JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


TMA YAZIDI KUIMARIKA, MAFANIKIO YAKE YATAJWA BUNGENI.

Share This

 


Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
SHUGHULI za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), zimeendelea kuimarika na kutoa huduma za utabiri wa kila siku, siku kumi na ule wa muda mrefu pamoja na tahadhari ya matukio ya hali mbaya ya hewa ili kuhakikisha usalama wa watu na mali zao.

Kufuatia uboreshaji unaoendelea kufanywa na Serikali, usahihi wa utabiri umefikia asilimia 86 ambao ni juu ya asilimia 70 ya kiwango cha usahihi kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amebainisha hayo leo, Mei 6,2024 jijini Dodoma wakati akiwasilisha utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha unaoisha wa 2023/24.

Amesema, TMA ilifanyiwa ukaguzi wa kimataifa kuanzia January 22 - 27, 2024, na kuendelea kukidhi vigezo vya kumiliki cheti cha ubora (ISO 9001: 2015).

61.

"Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 Ibara ya 59(j) na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano (FYDP III 2021/22-2025/26), Serikali iliahidi kuendelea kuimarisha miundombinu na huduma za hali ya hewa ikiwemo ununuzi wa rada" amesema Mbarawa.

Akielezea mafanikio ya TMA Prof. Mbarawa amesema Serikali kupitia TMA imefanikiwa kuendelea kuimarisha miundombinu na huduma za hali ya hewa, ikiwemo kwa kukamilisha ununuzi na ufungaji wa rada za hali ya hewa katika mikoa ya Kigoma na Mbeya na kufikisha jumla ya rada tano huku utengenezaji wa rada nyingine mbili (2) unaendelea kiwandani nchini Marekani na zinatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2024

"Sambamba na hilo, Serikali imeingia mkataba wa kuboresha rada za hali ya hewa zilizofungwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza ili kuendana na teknolojia ya kisasa ya rada za hali ya hewa," amesema Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa, Serikali kupitia TMA imefanikiwa kukamilisha ufungaji wa mitambo mitano ya kutoa huduma za hali ya hewa katika viwanja vya ndege vya Songwe, Zanzibar, Arusha na Songea, ili kuboresha huduma hizo kwenye usafiri wa anga.

"Taratibu za ufungaji mitambo mitatu ya kupima hali ya hewa kwenye viwanja vya ndege vya Musoma, Iringa na Mpanda, zinaendelea", amesema Mbarawa.

Pia, Serikali imekamilisha ununuzi wa seti 28 za mitambo ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe ambayo imefungwa katika vituo vya hali ya hewa vilivyopo kwenye viwanja vya ndege vya Mtwara, Songea na Arusha, huku mitamboi mingine 25 inaendelea na maandalizi ya kufungwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Morogoro, Iringa, Njombe, Tanga, Dodoma, Singida na Kilimanjaro.

“Kuhusu kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kujenga uwezo kwa watumishi, Serikali kupitia TMA imeendelea na ujenzi wa jengo la ofisi ya Kanda ya Mashariki na Kituo cha Tahadhari ya Matukio ya Tsunami, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 39. Vilevile, watumishi 74 wanaendelea na mafunzo ndani na nje ya nchi katika ngazi mbalimbali za elimu,” amesema Prof. Mbarawa.

Aidha Prof. Mbarawa amesema TMA inaendelea kufanya tafiti mbalimbali za masuala ya hali ya hewa na mabadiliko yake na tabia ya nchi, ambapo tafiti nne zilichapishwa katika majarida ya kimataifa ya kisayansi.

Miongoni mwa tafiti hizo ni kuhusu tathimini ya matukio ya hali mbaya ya hewa katika Bahari ya Hindi, tathimini ya ongezeko la joto kwa kipindi kati ya 1982 hadi 2022, tathimini ya hali ya mvua katika vituo vya hali ya hewa nchini na tathimini ya mabadiliko ya mvua na athari zake katika kilimo kwa nchi za Afrika Mashariki.

Pia, Prof. Mbarawa amesema kutokana na umahiri wa mamlaka hiyo kwenye utoaji wa huduma za hali ya hewa, 2019 WMO iliichagua Tanzania kupitia TMA kuendesha kituo cha kanda cha kutoa mwongozo wa utabiri wa hali mbaya ya hewa kwa nchi zilizopo ukanda wa Ziwa Victoria.

“Kituo hicho kipo Dar es Salaam na kinahudumia nchi tano ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, na Burundi. Sambamba na hilo, TMA iliteuliwa kutekeleza jukumu la kufuatilia ubora wa takwimu za hali ya hewa (data) zinazopimwa katika vituo vya hali ya hewa vya nchi sita (6) vya ukanda wa Afrika Mashariki ikujumuisha nchi ya Sudan Kusini,” amesema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa ameongeza kuwa, katika kuhakikisha kuwa umma wa Watanzania unapata taarifa sahihi za hali ya hewa, TMA imeongeza wigo wa kuhabarisha umma kwa kusaini mikataba ya utangazaji wa taarifa za hali ya hewa na Redio tano (5) za jamii ambazo ni Jambo FM (Shinyanga), Harvest FM (Pwani), Inland FM (Mwanza), Revival FM (Manyara) na CGFM (Tabora) na kuwa na jumla ya vyombo vya habari 108 vinavyohusisha redio 80, Televisheni 17, magazeti matatu (3) na Televisheni Mtandao (on-line TV) nane (8).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad