JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


1. Mkenda: Wabunifu wajikite kwenye mahitaji ya soko

Share This

 

Dar es Salaam
WABUNIFU  na watafiti nchini wametakiwa kuangalia mapengo yaliyopo katika soko la bidhaa na huduma ili kuelekeza ubunifu wao katika kutengeneza bidhaa zinazohitajika, badala ya kuwekeza katika teknolojia zisizo na uhakika wa kupata soko.

Hatua hiyo inalenga kuifanya sayansi na teknolojia kuwa kichocheo cha uzalishaji viwandani, kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na kuongeza fursa za biashara kwa wabunifu wa ndani.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akizungumzia maandalizi ya kilele cha maadhimisho ya miaka 40 ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), yatakayofanyika Novemba 17 na 18 mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Profesa Mkenda amesema Tanzania ina watafiti na wabunifu wenye uwezo wa kutengeneza teknolojia mbalimbali, lakini changamoto iliyopo ni kuhakikisha ubunifu huo unajibu mahitaji halisi ya soko na kugeuzwa bidhaa zinazoweza kuzalishwa kwa wingi.

"Hakuna nchi duniani inaweza kuendelea bila kuwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia na kwenye ubunifu unaosaidia sekta mbalimbali kama kilimo, madini, huduma mbalimbali," amesema.

Amesema badala ya taasisi za elimu na utafiti kuwekeza katika malengo makubwa yasiyoendana na uwezo wa sasa wa uzalishaji, zinapaswa kuanza kwa kubaini bidhaa ambazo nchi inazihitaji na ambazo bado zinategemea kuagizwa kutoka nje.

Ametolea mfano Chuo cha DIT, akisema kinaweza kuelekeza nguvu katika kutengeneza vipuri vya magari na pikipiki, ikiwamo mifumo ya breki (brake pads), ambavyo vina soko nchini kutokana na matumizi ya vyombo hivyo vya usafiri.

"Huwezi kuanza kutengeneza gari, au pikipiki au helkopta lazima uanze na vipuri mfano nimewapa kazi DIT waangalie kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania ni bidhaa au vipuri gani vya pikipiki ambazo zinaagizwa sana kutoka nje, halafu angalieni namna ya kuanza kuzalisha kisha mnakuja na kampuni tanzu," amesema.

Kwa mujibu wa waziri huyo, mkakati huo utasaidia kujenga uwezo wa viwanda vya ndani hatua kwa hatua, huku ukitoa nafasi kwa wabunifu kushirikiana na taasisi za uzalishaji na wafanyabiashara.

Baadhi ya bunifu zilizofanywa na Watanzania tayari zimeonyesha uwezekano wa kupata soko hata nje ya nchi, akitaja kifaa cha Mkanda Salama kinachosaidia kudhibiti tatizo la kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua (Postpartum Haemorrhage—PPH).

Amesema kiwanda cha kutengeneza kifaa hicho kimeanzishwa Kimara Suka, Dar es Salaam, huku Rwanda na Ethiopia zikionyesha nia ya kukinunua.

Bunifu nyingine ni chanjo ya samaki inayolenga kuzuia magonjwa katika ufugaji wa samaki na teknolojia nyingine ya kuzalisha gesi ya oksijeni na hidrojeni kwa kutumia maji, iliyobuniwa na Mbunifu Luvanda wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).

"Unatenganisha gesi hizo ambapo Oksijeni unaweza kutumia hospitalini na hidrojeni unawwza ukatumia kupikia. Tumeagiza vyuo vyetu viangalie ili ikiwa sawa tuokoe hela kwa kutumia maji tu tunayoyachota" amesema.

Pia ametaja teknolojia ya kutengeneza saruji ya gharama ndogo zaidi kwa kuchanganya pozzolana na chokaa, iliyobuniwa na mwanafunzi wa shahada ya uzamivu kutoka Ethiopia anayesoma Chuo cha Nelson Mandela jijini Arusha.

"Kimachobuniwa tunatakiwa tuhakikishe kinaingia sokoni, sio kila mara tunaonesha leo tumebuni gari miaka 20 mbele halisogei. Tunataka ubunifu unaozalisha," amsema.

Profesa Mkenda amesema mifano hiyo inaonyesha umuhimu wa kuunganisha utafiti, ubunifu na mahitaji ya watumiaji ili kuhakikisha teknolojia zinazotengenezwa zinakuwa na matumizi yanayoeleweka na uwezo wa kuuzwa.

Hata hivyo, amesema mafanikio ya ubunifu hayawezi kupimwa kwa idadi ya teknolojia zinazoonyeshwa kwenye maonesho au zinazobaki maabara, bali kwa uwezo wake wa kutatua changamoto, kuzalishwa kwa wingi na kuingia sokoni.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira ya kukuza ubunifu kupitia Mfuko wa Ubunifu wa Samia (Samia Innovation Fund), unaolenga kusaidia wabunifu kuendeleza mawazo yao na kuyageuza kuwa biashara zinazoweza kuzalisha ajira na kuchochea uchumi.

Amesema pia inawekeza katika elimu ya sayansi, ufadhili wa wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya sayansi na utoaji wa tuzo kwa wahadhiri na watafiti wanaofanya tafiti zenye mchango mkubwa.

Waziri huyo amesema kilele cha maadhimisho ya miaka 40 ya Costech kitakuwa fursa kwa wananchi kujionea bunifu mbalimbali za Watanzania na kujifunza namna sayansi na teknolojia zinavyoweza kutumika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele hicho Novemba 18.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad