
Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini yametakiwa kuimarisha mifumo ya uongozi, usimamizi wa fedha, uwazi na uwajibikaji pamoja na kuwekeza katika ubunifu ili kuongeza uwezo wa kujiendesha na kuendeleza huduma kwa jamii.
Wito huo umetolewa na wadau mbalimbali wa sekta hiyo, walioeleza kuwa uongozi bora, uzingatiaji wa sheria za kodi na matumizi sahihi ya rasilimali ni miongoni mwa misingi muhimu ya kuhakikisha mashirika hayo yanakuwa endelevu na yanaendelea kuchangia maendeleo ya Taifa.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania (IDT), Saidi Kambi, amesema uendelevu wa mashirika hayo unaanzia katika uongozi bora, bodi imara na mifumo inayozingatia uwazi na uwajibikaji.
Amesema mashirika yanahitaji kujenga uaminifu kwa wadau na kupanua vyanzo vya mapato ili kupunguza utegemezi wa ufadhili na kuhakikisha yanaendelea kutekeleza malengo yake.
“Uaminifu unakuja kwa kiasi kikubwa kupitia uongozi imara, uwazi na uwajibikaji. Hata hivyo, si suala la kusimamia fedha pekee, bali pia kupanua vyanzo vya mapato ili kuhakikisha malengo ya taasisi yanafanikiwa,” amesema Kambi.
Ameeleza kuwa uongozi bora ni muhimu pia katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayojikita katika uchumi imara na shindani, maendeleo ya watu na jamii pamoja na uhifadhi wa mazingira, akibainisha kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali yana nafasi kubwa katika kufanikisha maeneo hayo.
Kambi amesema Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania imesaini hati ya makubaliano na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) kwa lengo la kushirikiana kuimarisha mifumo ya uongozi na uadilifu katika mashirika hayo.
Kwa upande wake, mtaalamu wa ukaguzi wa hesabu (Auditor), Anna Mzokayape, amesema uzingatiaji wa sheria za kodi, ukaguzi wa hesabu na usimamizi wa fedha ni muhimu katika kuongeza uaminifu wa mashirika kwa wafadhili na kuimarisha uendelevu wake.
Mzokayape amesema kupitia hati ya makubaliano (MoU) aliyoingia na NaCoNGO, yeye pamoja na kampuni yake wanalenga kuyajengea uwezo mashirika ya ndani na ya kimataifa katika masuala ya ukaguzi wa hesabu, sheria za kodi, upangaji wa bajeti na usimamizi wa matumizi ya fedha.
Amesema baadhi ya mashirika yanapokea fedha kutoka kwa wafadhili wa ndani na nje ya nchi, lakini hukumbana na changamoto ya kuelewa na kutekeleza masharti ya ufadhili, ikiwemo utunzaji wa kumbukumbu sahihi za fedha na kufanya ukaguzi wa hesabu.
“Tunataka kuyasaidia mashirika yaelewe sheria za kodi zinasemaje, namna ya kutengeneza hesabu, kuandaa bajeti na kujua wajibu wao wa kifedha ili yaweze kuwasilisha taarifa sahihi TRA na kutimiza masharti ya wafadhili,” amesema Mzokayape.
Ameongeza kuwa mashirika yanapokuwa na mifumo mizuri ya usimamizi wa fedha na kuzingatia sheria, yanajenga uaminifu kwa wafadhili na kuongeza nafasi ya kupata ufadhili zaidi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Katika eneo la ubunifu, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Bora Women Go Green NGO, Gretha Haule, amesema taasisi hiyo itatumia jukwaa hilo kuonesha teknolojia bunifu ya kupikia kwa kutumia nishati ya hydrogen inayozalishwa kwa kutumia maji na umeme unaotokana na jua.
Haule amesema teknolojia hiyo inalenga kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuonesha namna ubunifu unavyoweza kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi.
“Teknolojia yetu ni rahisi sana. Ukiwa na jua na maji unaweza kupika. Tunawaalika wadau wote wajitokeze katika jukwaa hilo ili kujionea teknolojia hii kwa vitendo,” amesema.
Amesema mbali na maonesho hayo, atashiriki pia katika mjadala wa jukwaa kama mjumbe wa jopo, akichangia mada kuhusu nafasi ya ubunifu katika kutatua changamoto za kijamii na kuimarisha matumizi ya nishati safi nchini.
Haule amesema taasisi hiyo imeamua kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, akieleza kuwa ubunifu huo ni sehemu ya mchango wao katika kutekeleza maono ya Tanzania ya kijani.
Jukwaa la Sita la Mwaka la Mashirika Yasiyo yab Kiserikali linatarajiwa kufanyika jijini Dodoma kuanzia Novemba 25 hadi 28, 2026, likiwa na kaulimbiu inayosisitiza uendelevu wa mashirika hayo kupitia ubunifu, ubia na upatikanaji wa rasilimali fedha kutoka vyanzo vya ndani.
Jukwaa hilo linatarajiwa kuwakutanisha washiriki takribani 3,500 kutoka serikalini, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, vyombo vya habari na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa ajili ya kujadili mikakati ya kuimarisha sekta hiyo na mchango wake katika maendeleo ya Taifa..jpeg)
.jpeg)
.jpeg)




No comments:
Post a Comment