Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akizungumza wakati wa Mkutano
wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu dhana ya wajibu wa kuwalinda
raia, ambapo alisema licha ya kuasisiwa kwa dhana hiyo dunia bado
imeendelea kushuhudia maisha ya watu wasiokuwa na hatia yakiendelea
kupotea kwa sababu tu Jumuiya ya Kimataifa inashindwa kutumiza wajibu
wake kwa wakati.
Balozi
Tuvako Manongi akizungumza wakati wa Majadiliano ya Baraza Kuu la Umoja
wa Mataifa kuhusu dhana ya kuwalinda raia (R2P) majadiliano
yaliyojielekeza katika kutathimini mafanikio na changamoto za utekelezi
wa dhana hiyo ikiwa ni miaka kumi tangu kuasisiwa kwake.
Picha hii ya maktaba ni ya wakimbizi katika kambi moja nchini
Tanzania, ambao jana jumanne akizungumza katika Mkutano wa Baraza Kuu
la Umoja wa Mataifa, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika UN Balozi
Tuvako Manongi amesema kutoka na wimbi kubwa linaloendelea la wakimbizi
kukimbilia mataifa mengine kutafuta usalama wao. Jumuiya ya kimataifa
haina budi kushirikiana na bila kubagua katika kuwalinda na utoaji wa
huduma na misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi.
Na Mwandishi Maalum, New York
Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, imetoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa wa kushirikiana
katika wajibu wa kuwalinda na kuwapatia
misaada ya kibinadamu, wakimbizi wanaokimbia
machafuko, vita na migogoro katika nchi
zao.
Wito huo umetolewa
siku ya jumanne na Balozi Tuvako Manongi,Mwakilishi
wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, wakati
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,
lilipokutana kwa majadiliano ya
siku moja kuhusu utekelezaji wa dhana juu ya wajibu wa kulinda raia
(R2P) mafanikio na changamoto zake.
Dhana ya wajibu wa kuwalinda raia dhidi ya
mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita,
mauaji ya kikabila na uhalifu dhidi ya
binadamu ilianzishwa mwaka 2005
wakati wa mkutano wa Kimataifa uliofanyika mwaka huu, ambapo viongozi
wakuu wa nchi na serikali walikubaliana kwamba wajibu
wa kwanza wa kuwalinda raia dhidi ya
udhalimu wa aina yoyote ile ni wa serikali yenyewe husika.
Kupitia dhana hiyo ya R2P viongozi hao walikubaliana pia kwamba ikiwa
itadhihirika kuwa serikali ya nchi husika inashindwa kuwalinda raia wake kwa
sababu zozote zile basi jumuiya ya
kimataifa inapashwa kuchukua maamuzi ya
kuwalinda raia hao.
Akichangia majadiliano hayo ambayo yaliyofunguliwa na Katibu Mkuu Ban Ki moon, Katika Balozi
Manongi, ameeleza kwamba, dhana ya kuwalinda raia inapashwa pia kuhusisha tatizo
la wakimbizi wanaokimbia nchi zao kwa sababu mbalimbali na kwenda kutafuta
usalama katika mataifa mengine.
Akasema , Tanzania ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikiwapokea na kuwahifadhi wakimbizi kutoka mataifa mbalimbali, kwa uzoefu wake inatambua dhahiri kuwa ushirikiano wa
kimataifa ni muhimu sana na kwamba
Jumuiya ya kimataifa inatakiwa kuuboresha na kuimarisha ushirikiano huo.
“Tatizo linaloendelea hivi sasa la wimbi kubwa la wakimbizi wanaokimbilia Ulaya wakitokea Syria, Libya na kwingineko,
ni changamoto yetu sote, ni
changamotoya kimataifa, wakimbizi hawa
na wengineo wanapashwa kulindwa na kusaidiwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa zikiwamo sheria za
haki za binadamu ”.
Akasema Balozi Manongi.
“ Tanzania kama nchi ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikiwapokea na kuwahifadhi wakimbizi, inatambua kwamba ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika
kuwasaidia wakimbizi. Ni Muhimu
basi tuimarisha na kuboresha misingi
ya kusaidiana katika kulibeba jukumu hili” akasema Balozi
Manongi
Akizungumzia Zaidi kuhusu dhana ya wajibu wa kuwalinda raia, dhana ambayo
tafsiri yake bado haijapokelewa
vema miongoni mwa nchi wanachama Balozi amesema. Tanzania inaamini kwamba
kanuni za sheria za kimataifa zikiwamo zile za
uhusiano na ushirikiano baina ya
nchi marafiki ni muhimu
katika kuielewa, kutafsiri
na utekelezaji wa dhana ya wajibu wa kuwalinda raia kutoka na ukweli
kwamba ni dhana ambayo haijjitegemei.
Aidha Mwakilishi huyo wa Tanzania katika Umoja wa
Mataifa, amebainisha kuwa, ingawa wajibu wa kwanza wa utekelezaji wa
wajibu wa kuwalinda raia ni wa Nchi au Serikali
husika, lakini nchi
hiyo inaposhindwa kutimiza wajibu wake huo, basi Jumuiya ya Kimataifa inapashwa kusaidia
kwa kuiwezesha nchi hiyo kutekeleza wajibu huo.
Awali Akifungua majadiliano hayo
Katibu Mkuu, Ban Ki Moon, asema, ni jambo la kusitikisha sana kwamba miaka kumi tangu kuasisiwa kwa
dhana hiyo ya R2P bado watu wengi
wakiwamo watoto wameendelea kupoteza
maisha kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za vita na
migogoro.
“ Ninasikitiza kueleza kwamba miaka
kumi tangu kuanzishwa kwa dhana hii, dunia imeendelea kushuhudia matukio ya watu kupotezesha maisha yao kwasababu tumeshindwa
kuwalinda. Tunaendelea kushuhudia watu wakipoteza maisha huko Sudan ya Kusini,
Sudan katika jimbo la Darfur, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Libya, Syria,
Yemen, Mali, Jamhuri ya Afrika ya
Kati na kwiengineko”.akaeleza Ban Ki
Moon.
Na kwa sababu hiyo Katibu Mkuu amependekeza mambo
kadhaa ambayo anaamini yatasaidia
kuongeza kasi ya utekelezaji wa dhana
hii.
Baadhi ya Mambo hayo ni,
nchi wanachama na hasa Baraza
Kuu la Usalama, kuwa tayari kwa kuweka
mazingira ya kisiasa ya kuzuia na
kuitikia pale
inapojidhirisha kuwapo kwa dalili
za kutokea kwa uhalifu, utoaji wa tahadhari na kuchukua hatua.
Wazungumzaji wengine katika mkutano huo
wamelinyoshea kidole Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa na
hasa katika matumizi ya kura ya Veto
yanayofanywa na wajumbe wa kudumu wa baraza hilo.
Baadhi ya wachangiaji wameeleza
kwamba ili kanuni ya wajibu wa kuwalinda raia iweze kutekelezwa kwa haraka na kwa wakati,
wajumbe wa watano wa kudumu wa Baraza Kuu la Usalama, wanapashwa kuonyesha utashi wa kisiasa na kuacha kutumia
kura hiyo kwa maslahi binafsi.
Wajumbe wengine , licha ya kuelezea nchi zao kutoridhishwa kwa
tafsiri ya dhana ya wajibu wa
kuwallinda raia lakini pia wamesema
hawakubaliani na matumzi ya nguvu kuingilia nchi nyingine kwa na hata kuwaondoa madarakani viongozi kwa kisingizio utekelezaji wa dhana ya wajibu wa kuwalinda
raia.
Wajumbe wengine wameeleza wazi wazi kupinga kwao hoja
ya kutaka kuingizwa kwa
dhana hiyo ya R2P katika
ajenda za Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa. Sababu zikiwa ni pamoja na kuwa dhana hiyo bado inautata na inahitaji kuendelea kujadiliwa
miongoni mwa nchi wanachama.
No comments:
Post a Comment