JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


WAZIRI MKUU AAGIZA MPANGO WA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA TAASISI ZA DINI KATIKA ELIMU

Share This
▪️︎ Asema Serikali inathamini mchango wa taasisi za dini katika maendeleo

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amemwelekeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, kuandaa mpango wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini katika elimu, kwa kuzingatia uzoefu wa ushirikiano uliopo katika sekta ya afya.

Ametoa maelekezo hayo leo (Jumapili, Novemba 1, 2026), wakati akimwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ibada ya uzinduzi wa nyumba mpya ya ibada ya Bethel ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Nshara, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.

“Mheshimiwa Waziri, utaenda ukae na wenzako. Kaa na Waziri wa Afya,” amesema.

Dkt. Mwigulu ameelekeza wataalamu wa wizara hizo kuangalia namna ya kuimarisha ushirikiano katika elimu na kuandaa mpango utakaowasilishwa kwa Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kupata ridhaa ya Serikali.

Maelekezo hayo yamefuatia maelezo kuhusu ujenzi wa kampasi ya Machame ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCo), kinachomilikiwa na KKKT, Dayosisi ya Kaskazini, pamoja na ombi la kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa katika kutoa elimu.

Akifikisha salamu za Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa taasisi za dini katika maendeleo ya Taifa na itaendelea kushirikiana nazo katika kutoa huduma kwa wananchi.

Amesema historia ya maendeleo ya Tanzania haiwezi kutenganishwa na mchango wa Kanisa, hususan katika elimu na afya, ambako taasisi za dini zimekuwa zikihudumia wananchi bila kujali imani zao.

“Hauwezi ukayataja maendeleo ya nchi yetu hii kwa ustadi wowote ule bila kutaja mchango wa Kanisa,” amesema.

Dkt. Mwigulu amewapongeza washarika wa Nshara, viongozi wa Kanisa, kamati ya ujenzi na wadau wote waliofanikisha ujenzi wa nyumba hiyo ya ibada, akisema wamefanya kazi kubwa inayostahili kupongezwa.

Kuhusu mazingira, Waziri Mkuu amehimiza wananchi kuchukulia kwa uzito utunzaji wa miti na athari za mabadiliko ya tabianchi. Amemwelekeza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, kufuatilia hoja ya ukataji miti iliyowasilishwa katika ibada hiyo, kwa kushirikiana na viongozi na wadau husika.

Aidha, amemwelekeza Mkuu wa Mkoa kufanyia kazi ombi la kufungwa taa za barabarani katika eneo la kanisa na kufuatilia hoja za miundombinu zilizowasilishwa na Mbunge wa Hai.

Kwa upande wake, Mkuu wa KKKT, Askofu Dkt. Alex Malasusa, amewapongeza washarika na wadau waliofanikisha ujenzi huo, huku akisisitiza umuhimu wa malezi bora, mazungumzo katika familia na upatanishi katika jamii.

Naye Mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, ameomba ushirikiano wa Serikali na Kanisa katika elimu na afya uendelezwe. Amesema uzoefu huo ni msingi wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), unaolenga kutoa huduma kwa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Ujenzi, Mjumbe wa Kamati hiyo, Freeman Mbowe, amesema wananchi walitenga eneo la ekari 50 kwa ajili ya maendeleo ya elimu na kulikabidhi kwa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini. Ameeleza matarajio yao ya kuona chuo hicho kinatoa elimu bora inayozingatia sayansi na teknolojia.

Kwa mujibu wa risala ya Usharika wa Nshara, nyumba hiyo ya ibada imejengwa kwa zaidi ya miaka kumi kwa gharama zinazokadiriwa kufikia Sh. bilioni 6.5 na ina uwezo wa kuketisha waumini 2,000 kwa ibada.

Ibada ya uzinduzi na kubariki nyumba hiyo imeongozwa na Askofu Dkt. Shoo, huku Askofu Dkt. Malasusa akitoa mahubiri.





















No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad