Na Mwandishi Wetu
MKUTANO wa Maafisa Watendaji Wakuu wa Makampuni (CEOs) kutoka sehemu mbalimbali duniani, The World CEO Summit Africa 2026, unatarajiwa kuwa chachu ya kukuza uchumi wa Tanzania kupitia kubadilishana uzoefu, maarifa na fursa za uwekezaji.
Mratibu wa mkutano huo, Deogratius Kilawe, amesema Tanzania itanufaika na mkutano huo kutokana na fursa ya kuwakutanisha viongozi wa makampuni na taasisi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kujadili mikakati ya kuboresha uendeshaji wa biashara na kukuza uchumi.
Kilawe amesema hayo wakati akizungumzia maandalizi ya mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 26 na 27 katika Ukumbi wa Ocean View Arena Kawe jijini Dar es Salaam mwaka huu,
Ameeleza kuwa kuwa washiriki watapata fursa ya kujifunza uzoefu wa makampuni ya kimataifa yaliyofanikiwa katika uendeshaji na usimamizi wa biashara.
Amesema mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu la kukutanisha wadau na watoa maamuzi kutoka sekta mbalimbali ili kujadili changamoto zinazokabili biashara na uwekezaji, pamoja na kutafuta suluhisho zitakazosaidia kuboresha mazingira ya biashara nchini.
Aidha, amesema mkutano huo utatoa fursa kwa vijana na wanawake kujifunza kutoka kwa viongozi wenye uzoefu katika sekta mbalimbali, kupata maarifa na kutumia fursa zitakazojitokeza katika kujenga uwezo wao wa kiuchumi.
Amehimiza wadau wa sekta binafsi na umma kutumia fursa ya mkutano huo kushiriki kikamilifu katika majadiliano yatakayochochea ukuaji wa biashara, uwekezaji na uchumi wa Tanzania.




No comments:
Post a Comment