JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


TAMKO LA SHIRIKISHO LA VYUO VYA ELIMU YA JUU TANZANIA-CCM

Share This
 SHIRIKISHO la Taifa tunawapongeza wajumbe wote wa vikao vyote vya maamuzi ndani ya chama chetu kwa kutenda haki na kumteua mgombea safi, muadilifu, mchapa kazi, mzalendo, ambaye hakuwa na kundi na hadi kwa sasa hana kundi, mwenye dhamira ya dhati na utashi wa kudumisha umoja na mshikamano ndani na nje ya chama chetu.

Shirikisho Taifa tunapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Daktari John Pombe Magufuli na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassani kuteuliwa kuwa wapeperusha bendera ya CCM 2015 katika nafasi ya Urais na Umakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Dr Ali Mohammed Shein kwa kuteuliwa kupeperusha bendera ya uraisi kwenye serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Tunapenda kuwakumbusha kuwa watanzania wana mategemeo makubwa kwao kwa fursa hii waliyoipata.  Kwa uteuzi huu, tunapenda kukipongeza chama chetu chini ya uongozi wa Daktari Jakaya Mrisho Kikwete kwa mara ya kwanza katika historia kwa kuwaamini na kuwapa fursa wanawake na kuwapa nafasi za juu kabisa za uongozi wa nchi yetu.

Tunapenda kuwakumbusha wanachama wenzetu waliojitokeza kuomba ridhaa ya uteuzi wa chama chetu kuwa mgombea aliyepatikana ni kwa mujibu wa taratibu na kanuni za uteuzi za chama chetu na si vinginevyo. Pia wakumbuke kuwa watia nia wote 42 walikuwa na nafasi sawa katika uteuzi lakini walitofautiana sifa za uteuzi.  Hivyo basi hakukuwa na suala la mtu kushinda au kushindwa kilichokusudiwa ni suala la chama kumteua mtia nia aliyekidhi vigezo na sifa za uteuzi, jambo ambalo limefanikiwa.

Shirikisho Taifa tunapenda kukumbusha kuwa misingi ya utawala wa kidemokrasia inatoa fursa ya kuwapa watu fursa ya kutoa maamuzi kwa pamoja.  Hii inathibitika kutoka kwenye kauli ya ya Mwl. JK. Nyerere aliowahi kuiandika kwenye maudhui yake ya dhana ya falsafa ya UHURU NA MAENDELEO: Mwalimu alisema hivi;

Tanzania ni ya Watanzania, na Watanzania ni wote. Hakuna mtu mwenye haki ya kusema ‘mimi ndiyo watu’. Wala hakuna Mtanzania, mwenye haki ya kusema, ‘Najua linalowafaa Watanzania, na wengine lazima wafuate’. Watanzania wote lazima waamue mambo ya Tanzania. Wote lazima wafanye kazi, na wote sisi lazima tuzikubali kanuni tunazojiwekea………Kanuni nyingine ni za Taifa zima, na kanuni ya namna hiyo ndiyo sheria ambayo wote tunapaswa kuitii”.

Kutokana na maandiko haya ya Muasisi wa taifa letu, Shirikisho Taifa tunapenda kurejea kauli yetu ya awali ya TAREHE 4 JULAI 2015 kuwa:
“CCM ni taasisi iliyoundwa kwa muundo wa kuongoza kwa pamoja na kutoa maamuzi kwa pamoja. Dhana hii inaonesha kuwa CHAMA chetu si mali ya Mtu binafsi au taasisi ya mtu mmoja inayotarajiwa kutoa maamuzi yanayotarajiwa kumfurahisha mtu huyo bali ni taasisi inayoweza toa maamuzi yasiyomfurahisha mtu mmoja mmoja kwa wakati wote.”

Kauli hii inathibitishwa na namna ya wanachama wa CCM walivyofanya uteuzi wa Mgombea wa Urais 2015 kwa pamoja. Kitendo cha uteuzi wa mgombea wa URAIS uliofanywa kwa pamoja unathibitisha kuwa CCM ni chama cha watanzania walio wengi, na CCM ndio Tanzania, kwani CCM ndio chama kinachotawala Tanzania.

 Hivyo basi kwa umoja wao kama watanzania, kwa kauli moja wamefanya uamuzi kupitia Mkutano Mkuu Maalum kwa kumteua mtu makini, muadilifu, mpenda haki, anayefuata sheria na taratibu tulizojiwekea, mtu ambaye ni mfuatiliaji na mtekelezaji wa maamuzi, (kwa mfano; ni mtu mwenye uwezo wa kusema hili lifanyike na kuhakikisha linafanyika).

  Kwa uteuzi huu makini uliozingatia misingi yote mikuu ya demokrasia na utawala bora, Shirikisho Taifa hatutarajii kumuona mtu yeyote au kikundi chochote ndani na nje ya chama kidhihaki au kukejeli na kukosoa maamuzi haya matukufu ya Mkutano Mkuu wa CCM 2015, isipokuwa tunatarajia kusikia na kuona kila mwana CCM na watanzania kwa ujumla wetu kuendelea kuunga mkono maamuzi ya Mkutano Mkuu Maalum wa CCM na pia kuendelea kumuunga mkono Mgombea mwenyewe, Mh. Dkt. John Pombe Magufuli.

Mwisho, tunapenda kuwaambia wanachama, wapenzi, mashabiki, na wakereketwa wa Chama Cha Mapinduzi kuwa uchaguzi au uteuzi wa mgombea kwenye ngazi ya URAIS umekwisha.

 Hivyo basi makundi yote 42 yaliyokwenda Dodoma yamevunjwa baada ya uteuzi wa Mh. Dk. John Pombe Magufuli na kubaki kundi moja tu la CCM, kwani siku zote UMOJA NI USHINDI.

 Ni busara na wajibu wetu kuungana pamoja kumnadi, kumtembeza na kumsemea Mgombea wetu pamoja na kuitangaza ilani ya uchaguzi ya CCM kwa watanzania ili CCM ipate nafasi ya kushinda na kuendelea kuiongoza Tanzania. Shirikisho Taifa, tunapenda kuwaarifu wanaCCM wenzetu kuwa sisi makada wa vyuo vya elimu ya juu tutamtembeza, tutamsemea na kumnadi Dk. John Pombe Magufuli na Bi. Samia Suluhu Hassani kila kona ya Tanzania ili CCM ipate ushindi wa kishindo hapo Oktoba 2015.

Hata hivyo tunatuma salamu kwa vyama vya upinzani, tunaomba wajiandae kisaikolojia. Vijana wasomi wa CCM tutaifanya kazi yetu kwa ubora na ueledi wa hali ya juu kuhakikisha raisi anatokana na CCM, tutarudisha majimbo yaliyo shikiliwa na upinzani na hatutawapa nafasi ya wao kuupotosha umma mwaka huu. Niwatakia wale wote wanao chukua fomu za kugombea ubunge na udiwani kupitia CCM kila la heri.

 Wito wangu kwa vijana wasomi kujitokeza kwa wingi katika kugombea nafasi za uongozi ili tukisaidie chama na nchi katika kukuza uchumi wetu na kutumia taaluma na ujuzi tulio nao kuwasaidia watanzania kukabiliana na changamoto zinazo wakabili katika miaka mitano ijayo.

 Tunaamini wajumbe wa vikao vya maamuzi wamejifunza vya kutosha kupitia mchakato wa kumpata mgombea wa uraisi atakaye peperusha bendera ya CCM. Mkatuchagulie wazalendo, waadilifu, wawajibikaji wenye kukubalika ndani na nje ya chama chetu kwenye nafasi ya ubunge, uwakilishi na udiwani. Chama kwanza, mtu baadae.

 Umoja ni ushindi. Hatma ya nchi yetu ipo mikononi mwetu watanzania, ni jukumu la kila mmoja wetu kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa kuwapata viongozi bora.
Ushindi ni lazima.
 Mwenyekiti wa Shirikisho la vyuo vya Elimu ya Juu Taifa (MNEC) Bi. Zainab Abdalah Issa akiongea na waandishi wa habari(Hawapo Pichani) na kutoa tamko la kuwapongeza wajumbe wote wa vikao vya maamuzi ndani ya chama cha mapinduzi (CCM) kwa kutenda haki katika uteuzi wa wagombea watakaowakilisha chama hicho katika uchaguzi mkuu baadae mwezi kumi, wakati wa mkutano uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho hilo Bw. Hamid Saleh Mhina.
Baadhi ya waandishi wa Habari wakimsikiliza Mwenyekiti wa Shirikisho la vyuo vya Elimu ya Juu Taifa (MNEC) Bi. Zainab Abdalah Issa wakati wa mkutano huo

Picha na Hassan Silayo

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad