MAKUNDI ya wasichana na wanawake vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 katika Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani na maeneo ya jirani wanatarajiwa kunufaika na mradi wa mwaka mmoja wa uwezeshaji kiuchumi unaolenga kukuza ajira, kujitambua na tija kwa jamii.
Mradi huo ujulikanao kama ' Girls Round Table- Season 12', utatekelezwa kwa pamoja na shirka lisilo la lissrikali la Nuruyetu Foundation na Serikali kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii na mamlaka za serikali za mitaa katika maeneo ya mradi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi katika Shule ya Msingi Sofu, Manispaa ya Kibaha hivi karibuni, Afisa Mtendaji wa Kata ya Sofu, Bi Aloysia Nyeto, alisema mradi huo unatarajiwa kubadilisha maisha ya wasichana na wanawake vijana ambao wamepoteza mwelekeo wa maisha, huku pia ukijenga uwezo wa jamii katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
“Mradi huu utawafikia wasichana wetu na mabinti zetu, wengi wao waliokosa fursa za kufikia ndoto zao. Sambamba na hilo, jamii ambazo walengwa hawa wanatoka pia zitanufaika kwa namna moja ama nyingine kupitia programu za mradi huu. Tunashukuru sana Serikali kwa kutoa vibali kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kufanya kazi na makundi mbalimbali ya watu katika maeneo yetu, na hii inaonesha dhahiri dhana ya utekelezaji wa malengo ya Dira ya 2050,” alisema.
Aliongeza kuwa, kupitia uwezeshaji wa kiuwezo na mtaji utakaotolewa kupitia mradi huo kwa walengwa hao, jamii katika maeneo husika zitajifunza umuhimu wa kuyajali makundi ya wanawake na wasichana kwa faida ya familia na jamii nzima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nuruyetu Foundation, Bi Zauja Mohamed, alisema wanawake vijana na wasichana kutoka maeneo ya Picha ya Ndege, Kwamfipa, Visiga na Sofu watanufaika katika awamu ya kwanza ya mradi huo, ambao unafadhiliwa kwa pamoja na Global Affairs Canada na Cuso International.
Akifafanua mradi huo, alisema walengwa watapata fursa ya kujifunza ujuzi wa kidijitali na fedha, utengenezaji wa kazi za mikono na ujuzi wa ujasiriamali.
“Tutaendelea kutafuta fursa mbalimbali kwa walengwa wa mradi huu kadri muda unavyokwenda. Lengo ni kuwawezesha kunufaika kulingana na uwezo wao wa kutumia ujuzi watakaoujifunza,” alisema.
Aliongeza kuwa mwishoni mwa mradi, walengwa watapewa vifaa vya kuanzishia biashara ili kuanzisha biashara zao wenyewe.
Alisema shirika hilo pia litaunga mkono Serikali katika kuimarisha masomo ya ufundi stadi kwa wasichana katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, kama sehemu ya mradi huo.
Wakizungumza kwa niaba ya walengwa wengine, Olpa George wa Visiga na Rahma Hatibu wa Picha ya Ndege wote walionyesha matarajio makubwa ya mafanikio watakayoyapata kupitia mradi huo.


No comments:
Post a Comment