JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


MAKAMU WA RAIS AADHIMISHA KILELE CHA SIKU YA MARA (MARA DAY) BUTIAMA MKOANI MARA

Share This
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwasha Mshumaa katika Kaburi ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kama ishara ya Kumbukumbu wakati alipofika katika Jumba la makumbusho Butiama mkoani Mara leo Sept 15, 2015 baadda ya kuadhimisha Kilele cha Siku ya Mara (Mara Day) iliyofanyika Butiama.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiweka Shada la Maua katika Kaburi ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kama ishara ya Kumbukumbu wakati alipofika katika Jumba la makumbusho Butiama mkoani Mara leo Sept 15, 2015 baadda ya kuadhimisha Kilele cha Siku ya Mara (Mara Day) iliyofanyika Butiama. Kushoto ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa Kenya, Eugene Wamalwa. 
 Makamu wa Rais waJamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia wakati wa sherehe za maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mara (Mara Day) zilizofanyika  kwenye Uwanja wa Mwitongo, Butiama mkoani Mara leo Sept 15, 2015
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mbogo Futakamba (kushoto) akibadilishana mikataba na Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa Kenya, Eugene Wamalwa, mara baada ya kusainiana Mkataba huo wa Maridhiano ya Mto Mara, wakati wa sherehe za Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mara (Mara Day) zilizofanyika Butiama mkoani  Mara leo Sept 15, 2015. Kulia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanznia, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akishuhudia.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mbogo Futakamba (kushoto) na Waziri  wa Maji na Umwagiliaji wa Kenya, Eugene Wamalwa (katikati) wakitiliana saini mkataba wa Maridhiano ya Mto Mara wakati wa sherehe za Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mara (Mara Day) zilizofanyika Butiama mkoani  Mara leo Sept 15, 2015. Kulia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanznia, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akishuhudia.
  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Tuzo ya kushiriki maadhimisho na kutunza mazingira, Mwakilishi wa Serikali ya Jimbo la Narok nchini Kenya, Rebeccah Seenoi, wakati wa sherehe za maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mara (Mara Day) zilizofanyika  kwenye Uwanja wa Mwitongo, Butiama mkoani Mara leo Sept 15, 2015.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akipata maelezo kutoka kwa Eugene Muramira, wakati alipotembelea katika Banda la maonesho la Afrika Mashariki, wakati wa Sherehe za Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mara (Mara Day) zilizofanyika leo Sept 15, 2015 kwenye Uwanja wa Mwitongo Mkoani Mara. Picha na OMR






HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE  KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA MARA (MARA DAY), BUTIAMA-MARA 
TAREHE 15 SEPTEMBA 2015

Waheshimiwa Mawaziri kutoka  Tanzania na Kenya;
Makatibu Wakuu wa Wizara;
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na  Magavana wa Majimbo;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Wakurugenzi wa Halmashauri  pamoja na Caunt kutoka Kenya;
Wawakilishi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria;
Wataalam kutoka Wizara,  Taasisi mbalimbali  Kenya na Tanzania;
Wadau wa Maendeleo;
Wawakilishi wa Jumuiya za Watumiaji Maji;
Ndugu Wanahabari;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana

Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na afya njema na kutuwezesha kukusanyika hapa siku ya leo kushuhudia tukio hili muhimu. Napenda nitumie nafasi hii pia kuwashukuru waandaji wa shughuli hii, kunialika kuwa Mgeni Rasmi   katika siku hii ya pekee ambayo wadau wa Bonde la Mto Mara, wanakutana katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mara (Mara Day). Nimepokea mwaliko huu kwa mikono miwili, nasema; Asanteni Sana! Nitumie fursa hii pia kuwakaribisha mkoani Mara, hususani hapa Butiama, wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania. Nasema Karibuni Sana Butima. Jisikieni mpo nyumbani. Hili ni eneo lenye historia kubwa kwa Tanzania na Bara la  Afrika kwa ujumla kwani ndipo alipozaliwa na alipolala, Baba wa Taifa letu na Mtetezi wa Wanyonge Barani Afrika na Duniani kwa ujumla, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere(Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi). Napenda pia nitumie nafasi hii kuwashukuru waandaaji wa sherehe hizi na wadau mbalimbali waliochangia kwa namna moja ama nyingine kufanikisha shughuli hii. Endeleni na moyo huo, fanyeni kila linalowezekana kuzidi kuboresha jambo hili mwaka hadi mwaka.

Ndugu Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Tukio la leo linatoa fursa kwa wadau kutoka nchi mbili,  Tanzania na Kenya zinazopitiwa na Bonde la Mto Mara, kukutana pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya uhifadhi na matumizi endelevu ya Mto Mara na kutafakari mustakabali wa  Bonde hili kwa ujumla.  
Hifadhi za Mto Mara zina umuhimu mkubwa kiuchumi kwa nchi hizi mbili kutokana na mapato yatokanayo na utalii. Wanyama waliopo katika hifadhi za Serengeti nchini Tanzania na Maasai Mara kwa upande wa Kenya, hutegemea sana maji ya Mto Mara kwa maisha yao.  Aidha siku hii inakwenda sanjari na msimu wa uhamaji wa wanyamapori jamii ya nyumbu ambapo inakadiriwa kuwa jumla ya nyumbu Milioni mbili wanahama na kurudi kutoka  mbuga za Serengeti- Tanzania na Maasai Mara nchini Kenya  kwa kipindi cha  Julai na Oktoba kila mwaka.
Kaulimbiu ya Madhimisho ya  mwaka huu ni “Mto Mara: Maisha yangu, Maendeleo yangu”. Kaulimbiu hii ni nzuri kwani inalenga kusisitiza dhamira ya dhati ya usimamizi shirikishi wa rasilimali za maji na nyinginezo katika Bonde la Mto Mara. Fanyeni kila linalowezekana kuhakikisha mnabadilisha Bonde hili na kuwa mfano katika shughuli za maendeleo ikiwa pamoja na kufungua milango na fursa zaidi za uwekezaji. Ni wajibu wa wadau wote wa Bonde hili kuhakikisha chini ya Ushirikiano mzuri wa  Jumuiya ya Afrika Mashariki, vitega uchumi mbalimbali vinawekezwa katika Bonde hili ili kusaidia wananchi wa  nchi hizi mbili  kuondokana na umasikini .
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Mto Mara ni mto wa kimataifa unaounganisha nchi mbili za  Tanzania na Kenya. Wananchi na wadau mbalimbali  wa nchi hizi waishio katika Bonde la Mto Mara wanatumia maji na rasilimali zingine kama ardhi na misitu katika bonde hili kwa ajili ya kuendeleza maisha yao ya kijamii na kiuchumi kwa nia ya kupunguza umasikini. Hata hivyo kadri ya miaka inavyokwenda, hali ya rasilimali hizi imekuwa ikipungua kutokana na matumizi mbalimbali.
Hivi sasa tunashuhudia matumizi ya rasilimali hizi yakiongezeka kutokana na ongezeko la mahitaji ikiwa ni pamoja na ongezeko la fursa za kiuchumi. Kwa upande mwingine tunashuhudia rasilimali hizi zikipungua na kuharibika hivyo kupunguza fursa ya nchi hizi na jamii, kujikwamua kiuchumi na kupunguza umasikini. Wakazi wa Bonde hili sasa wanashuhudia kupungua kwa maji na  uchafuzi wa maji, kuzidi kupungua kwa misitu kunakosababishwa na ukataji holela wa miti, uharibifu wa ardhi na uharibifu mkubwa wa mazingira kwa ujumla unaosababishwa na shughuli za kibinadamu. Wito wangu kwenu tunapoadhimisha Siku hii ya Mara, ni wajibu wa kila mmoja wetu kutafakari juu ya changamoto za msingi zinazopaswa kuchukuliwa katika kuboresha matumizi endelevu na usimamizi wa  Bonde hili.  Sote tunafahamu kuwa Bonde la Mto Mara lina umuhimu mkubwa kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa eneo hili, hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha linatunzwa na kuendelezwa ili lisadie wananchi wetu kupata maisha bora na kuondokana na umasikini.
Ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunatilia mkazo suala la utunzaji mazingira katika Bonde hili. Uharibifu wa Mazingira ni  moja ya tatizo linalotishia kwa kiasi kikubwa uhai wa Bonde hili. Tusipotilia mkazo utunzaji mazingira katika eneo hili tutaathiri kwa kiasi kikubwa rasilimali zilizomo katika Bonde hili na kukwamisha juhudi za wakazi wa eneo hili kujikwamua na umasikini. Tukiendelea kuharibu mazingira ya Bonde hili tutasababisha matatizo mengi ikiwa ni pamoja na kupungua kwa kiasi kikubwa cha maji kwenye Mto Mara. Jambo hili halitaathiri wanyama tu bali linaweza hata kusababisha migogoro  ya wanaotumia maji hayo katika nchi hizi mbili. Rai yangu kwa wadau wote wa Bonde la Mto Mara ni kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Mara kila mwaka yawe  chombo cha kuhakikisha kuwa hatufiki huko. Naamini kwamba Serikali za nchi zote mbili Tanzania na Kenya  zina sera, sheria na mikakati mizuri inayolenga kuhifadhi na kuhakikisha usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali mbalimbali za Mto Mara kwa ajili ya maendeleo ya jamii kwa ujumla. Lazima tuwe na chombo chenye malengo ya pamoja ya kusimamia Sera na Sheria hizo.

Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu kwa mara nyingine naomba niwashukuru wadau wote mliofanyikisha Maadhimisho haya, bila kuwasahau ndugu zetu kutoka Jamhuri ya Watu Kenya kwa namna mlivyojitoa kufanikisha shughuli hii. Asanteni Sana! tuzidi kushirikiana na Karibuni tena na tena.
Baada ya kusema hayo, kwa heshima kubwa na taadhima sasa  natamka rasmi kuwa; Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Mara, zimefungwa rasmi.

Asanteni sana kwa kunisikiliza. 


CHIMBUKO LA MAADHIMISHO YA SIKU YA MARA.
1.  Utangulizi:
Maadhimisho ya siku ya Mara hutoa taswira ya jinsi viongozi na wananchi wanchi mbili za Kenya na Tanzania wanavyoshirikiana katika kusherehekea maadhimisho ya siku hiyo. Hii ni mojawapo ya shughuli muhimu katika kuimarisha ushirikiano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kilele cha Maadhimisho hayo huwa ni tarehe 15 Septemba ya kila mwaka.
2.  Bonde la Mto Mara:
Bonde hili ni moja kati ya mabonde yenye mito inayoingiza maji katika Ziwa Victoria. Bonde hili linahusisha nchi za pande mbili ambazo ni Kenya ambayo inamiliki takribani asilimia 65 ya eneo bonde na Tanzania asilimia 35. Asili ya mto Mara ni chemichemi ya Enapuyapui iliyoko kwenye misitu ya milima ya Mau katika nchi ya Kenya na maji yake hutiririka kuelekea katika pori la akiba la hifadhi ya Taifa ya Maasai-Mara kwa upande wa Kenya, na kwa upande wa Tanzania mto Mara unapita katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti kabla ya kumwaga maji yake katika Ziwa Victoria nchini Tanzania ambapo mto huo hupita katika Wilaya nne za Serengeti, Tarime, Butiama na Rorya. Ikolojia ya Bonde la mto Mara ni moja kati ya Ikolojia muhimu katika Bonde la Ziwa Victoria ambayo inachangia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii pamoja na utumiaji na uhifadhi wa uoto wa Asili.

3.  Chimbuko la Maadhimisho ya Siku ya Mara.
Maadhimisho hayo ni kufuatia maamuzi yaliyofanywa na Baraza la Mawaziri wanaohusika na masuala ya Bonde la Ziwa Victoria kwenye Mkutano wa kumi uliofanyika tarehe 04 Mei, 2012 huko Kigali Rwanda. Katika Mkutano huo iliamuriwa kuwa maadhimisho hayo yafanyike kwa kupokezana baina ya nchi zote mbili za Kenya na Tanzania.
4.  Faida ya maadhimisho haya:
Siku ya Mara hutumika katika kuendelea kulitangaza na kulifuatilia tukio muhimu la wanyamapori hasa nyumbu kuhama kutoka mbuga za hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda katika pori la hifadhi ya Taifa la Maasai-Mara katika Jamhuri ya Kenya na baadaye kurudi Tanzania na mara zote mbili wanyama hao huvuka mto Mara.
Uamuzi huo wa kuadhimisha Siku ya Mara, ulitokana na kutambua umuhimu wa Ikolojia ya Bonde la mto Mara ambapo siku hiyo itatumika kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mto Mara. Aidha, maadhimisho ya siku ya Mara pia hutumika katika kufanya yafuatayo:
i.                 Kujengea jamii uwezo juu ya uelewa wa masuala ya mazingira na changamoto za kijamii zinazojitokeza katika Bonde la mto Mara.
ii.                Kuwawezesha wadau kushiriki katika fursa zinazohusiana na Bonde la mto Mara
iii.              Kuitambulisha sura ya Bonde la mto Mara kama eneo muhimu la uwekezaji
iv.              Kujadili mwendelezo wa utekelezaji wa shughuli zilizoratibiwa katika Bonde la mto Mara.
5.  Changamoto zinazolikabili Bonde la mto Mara
Jamii inayoishi katika Bonde la mto Mara pamoja na wadau mbalimbali wameendelea kushuhudia upungufu mkubwa wa kiwango cha maji pamoja na uchafuzi wa vyanzo vya maji kutokana na shughuli za kibinadamu, hali inayopelekea kuwa kikwazo kwa jamii inayoishi katika Bonde la mto Mara katika juhudi zao za kujiongezea kipato, kuwa na afya imara, kuwa na chakula cha uhakika pamoja na kukuza uchumi.
Changamoto hizi zinazotishia kutoweka kwa maliasili (Ikolojia) ya Bonde la mto Mara zinatokana na shughuli za kila siku za kibinadamu ambazo ni pamoja na matumizi ya ardhi yasiyo endelevu, ukataji miti holela kwa ajili ya kuchoma mkaa na ujenzi, uchimbaji holela wa madini, uchafuzi wa vyanzo vya maji, kilimo kisicho endelevu na ufugaji usio endelevu.
Shughuli zingine ni sera na sheria za nchi mbili kutofautiana, ukosefu wa elimu ya hifadhi ya mazingira kwa wakazi waishio katika Bonde la mto Mara, umaskini kwa wakazi wengi wanaoishi katika Bonde, udhaifu wa kusimamia sheria pamoja na ukosefu wa chombo shirikishi cha kusimamia rasilimali za bonde la mto Mara, hizi zikiwa ni baadhi tu ya changamoto.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad