JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


MWALONGO: BIMA YA AFYA KWA WOTE IZINGATIE UWEZO WA KIPATO CHA MWANANCHI

Share This

Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO), Bonaventura F. Mwalongo, Amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unazingatia uwezo wa kipato cha wananchi, upatikanaji wa huduma bora na ushirikishwaji wa wadau wa Tiba Asili.

Mwalongo amesema pamoja na umuhimu wa mpango huo katika kuboresha huduma za afya nchini, ni muhimu kuweka viwango vya michango vinavyozingatia hali za kiuchumi za wananchi, hususan wakulima, wafanyabiashara wadogo na watu wanaojiajiri ambao hawana kipato cha uhakika kila mwezi.

Ameshauri wananchi wenye uwezo mkubwa kuchangia zaidi, wenye kipato cha chini kulipia michango nafuu, huku wasiokuwa na uwezo wakisaidiwa na Serikali kupitia ruzuku.

Aidha, amesisitiza kuwa mafanikio ya bima hiyo hayatapimwa kwa idadi ya watu waliojiunga pekee, bali pia upatikanaji wa dawa, wataalamu na huduma bora katika hospitali na vituo vya afya, ikiwemo maeneo ya vijijini.

Kuhusu Tiba Asili, Mwalongo amesema sekta hiyo inapaswa kupewa nafasi katika mijadala ya Bima ya Afya kwa Wote kupitia utafiti, uthibitishaji wa ubora, usalama na viwango vya dawa na huduma zinazostahili kutambuliwa.

Amesema ushirikishwaji wa wataalamu wa Tiba Asili utasaidia kupanua mawazo na fursa za kuboresha sekta ya afya nchini, bila kupuuza umuhimu wa tiba ya kisasa.

Aidha, ameitaka Serikali kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu michango, huduma wanazostahili kupata na taratibu za kutumia bima hiyo ili kujenga uelewa na imani kwa mfumo huo.

Akihitimisha, Mwalongo amesema Bima ya Afya kwa Wote inapaswa kuwa kinga ya maisha na si mzigo kwa familia, huku akisisitiza umuhimu wa kujenga mfumo unaoaminika na kumudu na kila mwananchi.

Bonaventura F. Mwalongo
Katibu Mkuu – TRAMEPRO
Mtaalamu wa Tiba Asili

 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad