Na Bashir Yakub.
Kisheria ndoa inapokuwa imefungwa kuna haki za msingi ambazo huibuka. Hizi huitwa haki za moja kwa moja ( automatic right). Huitwa haki za moja kwa moja kwakuwa hazina uhiari katika kutekelezwa kwake. Kuwapo kwa ndoa ndio kuwapo kwake na hivyo haihitaji mtu kuziomba. Kimsingi haki hizi zipo nyingi ambapo tutaona baadhi yake hapa huku makala yakijikita katika haki moja ya matunzo kwa wanandoa.
1.BAADHI YA HAKI ZINAZOIBULIWA NA NDOA.
( a ) Haki ya tendo la ndoa. Hii ni haki ya lazima kwa wanandoa na kutokuwepo kwake kunaweza kubatilisha ndoa iwapo mmoja wa wanandoa ataamua kufanya hivyo. Ni haki ambayo huchukuliwa kama ndio ndoa yenyewe na hivyo kuifanya kuwa na umuhimu wa pekee.
( b ) Haki ya kutumia jina la mume. Hii ni haki aliyonayo mwanamke ambapo anaruhusiwa kutumia jina la mme wake badala ya lile la baba yake. Hata hivyo sheria haikueleza iwapo mwanaume naye anaweza kutumia jina la mke wake, au la baba wa mke wake, au la ukoo wa mke wake. Pia si tu mwanamke ameruhusiwa kutumia jina la mme wake isipokuwa hata lile la ukoo wa mme wake.
( c ) Haki ya kutumia mali za familia kwa pamoja. Haijalishi mali hizo ni mwanamke mwanaume ataruhusiwa kutumia na haijalishi mali hizo ni za mwanaume mwanamke ataruhusiwa kutumia. Isipokuwa yawe matumizi ambayo hayako kinyume cha sheria.
( d ) Haki ya kutunza watoto/mtoto kama yupo. Ikiwa familia imebarikiwa na mtoto/watoto basi wanadoa kwa pamoja wanawajibika kuwatunza watoto hao kila mtu kwa nafasi yake. Hii ina maana mwanamke anawajibika zaidi kuwa mwangalizi mkuu wa kila siku wa watoto huku mwanaume akilazimika kutoa matumizi hasa yale ya kifedha.
( e ) Haki ya kugawana mali pindi ndoa inapovunjika. Hii huhusisha mali zote ambazo huitwa mali za machumo ya pamoja baina ya mwanamke na mwanaume.
( f ) Pia ipo haki ya kurithi na kurithiana iwapo kuna kifo cha mmoja wa wanandoa. Mwanamke aweza kurithi mali za mme wake halikadhalika mwanaume. Hii huenda mpaka kwa watoto waliopatikana katika ndoa ambapo huweza kurithi mali za baba, mama au wote wawili.
( g ) Haki ya matunzo baina ya wanandoa. Hii ndiyo itakayojadiliwa japo kwa ufupi .
2. MWANAUME KUMTUNZA MWANAMKE.
Sura ya 29 ya Sheria ya ndoa kifungu cha 63 ( a ) kinasema kuwa ni wajibu wa kila mwanaume kumtumza mke/wake zake kutokana na njia za kipato chake. Neno njia za kipato chake maana yake ni namna anavyopata kipato ndivyo atavyotakiwa kutoa matunzo kwa mwanamke. Haiwi kuwa mwanaume anapata kipato kidogo halafu alazimishwe kutoa matunzo makubwa. Ushahidi wa namna anavyopata kipato chake ndio utakaoainisha kiasi cha matunzo kwa mke wake.
Aidha kwa mujibu wa kifungu hicho matunzo yanayoongelewa hapa yanahusisha makazi, mavazi, chakula na huduma nyingine kama za afya n.k. Kitu cha msingi hapa ni kuwa ni lazima kwa mwanaume kutoa vitu hivi kwa mke wake.
3. MWANAMKE KUMTUNZA MWANAUME.
Kifungu hichohicho cha 63 ( b ) kinasema kuwa utakuwa ni wajibu wa kila mwanamke lakini mwenye uwezo kutoa matunzo kwa mume wake iwapo mume huyo ana ulemavu/hajiwezi jumla au sehemu ya mwili wake, kiakili au kimwili na hivyo kutokuwa na uwezo wa kuingiza kipato kutokana na hali hiyo.
Kwa kifungu hiki tunaona kuwa mwanamke anao wajibu wa kumtunza mume wake lakini iwapo tu kwanza ana uwezo, pili mwanaume awe na tatizo ambalo kwalo hawezi kuingiza kipato na tatizo hilo liwe la kimwili au kiakili. Kumbe basi tunaona kuwa mwanaume kumhudumia mwanamke ni lazima hata mwanamke awe mzima wa afya huku hafanyi kazi wakati mwanamke kumhudumia mwanaume ni pale tu atapokuwa ana tatizo ambalo linamfanya asiweze kufanya kazi. Lakini pia sheria imesema mwanamke atatoa huduma iwapo ana uwezo wakati neno iwapo ana uwezo haikuliwekwa kwa mwanaume.Kwa mwanaume kutoa ni kutoa tu.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment