JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Huduma za Watoto Njiti Zaokoa Maisha Kwimba

Share This
 


Na Mwandishi Wetu
HUDUMA za afya kwa watoto njiti na wanaozaliwa wakiwa na changamoto mbalimbali zimeonyesha mafanikio makubwa katika Wilaya ya Kwimba, Mwanza, baada ya kuanzishwa kwa Kitengo cha Huduma kwa Mama na Mtoto, hatua iliyosaidia kupunguza kwa asilimia 64 kiwango cha vifo vya watoto wanaolazwa katika kituo hicho.

Akizungumza Novemba 15, 2026, Muuguzi Daraja la II na Mkuu wa Wodi ya Watoto Wachanga katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, Ernest John Kibona, amesema katika miezi tisa ya kwanza tangu kitengo hicho kuanza kufanya kazi, jumla ya watoto 542 wenye matatizo mbalimbali ya kiafya wamehudumiwa, ikilinganishwa na watoto 183 waliopatiwa huduma katika kipindi kama hicho kabla ya kuanzishwa kwa kitengo hicho.

Kibona amesema kati ya watoto 542 waliolazwa tangu kitengo hicho kilipoanza kufanya kazi Februari 26, 2026, watoto 250 sawa na asilimia 46 walikuwa wamezaliwa kabla ya wakati, huku watoto 66 sawa na takribani asilimia 12 ya waliolazwa wakifariki. Amesema hali hiyo ni tofauti na kipindi cha miezi tisa iliyotangulia, ambapo kati ya watoto 183 waliolazwa, 63 walifariki, sawa na asilimia 34.

Amesema takwimu hizo zinaonyesha kupungua kwa takribani asilimia 64 kwa uwiano wa vifo vya watoto waliolazwa, licha ya kuongezeka kwa kiasi kikubwa kwa idadi ya watoto wanaopatiwa matibabu katika kituo hicho.

Mbali na kuongeza upatikanaji wa huduma za matibabu, kuanzishwa kwa kitengo hicho kumepunguza pia ulazima wa familia kusafiri nje ya wilaya kutafuta huduma maalumu kwa watoto wachanga, hususan katika Jiji la Mwanza ambako hospitali za rufaa ziko zaidi ya kilomita 90 kutoka Kwimba.

Kabla ya kuanzishwa kwa kitengo hicho, watoto wachanga waliohitaji huduma maalumu walikuwa wakipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou Toure na Bugando Medical Centre. Safari hizo ziliongeza gharama na changamoto za usafiri kwa familia, huku Kibona akisema idadi ya rufaa kwenda hospitali za Mwanza imepungua kwa zaidi ya asilimia 67, wakati kitengo hicho sasa kinahudumia pia wagonjwa kutoka wilaya tano jirani.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Doris Mollel Foundation, Doris Mollel, kabla ya huduma hizo kusogezwa karibu na wananchi, baadhi ya mama walilazimika kupitia hatua kadhaa za rufaa kabla ya watoto wao kupata huduma stahiki. Amesema mama anaweza kuanza safari ya kujifungua katika zahanati, lakini mtoto akizaliwa njiti huhitaji kupelekwa kituo cha afya kwa huduma maalumu, huku baadhi ya vituo hivyo vikiwa umbali wa hadi saa mbili kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kwimba.

Amesema iwapo kituo cha afya hakina uwezo wa kutoa huduma inayohitajika, mtoto hulazimika kupewa rufaa nyingine kwenda hospitali ya mkoa, hali ambayo huongeza hatari kwa mtoto pamoja na mzigo wa kifedha na kimazingira kwa familia. Kwa hiyo, amesema kuanzishwa kwa Kitengo cha Huduma kwa Mama na Mtoto, kwa msaada wa Doris Mollel Foundation, kumechangia kusogeza huduma za watoto wachanga karibu na jamii na kupunguza safari ndefu za kutafuta matibabu.

Mafanikio hayo yanakuja wakati Tanzania ikiendelea kukabiliwa na changamoto ya vifo vya watoto wachanga, hasa ndani ya siku 28 za kwanza baada ya kuzaliwa. Kwa mujibu wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto pamoja na Viashiria vya Malaria Tanzania wa mwaka 2022, kiwango cha vifo vya watoto wachanga nchini kilikuwa vifo 24 kwa kila vizazi hai 1,000, kutoka vifo 25 kwa kila vizazi hai 1,000 vilivyorekodiwa katika utafiti wa mwaka 2015/16.

Hata hivyo, Kibona amesema kitengo hicho bado kinakabiliwa na changamoto za uhaba wa wataalamu na vifaa muhimu vya matibabu, hali inayopunguza uwezo wa kutoa huduma kamili kwa idadi inayoongezeka ya watoto wanaohitaji matibabu. Amesema kuna uhitaji wa mtaalamu wa huduma za watoto wachanga, madaktari zaidi pamoja na wauguzi wa kuongeza nguvu katika kitengo hicho.

Amesema pia kitengo hakina kiwanda cha kuzalisha oksijeni na kinahitaji vifaa zaidi, ikiwamo radiant warmers kwa ajili ya kudhibiti joto la mwili wa watoto wachanga pamoja na mashine za phototherapy zinazotumika kutibu manjano kwa watoto wachanga. Changamoto hizo zinaonyesha umuhimu wa kuambatana kwa uwekezaji katika miundombinu ya afya na uwezeshaji wa kutosha kwa wataalamu, vifaa na dawa ili huduma ziendelee kuwa bora.

Wakati huo huo, katika kuadhimisha Siku ya Watoto Njiti Duniani mwaka huu, Doris Mollel Foundation imeandaa hafla ya jioni jijini Dar es Salaam, ambapo vitabu vitatu vinavyolenga kuongeza uelewa kuhusu watoto njiti, ushiriki wa wazazi na huduma kwa watoto wachanga vinatarajiwa kuzinduliwa.

Machapisho hayo ni My Baby Is Born Too Soon. What Do I Do? (Nimezaa Njiti, Nifanyeje?), kinachotoa mwongozo kwa wazazi na walezi; How We Want Neonatal Care Units to Look Like, kilichoandaliwa na Tanzania Preterm Family Network; pamoja na mwongozo kuhusu utoaji wa huduma na msaada wa kisaikolojia kwa mama walio na watoto njiti.

Machapisho hayo yanalenga kushughulikia mahitaji ya kitabibu, kihisia na kisaikolojia ya familia zinazokumbwa na changamoto ya kujifungua watoto njiti, sambamba na kutoa mwongozo kwa wahudumu wa afya na wadau wanaohusika na upangaji na uendelezaji wa vituo vya huduma za watoto wachanga. Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence George Samizi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad