MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kuendelea kulima na kuzalisha mazao kwa wingi, akieleza kuwa Serikali itahakikisha kuwa wakulima wananufaika na mfumo bora wa soko na bei za mazao, hususan Mahindi.
Amesema hayo tarehe 10 Novemba 2026 akiwa katika ziara ya kikazi Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma ambapo amekagua na kuzindua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbinga wenye gharama ya Shilingi Bilioni 3.62; kukagua ujenzi wa barabara ya kilometa 35 ya Amani Makoro-Ruanda; pamoja na mradi wa maji katika kijiji cha Mtyangimbole, Wilaya ya Madaba.
Akizungumza katika ziara hiyo, Makamu wa Rais Ndejembi amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza katika Sekta ya Kilimo ili kuongeza uzalishaji, kuboresha masoko na kuimarisha usalama wa chakula nchini. Amesisitiza kuwa pamoja na kuongeza uzalishaji, hatua mahsusi zinaendelea kuchukuliwa ili kuimarisha uhifadhi wa mazao, kuongeza thamani kupitia usindikaji wa ndani na kulinda wakulima dhidi ya kushuka kwa bei wakati wa mavuno mengi.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) ameeleza kuwa Wizara itaendelea kuisimamia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili kuhakikisha unaendelea kuwa kichocheo cha bei nzuri za mazao na kutoa uhakika wa soko kwa wakulima. Kuhusu kauli ya Mhe. Judith Kapinga (Mb), Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbinga vijijini kuhusu ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mazao na kiwanda cha kusaga unga, Waziri Chongolo amesema kuwa ni nguzo muhimu ya kuhakikisha thamani ya mazao ya nafaka iyakiwemo Mahindi inaongezeka huku wakulima wakipata mapato bora na yenye tija zaidi.
Kuhusu upatikanaji wa pembejeo, Waziri Chongolo amewahakikishia wakulima wa Mbinga na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kuwa Serikali imeendelea kutoa ruzuku ya mbolea kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji. Amefafanua kuwa ruzuku hiyo imepunguza bei ya mbolea kwa wastani wa Shilingi 63,000 hadi 65,000 kwa mfuko, wakati bei ya soko ya mfuko wa DAP ni takribani Shilingi 158,000.
.jpeg)


.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)


No comments:
Post a Comment