Farida Mangube, Morogoro
WANANCHI wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki wamenufaika na huduma za matibabu ya kibingwa bila gharama baada ya Mbunge wa jimbo hilo, Hamis Taletale maarufu Babu Tale kugharamia vipimo, matibabu na dawa kwa wote watakaohudhuria kambi maalumu ya afya inayoendelea katika Tarafa ya Ngerengere.
Kambi hiyo ya siku 10, imeanza Novemba 10 na kutarajiwa kuhitimishwa Novemba 20, 2026, imeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Mbunge na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ikiwa na lengo la kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Sendiga, Babu Tale amesema hakuna mwananchi atakayeshindwa kupata huduma kwa sababu ya kukosa fedha, akisisitiza kuwa gharama zote za matibabu kwa watakaohudhuria kambi hiyo zitagharamiwa.
Amebainisha kuwa huduma zitakazotolewa bure ni pamoja na vipimo vya moyo kwa kutumia teknolojia za ECHO na ECG, uchunguzi wa afya, ushauri kutoka kwa madaktari bingwa, matibabu pamoja na dawa kulingana na mahitaji ya wagonjwa.
Hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo, ambayo yanahitaji utambuzi wa mapema na uangalizi wa kitaalamu ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Katika kuimarisha zaidi ustawi wa wananchi wenye hali ngumu kiuchumi, Babu Tale pia ametangaza mpango wa kutoa bima za afya bure kwa kaya maskini 150 zisizo na uwezo ndani ya jimbo hilo.
Mpango huo unatajwa kuwa sehemu ya jitihada za kupunguza changamoto ya wananchi kushindwa kupata huduma za afya kutokana na gharama, huku ukilenga kuhakikisha familia zenye uhitaji zinapata fursa ya kupata matibabu bila kukabiliwa na vikwazo vya kifedha.
Kambi hiyo ya matibabu ya kibingwa inatarajiwa kuwa mkombozi kwa wakazi wa Ngerengere na maeneo jirani, kwa kuwapa nafasi ya kupata huduma za kitaalamu ambazo kwa baadhi yao zimekuwa ngumu kuzipata kutokana na umbali na gharama za matibabu.

.jpeg)


.jpeg)


No comments:
Post a Comment