JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


ECOBANK TANZANIA YAIMARISHA USHIRIKIANO NA SHULE BINAFSI KUPITIA HUDUMA MAALUM ZA KIFEDHA

Share This

 Ecobank Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano na Taasisi za elimu nchini kwa kuweka mikakati ya kutoa suluhisho za kifedha zinazolenga kusaidia shule binafsi kukua na kujiendesha kwa uendelevu, ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kupanua huduma za kifedha katika sekta ya elimu.


Katika kuendeleza mkakati huo, benki hiyo imeandaa mkutano maalumu wa kifungua kinywa kwa Wakurugenzi Wakuu na viongozi wa shule binafsi (Private School CEOs’ Breakfast on Sustainable School Finance), uliofanyika Novemba 16, 2026, katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, uliowakutanisha viongozi wa Taasisi za elimu na wadau mbalimbali kujadili mikakati ya upatikanaji wa fedha na ukuaji endelevu wa shule.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Ecobank Tanzania, Dkt. Charles Asiedu, alisema mpango huo ni sehemu ya juhudi za benki hiyo kuimarisha ushirikiano na taasisi za elimu nchini kwa kuelewa mahitaji yao ya kifedha na kutoa huduma zinazozingatia mazingira na uwezo wa kila shule.

Alisema Ecobank inalenga kupanua ushirikiano na shule nyingi zaidi nchini kupitia vyama mbalimbali vya wamiliki na waendeshaji wa shule, akieleza kuwa mawasiliano ya karibu na viongozi wa shule yataisaidia benki kubuni suluhisho za kifedha zitakazochochea ukuaji, kuongeza ufanisi wa uendeshaji na kuhakikisha taasisi hizo zinaendelea kuwa endelevu.

Kupitia huduma maalumu za kifedha kwa sekta ya elimu (Education Financial Services), Ecobank inatoa suluhisho mbalimbali zikiwemo mikopo ya ujenzi na upanuzi wa madarasa, maabara, maktaba na mabweni; ufadhili wa ununuzi wa mabasi ya shule, kompyuta na vifaa vya kufundishia; mitaji ya kuendesha shughuli za kila siku; pamoja na huduma za kidijitali za ukusanyaji wa ada na usimamizi wa fedha. Aidha, benki hiyo inatoa huduma za kibenki kwa wafanyakazi wa shule ili kuwawezesha kupata huduma zinazochangia ustawi wao wa kifedha.

Dkt. Asiedu alisisitiza kuwa Ecobank haitaki kuwa mtoa huduma za kibenki pekee, bali mshirika wa kimkakati wa taasisi za elimu katika kutekeleza mipango yao ya maendeleo. Aliwahimiza wamiliki na wasimamizi wa shule kushirikiana na benki zao mapema kwa kueleza mipango ya upanuzi na uwekezaji wanaokusudia kufanya ili kupata suluhisho zinazolingana na mahitaji na uwezo wao wa kifedha.

Aidha, mkutano huo umefanyika wakati sekta ya elimu nchini ikijiandaa na mabadiliko yanayotarajiwa katika idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule, yakiwemo makadirio ya kundi kubwa la wanafunzi wanaotarajiwa kuingia katika mfumo wa elimu mwaka 2028 (double cohort). Hali hiyo inatarajiwa kuongeza mahitaji ya miundombinu, vifaa vya kujifunzia na uwezo wa shule kutoa huduma bora, hivyo kuhitaji mipango madhubuti ya kifedha. Kupitia mpango huo, Ecobank inalenga kuendelea kushirikiana na wadau wa elimu kujenga shule imara na endelevu zitakazochangia maendeleo ya elimu na uchumi wa Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa Ecobank Tanzania, Dkt. Charles Asiedu akizungumza na Wakurugenzi Wakuu na viongozi wa shule binafsi (Private School CEOs’ Breakfast on Sustainable School Finance) kwenye mkutano maalum uliofanyika Novemba 16, 2026 jijini Dar es Salaam.


Baadhi ya wafanyakazi wa Ecobank Tanzania pamoja na Wakurugenzi Wakuu na viongozi wa shule binafsi (Private School CEOs’ Breakfast on Sustainable School Finance) wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Ecobank Tanzania, Dkt. Charles Asiedu.
Picha ya pamoja

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad