
Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
TANZANIA imeendelea kupanua ushawishi wake katika masuala ya uchumi, biashara, uwekezaji na afya barani Afrika kupitia ziara za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini Uganda na Ethiopia.
Ziara hizo zilizofanyika Novemba 18 hadi 19, 2026, nchini Uganda na Novemba 22 hadi 23, 2026, nchini Ethiopia, zimeweka msukumo katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kufungua fursa mbalimbali kwa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matokeo ya ziara hizo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, amesema ziara ya Uganda ilijikita katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, biashara na uwekezaji, huku ile ya Ethiopia ikiimarisha nafasi ya Tanzania katika uongozi wa afya ya mama na mtoto barani Afrika.
Amesema katika ziara ya Uganda, Rais Samia na mwenyeji wake, Rais Yoweri Kaguta Museveni, walikubaliana kuharakisha utatuzi wa vikwazo visivyo vya kikodi vinavyokwamisha biashara kati ya nchi hizo mbili ili kupanua masoko na kuimarisha biashara.
Katika sekta ya nishati, viongozi hao walipokea taarifa kuwa utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umefikia asilimia 93.9, pamoja na taarifa ya kutiwa saini kwa mkataba wa mfumo wa ushirikiano kuhusu uendelezaji wa reli ya kisasa (SGR) katika njia ya Isaka, Rusahunga, Uromo, Kikagati hadi Mpondwe.
Aidha, Rais Samia alishiriki uzinduzi wa kiwanda cha kuunganisha magari cha Double Q nchini Uganda, ambako alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika Mashariki kujenga viwanda vinavyosaidiana na kuunganisha mnyororo wa thamani.
Kwa upande wa Ethiopia, Rais Samia alishiriki Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026) na kuzindua Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika wa mwaka 2026–2030, unaohusu nchi zote 55 za Umoja wa Afrika.
Mpango huo umejikita katika malengo matatu ya sifuri, ambayo ni sifuri ya kujifungulia nyumbani, sifuri ya vifo vya uzazi na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika na sifuri ya watoto wasiochanjwa.
Katika hatua nyingine, Rais Samia alitangaza ufadhili wa awali wa nafasi 60 za mafunzo ya ubobezi kwa wataalamu wa afya barani Afrika, katika fani za ukunga, ganzi, afya ya uzazi na huduma za watoto wachanga.
Machumu amesema ziara hizo zinaonesha umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kukuza uchumi na biashara, pamoja na kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.
.jpeg)
.jpeg)


No comments:
Post a Comment