Na Chalila Kibuda, Michuzi TV
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imejivunia umahiri ulioonyeshwa na vijana wanaosoma elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini katika mashindano ya kimataifa ya ufundi (Olympics) yaliyofanyika nchini Algeria.
Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa Wizara hiyo, Dkt. Fredrick Salukele, amesema vijana walioshiriki mashindano hayo wameonyesha uwezo mkubwa, huku hakuna mshiriki wa Tanzania aliyeshika nafasi za mwisho katika mashindano hayo.
Akizungumza mara baada ya kuwasili nchini, Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Fredrick Salukele, ambaye pia ni Mwakilishi Rasmi (Official Delegate), amesema ushiriki huo umeonesha kuwa Tanzania ina vijana wenye ujuzi na uwezo wa kushindana katika viwango vya kimataifa.
Dkt. Salukele ameyasema hayo wakati wa kuwasili nchini akitokea Algeria akiwa ameambatana na wanafunzi, wakufunzi pamoja na watendaji wa Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi (NACTVET) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Amesema matokeo hayo yanaonyesha kuwa vijana wanaopata mafunzo ya ufundi nchini wana uwezo wa kushindana kimataifa, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa kuhakikisha vyuo vinakuwa na vifaa vya kutosha na vya kisasa.
Tanzania iliwakilishwa na vijana watano walioshiriki katika fani za Uchomeleaji (Welding), Upakaji Rangi na Upambaji (Painting and Decorating), Usanifu na Utunzaji wa Mandhari (Landscape Gardening), Uokaji (Bakery) na Ufundi Bomba na Mifumo ya Joto (Plumbing and Heating).
Amesema mashindano hayo pia yamekuwa fursa ya kujifunza na kubaini maeneo yanayohitaji kuboreshwa katika utoaji wa mafunzo ya ufundi ili vijana waweze kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira na teknolojia inayobadilika.
Vijana wa Kitanzania wameshiriki kikamilifu na kuonesha umahiri katika Mashindano ya Olimpiki ya Ujuzi Afrika (African Skills Olympics) yaliyofanyika jijini Oran, Algeria, kuanzia Novemba 16 hadi 20, 2026, na kurejea nchini leo, Novemba 22, 2026.
Aidha, washiriki wote wa Tanzania walifanikiwa kukamilisha kikamilifu kazi walizopewa ndani ya muda uliopangwa.
Amesema ushiriki wa vijana hao umekuwa sehemu muhimu ya washiriki kutoka Tanzania kujifunza na kubadilishana uzoefu na washiriki kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
“Vijana hawa wameonyesha uwezo mkubwa, na sasa ni jukumu lao kutumia ujuzi walioupata kujiajiri au kuajiriwa. Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya mafunzo ili vijana waweze kupata ujuzi unaohitajika,” amesema Dkt. Salukele.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda, ambaye pia ni Mwakilishi wa Kiufundi (Technical Delegate), amesema Tanzania imejifunza ushiriki wa viwanda na waajiri katika kufanikisha mashindano ya ujuzi kupitia uchangiaji wa vifaa, utaalamu na rasilimali fedha.
Amesema baraza hilo linajivunia umahiri wa vijana wanaozalishwa katika vyuo vya kati, akieleza kuwa ujuzi wao ni muhimu katika kuchochea uzalishaji na kukuza uchumi wa Taifa.
Ametoa wito kwa wadau wa sekta ya umma na binafsi kushirikiana katika kuendeleza mashindano ya ujuzi nchini.
Amesema mashindano hayo yamekuwa changamoto na fursa ya kujifunza kwa taasisi zinazosimamia vyuo vya kati, hususan katika kuhakikisha mafunzo yanazingatia maendeleo ya teknolojia ya kisasa na mahitaji ya soko.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la NACTVET, Bernadetta Ndunguru, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka msisitizo katika maendeleo ya viwanda, hivyo kuna umuhimu wa kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi itakayoweza kutekeleza malengo ya maendeleo ya Taifa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema mafunzo ya ufundi stadi ni sehemu muhimu ya mkakati wa Afrika wa kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi, huku akiwahimiza vijana wanaochagua fani za ufundi kutumia fursa hizo na kupewa maarifa ya ujasiriamali ili waweze kujiajiri na kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Amesema makongamano yaliyofanyika sambamba na mashindano hayo yametoa fursa ya kushiriki mijadala ya kisera iliyosisitiza nafasi ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET) katika kuwawezesha vijana kupata ajira, kujiajiri na kuwa wabunifu.
Amesema nchi za Afrika zimekubaliana kuimarisha mifumo na mipango ya utekelezaji wa TVET ili kukuza uchumi wa bara hilo, akibainisha kuwa msisitizo huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, jambo linalohitaji kuwa na vijana wengi wenye ujuzi na umahiri unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Naye Mkurugenzi wa Mafunzo wa VETA, Dkt. Abdallah Ngodu, amesema ushiriki wa Tanzania katika mashindano hayo umewapa fursa ya kujifunza mbinu mpya za kuboresha utoaji wa mafunzo pamoja na kuimarisha mitaala ili iendane na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira.
Kwa upande wake, Emmanuel Paulo Saimoni ambaye ni miongoni mwa washindani amesema nafasi aliyopata imempa motisha ya kuendelea kujiimarisha katika fani yake, huku akitambua kuwa ana uwezo wa kushindana katika soko la ajira la kimataifa na kufanya vizuri.
Katika mashindano hayo, mshiriki wa Tanzania, Emmanuel Paul kutoka Chuo cha VETA Dodoma, alishika nafasi ya nne kati ya washiriki 12 katika fani ya Usanifu na Utunzaji wa Mandhari, huku mshiriki Ikwabe Ibrahim wa fani ya Upakaji Rangi na Upambaji wa chuo cha VETA Dar es Salaam akishika nafasi ya saba kati ya washiriki 26.
.jpeg)


.jpeg)
.jpeg)



No comments:
Post a Comment