Kaimu Katibu Mkuu huyo.
Alisema kwa upande wa madai yasiyohusu mishahara , ambayo yamekuwa yakilipwa kupitia fungu la Matumizi Mengineyo, madai ya kiasi Sh. bilioni 18 yalikwishahakikiwa na yanasubiri kulipwa.
Mkwizu aliongeza kwamba madeni hayo ya watumishi hao ni yale yaliyolimbikizwa hadi mwaka 2012/2013.
“ Serikali imepanga kulipa deni hilo lote katika kipindi cha kuanzia Oktoba 2013 hadi Januari,2016,kwa kuanzia Oktoba 2015 Serikali imetenga kiasi cha Sh. bilioni 4 na kiasi cha sh. bilioni 14 kitakachosalia kitalipwa kwa awamu ndani ya kipindi kilichopangwa,” alisisitiza.
Aidha Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema wakati wa kutekeleza malipo hayo, waajiri wameaagizwa kuwaandikia barua watumishi ambao madai yao yamekataliwa au kupunguzwa ili kuwafahamisha sababu za kutakataliwa kwake na hivyo kuwawezesha kuwa na taarifa sahihi kuhusu madai yao na kuondoa uwezekano wa kudai mara nyingine.
Akizungumzia kuhusu suala la uhakiki wa madeni alisema kwa upande wa madai yasiyohusu mishahara yalikuwa ni sh. bilioni 18,lakini baada ya kuhakikiwa yakafikia Sh. bilioni 14.
Alizitaja sababu mbalimbali za kukataliwa baadhi ya madeni hayo kuwa ni zipo tofauti na zinatokana na kutofuata sheria, kanuni na taratibu.
No comments:
Post a Comment