SERIKALI Mkoani Tabora imewataka wadau na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika wa tumbaku kukomesha vitendo vya utumikishwaji watoto mashambani, huku ikionya dhidi ya matumizi ya wafanyakazi wa kigeni bila kufuata taratibu za kisheria.

Maagizo hayo yametolewa na Wakuu wa Wilaya za Sikonge na Kaliua katika kikao cha wadau wa zao la tumbaku kilichoandaliwa na Kampuni ya Ununuzi na Uchakataji ya Alliance One, kilicholenga kuboresha maendeleo ya mkulima na kuimarisha utaratibu wa uzalishaji.
Kikao hicho kiliwakutanisha viongozi mbalimbali wa wilaya hizo mbili pamoja na wadau mbalimbali, wakiwemo Makatibu Tawala wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya,maafisa wa uhamiaji, wataalamu wa maendeleo ya jamii, Maafisa Watendaji wa Vijiji, Maafisa Watendaji wa Kata, pamoja na wawakilishi wa wakulima.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Dk. Gerald Mongella, amekemea vikali ajira za utotoni na kuonya kuwa hatua kali za kisheria, ikiwemo kufunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi, zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kukiuka maagizo hayo.
Dk. Mongella amesema serikali haitavumilia kuona haki za watoto zinaminywa kupitia ajira hizo, jambo linaloweza kuathiri vibaya soko la kimataifa la tumbaku inayozalishwa nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Michael Semindu, amewasihi viongozi wa wakulima kuhakikisha wanatumia njia halali wanapoleta wafanyakazi wa mashamba ya tumbaku kutoka nchi za jirani ili kuepuka migogoro na changamoto za kisheria.
“Hili la wahamiaji haramu likomeshwe na pale mnapohitaji kuwa na wafanyakazi wa namna hiyo, bora muwaendee Maafisa wa Uhamiaji watoe elimu ya kina kuhusu namna ya kuwaleta nchini kwa ajili ya kazi za misimu nchini,” amesisitiza Mhe. Semindu.
Msimamo huo umeungwa mkono na Idara ya Uhamiaji kupitia wilaya ya Kaliua, Rogatian Chuwa aliyeongea kwa niaba ya wenzake. Aliwataka waajiri kuwaombea vibali vya kazi wafanyakazi wa kigeni pamoja na kuwapa mikataba ili kuepuka makosa yanayoweza kufananishwa na kazi za kulazimishwa.
Naye Meneja na Msemaji wa Kampuni ya Alliance One, Wakili John Magoti, amewataka viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) kuwakumbusha wakulima kuacha kabisa kutumikisha watoto chini ya umri wa miaka 18 na badala yake kuwapa kazi nyepesi zisizozidi masaa sita kwa siku endapo hawapo shuleni.
“Watoto wasitumikishwe mashambani. Haki za binadamu na mikataba ya Umoja wa Mataifa inakataza jambo hili. Kampuni yetu imeweka mifumo thabiti kupitia sera ya ALP (Agricultural Labour Practices) kuzuia ajira za watoto na kuweka namba maalum za kuripoti matukio hayo,” amesema Wakili Magoti.
Pamoja na usimamizi wa sheria, Alliance One imepongezwa kwa mchango wake mkubwa wa kiuchumi mkoani humo. Wakili Magoti ameeleza kuwa mwaka huu kampuni hiyo imelipa shilingi bilioni 1.1 kama ushuru kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, pamoja na kulipa Dola za Marekani milioni 13 kama ushuru kwa AMCOS.
Wakiongea katika kikao hicho maafisa wengine mbalimbali walitoa ushauri kuhusu ajira za watoto na wafanyakazi wa kigeni. Ofisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii wilaya ya Kaliua, Magdalena Kanje amesema wamekubaliana kuendelea kutoa elimu kwa jamii na kuhamasisha miradi endelevu kama VICOBA ili kutokomeza ajira za watoto na kuinua kipato cha wakulima wa tumbaku.
Meneja Uhusiano na Msemaji wa Kampuni ya Tumbaku ya Alliance One Wakili John Magoti (Katikati) akiwasilisha mada kwenye mkutano wa wadau wa tumbaku wa wilaya za Sikonge na Kaliua uliofanyika mkoani Tabora.Kulia ni Mkuu wa Wialaya ya Sikonge Bw.Michael Semindu, kushoto ni Afisa Tawala wa wilaya hiyo Bw.Andrea Ng'hwani.
Mkuu wa Mkoa wa Wilaya ya Sikonge Michael Semindu, akitoa hotuba ya ufunguzi katika kikao cha wadau wa tumbaku kwa wilaya za Sikonge na Kaliua, kilichofanyika mwishoni mwa wiki, huku Meneja Mahusiano kwa Umma na Msemaji wa Kampuni ya Alliance One Wakili John Magoti(kushoto) akifuatilia kwa makini.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Sikonge, Andrea Ng'hwani akifafanua jambo katika kikao cha wadau wa tumbaku kwa wilaya za Sikonge na Kaliua kilichoandaliwa na Kampuni ya Tumbaku ya Alliance One.Kulia ni Meneja Uhusiano na Msemaji wa Kampuni hiyo, Wakili John Magoti. .jpeg)




No comments:
Post a Comment