
Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, amezialika kampuni za Algeria za teknolojia ya kilimo, ufugaji na usindikaji wa mazao ya chakula kuja nchini kuona fursa zilizopo za biashara na uwekezaji.
Akizungumza na vyombo vya habari vya Algeria kwenye ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Algiers, Balozi Matinyi alisema Serikali ya Tanzania imeweka mkazo kwenye uboreshaji wa sekta ya kilimo na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo na kwamba utaalam na uzoefu wa kampuni za Algeria unahitajika Tanzania.
Akielezea maendeleo ya ushirikiano baina ya Tanzania na Algeria kwa mwezi Oktoba, Balozi Matinyi alisema Ubalozi ulialikwa kwenye maonesho ya kilimo na pia kufanya ziara kwenye viwanda vya kusindika bidhaa za kilimo na ufugaji na kutumia fursa hiyo kuzialika kampuni mbalimbali za Algeria kuja nchini.
Balozi Matinyi alisema kwamba mbali ya juhudi katika sekta ya kilimo, Serikali ya Tanzania inatekeleza pia miradi ya ujenzi wa mji mkuu wa Dodoma, inapanua sekta ya dawa na nishati, inafufua viwanda na inaimarisha miundombinu ya uzalishaji na usafirishaji ili kukidhi mahitaji ya kitaifa na kikanda.
“Kufanya biashara na kuwekeza Tanzania kutaimarisha ushirikiano wa kiuchumi uliopo baina ya nchi zetu mbili rafiki na kuchochea ukuaji wa biashara barani Afrika,” alidokeza Balozi Matinyi mbele ya vyombo hivyo vya habari.
Awali Balozi Matinyi alimshukuru Waziri wa Biashara ya Nje na Uhamasishaji wa Mauzo ya Nje, Mhe. Kamel Rezig, kwa kumwalika kwenye Maonyesho ya Biashara ya Chakula na Kilimo yaliyoandaliwa na wizara hiyo na kufanyika mjini Blida tarehe 17 Oktoba, 2026 huku yakivutia washiriki zaidi ya 100.
Balozi Matinyi alitaarifu kuwa katika maonesho ya Blida na mengine ya jijini Annaba na Constantine, Ubalozi ulizielezea fursa zilizopo Tanzania na kuzikaribisha kampuni nyingi zikiwemo za usindikaji nyama na mazao ya kilimo, teknolojia ya ufugaji, uzalishaji chakula cha mifugo na mbolea, umwagiliaji na ufungashaji wa bidhaa za chakula.
“Mbali ya Blida tulipata fursa ya kuongea na kampuni kadhaa tarehe 13 jijini Annaba kwenye maonesho ya Agri Tech Expo na tarehe 28 jijini Constantine kwenye maonesho ya Agrest Expo na zote tumezialika zije Tanzania kuona fursa zilizopo na namna ya kushirikiana na Watanzania,” alisema Balozi Matinyi.
Balozi Matinyi aliongeza, “Tulifanya pia ziara mjini Blida tarehe 21 Oktoba kuona teknolojia ya juu ya usindikaji nyama ya kuku kwenye kiwanda cha Groupe Bellat na pia kushuhudia teknolojia ya usindikaji nyanya na pilipili kwenye kiwanda cha Groupe Amour na tumewakaribisha waje kuona fursa zilizopo Tanzania”.
Aidha, Balozi Matinyi pia alikuwa mgeni wa heshima kwenye maonesho ya sekta ya ujenzi jijini Constantine mnamo tarehe 14 Oktoba na siku iliyofuatia Ubalozi ulifanya ziara kwenye kiwanda cha dawa za tiba cha Physiopharm ili kukivutia kije kuwekeza nchini.
Kampuni ya TANOIL ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) nayo ilituma ujumbe wake uliongozwa na Kaimu Maneja Mkuu, James Sanawa, kuhudhuria Maonesho na Mkutano wa Nishati na Haidrojeni wa Afrika Kaskazini na Mediterania, uliofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 7 Oktoba jijini Oran, Algeria.
TANOIL ambayo husambaza bidhaa za gesi na petroli nchini, ilipata fursa ya kujadiliana namna ya kushirikiana kiufundi na kampuni mbalimbali likiwemo Shirika la Algeria la Gesi na Mafuta (Sonatrach) na kampuni yake tanzu ya usambazaji ya Naftal.
Ukiwa jijini Oran, Ubalozi pia ulifanya ziara tarehe 6 Oktoba kwenye kiwanda cha Tapidor kinachotengeneza mazulia ya nyuzi zitokanazo na kemikali za petroli kwa lengo la kukivutia kuanzisha biashara nchini Tanzania na kulenga soko kubwa zaidi ya kikanda.
Kadhalika, Mamlaka ya Taifa ya Bidhaa za Dawa ya Algeria (ANPP) ikiambatana na kampuni ya serikali ya dawa ya Saidal Group na baadaye kampuni binafsi ya dawa ya Frater Razes nazo zilifanya ziara nchini Tanzania ili kuanzisha ushirikiano wa kiufundi, kibiashara na kiuwekezaji katika sekta ya afya.


No comments:
Post a Comment