JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


KAHAMA YAKARIBISHA UWEKEZAJI, YATAJA FURSA ZA KIUCHUMI NA USHIRIKIANO NA TASAC

Share This

 


MKUU wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Dkt. Francis Mlacha, amesema Wilaya ya Kahama ina fursa nyingi za uwekezaji na iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), katika kuimarisha uchumi na kukuza sekta ya viwanda.

Akizungumza leo, tarehe 6 Novemba, 2026, alipokutana na Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC, amesema Kahama imejipanga kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali, hususan viwanda, ili kuongeza uzalishaji, ajira na biashara.

Amesema Wilaya hiyo ina maeneo yenye fursa kubwa za uwekezaji, yakiwemo Buzwagi, Nyashimbi na Chapurwa, pamoja na rasilimali za madini na kilimo zinazoweza kuchochea maendeleo ya viwanda.

Aidha, amesema Kahama ina nafasi ya kimkakati kijiografia inayoiwezesha kufikia masoko ya nchi tano jirani ambazo ni Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Uganda, Rwanda na Burundi, hivyo kuwa na fursa pana za biashara na uwekezaji.

Amesisitiza kuwa Serikali ya Wilaya iko tayari kupokea mapendekezo ya wadau yatakayosaidia kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuondoa changamoto za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC, Nahodha Mussa Mandia, amesema ufanisi wa shughuli za bandari na sekta ya usafirishaji unahitaji ushirikiano na uratibu mzuri kati ya Serikali na wadau wa biashara.

Amesema ziara ya Bodi imelenga kujionea utendaji wa shughuli za bandari, kubaini changamoto za wadau na kutafuta suluhisho la kuboresha huduma, kurahisisha biashara na kuvutia uwekezaji.

Katika ziara hiyo, Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC ilitembelea eneo la GALCO Inland Container Depot (ICD) Isaka, kujionea miundombinu na shughuli za bandari kavu zinazosaidia kurahisisha usafirishaji wa mizigo na kukuza biashara.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad