Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Rolf Kibaje, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukamilika kwa mchakato wa upigaji kura na waandishi 64 pamoja na vyombo vya habari 11 vilivyofuzu kuwania tuzo za Samia Kalamu Awards (SKA) 2026. Hafla ya kutangaza washindi inatarajiwa kufanyika Desemba 5, 2026, katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kutangaza washindi wa tuzo za uandishi wa habari za maendeleo za Samia Kalamu Awards (SKA) 2026, itakayofanyika Desemba 5 mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Katika tuzo hizo, waandishi wa habari 64 na vyombo vya habari 11 vimefuzu kuingia hatua ya mwisho ya kuwania tuzo hizo, baada ya kukamilika kwa mchakato wa tathmini na upigaji kura kwa umma.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Peter Mwasalyanda, Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano, Rolf Kibaje kuhusu kukamilika kwa mchakato huo, amesema jumla ya kazi 3,003 ziliwasilishwa kwa ajili ya kushindanishwa katika tuzo hizo.
Amesema baada ya tathmini ya majaji, kazi 882 zilifuzu kuingia katika hatua ya upigaji kura kwa umma, ambapo jumla ya kura 317,399 zilipigwa
"Waandishi waliofuzu wamepatikana kupitia mchakato wa upigaji kura kwa umma pamoja na tathmini ya majaji 19 waliobobea katika taaluma ya uandishi wa habari na mahusiano kwa umma...tathmini hiyo ilizingatia vigezo mbalimbali, vikiwemo ubora wa maudhui, uzingatiaji wa maadili ya taaluma, matumizi ya utafiti na takwimu, athari chanya kwa jamii na mchango katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Tuzo hizo zinajumuisha tuzo za kisekta, tuzo za vyombo vya habari na tuzo maalum za kitaifa, huku zikitambua kazi za waandishi wa habari, maafisa habari na vyombo vya habari zilizochapishwa au kurushwa hewani ndani ya kipindi kilichoainishwa kwenye mwongozo wa tuzo.
Mhandisi amesema washindani na mwitikio wa wananchi kupitia upigaji kura unaonesha umuhimu wa tuzo hizo katika kuhamasisha uandishi wa habari unaozingatia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Aidha ameeleza kuwa, Orodha ya waandishi wa habari na vyombo vya habari vilivyofuzu kuingia hatua ya mwisho inapatikana kupitia tovuti ya www.samiawards.co.tz. na washiriki waliofuzu watapokea maelekezo kuhusu ushiriki wao katika hafla hiyo kutoka kwa kamati ya maandalizi.
Samia Kalamu Awards ni tuzo maalum za kitaifa zilizoanzishwa mwaka 2024 kwa lengo la kutambua, kuenzi na kuhamasisha ubora, weledi na ubunifu katika uandishi wa habari na makala za maendeleo nchini.
Tuzo hizo zinaratibiwa na TCRA kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na JAMU, kupitia kaulimbiu ya mwaka huu isemayo Kalamu kwa Maendeleo.
Kaulimbiu hiyo inahimiza uzalishaji wa maudhui ya ndani yenye ubora yanayozingatia utafiti na takwimu, usahihi, weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
.jpeg)



No comments:
Post a Comment