Kamishna Msaidizi wa
Madini Kanda ya Kati Singida, Sosthenes Masolla (aliyesimama), akifungua semina
kwa wachimbaji wadogo wa madini kuhusu mfumo mpya wa huduma za utoaji wa leseni
za madini kwa njia ya mtandao. Semina hiyo ilifanyika mjini Singida Septemba 5,
mwaka huu. Wengine pichani ni wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini.
Kutoka kushoto ni Placid Kabyemera, Juma Masoud, Mhandisi Nuru Shabani,
Mhandisi Gabriel Senge na Tantao Tantao.
Sehemu ya washiriki
wa semina kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa huduma za utoaji wa leseni kwa njia
ya mtandao iliyofanyika mjini Singida Septemba 5, mwaka huu. Semina hiyo ni
mwendelezo wa zoezi la utoaji mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini nchi
nzima kuhusu matumizi ya huduma hiyo mpya.
Na
Veronica Simba - Singida
Imeelezwa kuwa ni
marufuku kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18 kuandikishwa kama wabia wa
umiliki wa leseni za madini za aina yoyote hapa nchini.
Hayo yameelezwa hivi
karibuni na Mtaalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Nuru Shabani
wakati wa semina kwa wachimbaji wadogo wa madini mkoani Singida kuhusu matumizi
ya mfumo mpya wa huduma za utoaji leseni za madini kwa njia ya mtandao
ujulikanao kama OMCTP (Online Mining Cadastre Transactional Portal.)
“Sheria hairuhusu kutoa leseni kwa watoto
walio chini ya umri wa miaka 18 na kwa wale watakaobainika kutoa taarifa zisizo
za kweli kwa kuwaandikisha watoto walio chini ya umri husika kama wabia wa
umiliki wa leseni za madini, watachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema
Mhandisi Shabani.
Aidha, Mhandisi
Shabani aliwataka washiriki wa semina hiyo na watanzania wote kwa ujumla
kufahamu kuwa ni Wizara ya Nishati na Madini pekee ndiyo yenye mamlaka ya kutoa
leseni za madini za aina zote hapa nchini.
Alitoa ufafanuzi huo
baada ya baadhi ya washiriki wa semina kuuliza iwapo kuna mamlaka nyingine
nchini zinazoruhusiwa kisheria kutoa leseni za madini.
“Kuna baadhi ya watu
au vikundi vya watu au taasisi ambazo zimekuwa zikiingilia zoezi la utoaji wa
leseni za madini kwa baadhi ya waombaji nchini. Naamini wanafanya hivyo kwa
kutokujua sheria, hivyo ni vyema watu wote wafahamu kuwa hakuna mamlaka
nyingine hapa nchini yenye ruhusa ya kutoa leseni za madini kisheria isipokuwa
Wizara ya Nishati na Madini pekee,” alisisitiza.
Mhandisi Shabani
aliwataka wananchi hasa wamiliki halali wa leseni za madini wanaokumbana na
matatizo ya kutotendewa haki kwa kuzuiliwa kuendesha shughuli zao katika maeneo
yao kisheria, kutoa taarifa kwa ofisi za madini zilizopo karibu naoi li waweze
kupatiwa msaada kwa kufuata sheria.
Pia, aliwaasa
wachimbaji madini wadogo na wamiliki wa leseni pamoja na wananchi wote hususani
viongozi wa vijiji, halmashauri na taasisi mbalimbali, kuisoma na kuifahamu Sheria
ya Madini ya mwaka 2010 ili kuepusha migogoro mbalimbali inayotokea kuhusiana
na shughuli za uchimbaji wa madini.
Semina iliyofanyika
Singida kwa wachimbaji wadogo wa madini kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa huduma
za utoaji wa leseni za madini kwa njia ya mtandao, ni mwendelezo wa mafunzo
yanayoendelea kutolewa kwa wachimbaji wadogo nchi nzima chini ya Wizara ya
Nishati na Madini kwa lengo la kuongeza uwazi na kuboresha zaidi huduma za
sekta ya madini.
Washiriki mbalimbali
wa semina kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa huduma za utoaji wa leseni kwa njia
ya mtandao, wakiuliza maswali wakati wa semina hiyo. Semina ilifanyika mjini
Singida Septemba 5, mwaka huu.
Mhandisi Migodi
kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Nuru Shabani, akiwasilisha mada mbalimbali
kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa huduma za utoaji leseni za madini kwa njia ya
mtandao (Online Mining Cadastre Transactional Portal – OMCTP) kwa Wachimbaji
madini wadogo, wakati wa Semina maalumu iliyofanyika Septemba 5, mwaka huu
mjini Singida.
Viongozi na wataalamu
kutoka Wizara ya Nishati na Madini, wakiwa katika picha ya pamoja na wachimbaji
wadogo wa madini kutoka mkoani Singida walioshiriki katika Semina kuhusu matumizi
ya mfumo mpya wa huduma za utoaji wa leseni kwa njia ya mtandao. Wa tatu kutoka
kulia (Waliokaa kwenye viti) ni Kamishna Msaidizi wa Madini wa Kanda ya Kati –
Singida na Kulia kwake ni Mhandisi Migodi kutoka Wizara ya Nishati na Madini,
Nuru Shabani. Semina ilifanyika Septemba 5, mwaka huu.


No comments:
Post a Comment