JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


UHUSIANO WA TANZANIA NA CHINA WAZIDI KUIMARIKA

Share This
Na Beatrice Lyimo-Maelezo
SERIKALI imesema itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Jamhuri ya Watu wa China kwa kuimarisha  fursa mbalimbali za kijamii ikiwemo nyanja ya  kiutamaduni. 

Hayo yamesemwa leo Jumatatu (Oktoba 12, 2015)Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene wakati wa halfa ya uzinduzi wa chaneli mpya ya filamu ya China –Africa Movies itakayoonyeshwa kupitia kituo cha televisheni cha Easy Television kilichopo nchini.

Bw. Mwambene amesema kuwa uwepo wa chaneli hiyo utasaidia wazalishaji wa Tanzania kuonekana na kujulikana kimataifa na kuweza kujiongezea kipato na fursa kwa waandaaji hao.

“Chaneli hii itawapa fursa kwa pande zote mbili kwani filamu ya Tanzania itaonyeshwa china na kutafsiriwa kwa lugha yao na kwa upande wa Tanzania filamu za china zitaonyeshwa hapa Tanzania na kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili”

Aidha Mwambene alisema  Chaneli ya China –Africa movies, licha ya kuwa  daraja la kujifunza tamaduni za kichina  pia itatoa fursa kwa Watanzania kuweza kujifunza mbinu mbalimbali za biashara na kufungua milango kwa Watanzania kufahamu hatua mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na  kiutamaduni.

Mwambene ameitaka  Idara ya filamu nchini China kuitembelea Wizara ya Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni kwani ina kitengo kinachohusika na filamu za ndani.

Kwa upande wake Waziri wa Radio, Televisheni na usimamizi wa filamu wa Jimbo la Henan, China  Bi. Song Fengxian  alisema Serikali ya China itaongeza ubunifu kwa watazamaji wa pande zote mbili na kuwashukuru wadau wote waliosaidia kufanikisha uzinduzi wa filamu hiyo.  

Naye mwakilishi wa Kituo cha EASY TV Bi. Sophia Selis alisema kuwa katika kuendeleza urafiki baina ya Tanzania na China, kituo cha Easy Television imekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha, kujifunza na kubadilishana utamaduni kulingana na wakati.

“Tunarusha program zetu kwa kutumia lugha mbalimbali ikiwemo kiingereza, kichina, kiarabu, kihindi na Kiswahili ili kukidhi tija za watazamaji wetu wa mataifa mbalimbali kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayotoa picha zenye ubora” alisema Bi. Selis.

Easy television inarusha jumla ya chaneli 33 vya televisheni ikiwemo filamu, muziki, burudani, michezo, matukio, habari, vipindi vya watoto.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad