.jpeg)
Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), ikiambatana na Kamati ya Ukaguzi ya Chuo hicho, imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya katika Kampasi ya Tanga. Bodi imeeleza hayo wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi na kutathmini hatua zilizofikiwa.
Akizungumza baada ya ukaguzi, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TPSC, Dkt. Florens Turuka, amesema Bodi imefarijika kuona ujenzi ukiendelea vizuri. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Mei 2027.
“Tumefarijika kuona kuwa ujenzi wa jengo hili unaendelea vizuri. Tunatarajia kuwa ifikapo mwezi Oktoba mwakani, wanafunzi watakaodahiliwa wataweza kutumia majengo haya,” amesema Dkt. Turuka.
Mkuu wa Chuo cha TPSC, Dkt. Ernest Mabonesho, amesema jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya wanafunzi 2,500 kwa awamu moja. Amesema usanifu wake umezingatia mahitaji ya watu wenye mahitaji maalumu ili kuwawezesha kupata mazingira rafiki ya kujifunzia.
“Jengo hili litakuwa na miundombinu ya kisasa ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), itakayowezesha matumizi ya teknolojia katika ufundishaji, ujifunzaji na shughuli nyingine za kitaaluma,” amesema Dkt. Mabonesho.
Mradi wa awamu ya kwanza unahusisha ujenzi wa madarasa 26, ofisi 24 za watumishi, kumbi mbili za mikutano na vyoo 18 vya kisasa. Unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 5.6 hadi utakapokamilika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya TPSC, Ng’wanzalima Samwel John, ameipongeza Menejimenti ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa kusimamia mradi huo na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuufuatilia ili ukamilike kwa wakati uliopangwa.
Mshauri wa Mradi, Arch. Justo Lyatuu, amesema utekelezaji unaendelea vizuri na kwamba mradi unatarajiwa kukamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Bodi na Menejimenti ya TPSC za kufuatilia miradi ya maendeleo ya Chuo na kuhakikisha inatekelezwa kwa kuzingatia mipango, viwango na malengo yaliyokusudiwa.
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)



No comments:
Post a Comment