Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa, amezitaka serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha, watafiti, wabunifu, wajasiriamali na washirika wa maendeleo kushirikiana kufungua fursa za uwekezaji na biashara kwa ajili ya kujenga uchumi endelevu wa buluu katika Bahari ya Hindi ya Magharibi.
Kwagilwa amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kubadilisha uwezo wa uchumi wa buluu kuwa fursa endelevu zinazoweza kuwekeza na kuchochea maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa kuunganisha uongozi wa bahari, hifadhi, biashara na uwekezaji.
Akifungua Mjadala wa Jukwaa la Biashara kuhusu kufungua fursa za uwekezaji na biashara kwa ajili ya uchumi endelevu wa buluu katika Bahari ya Hindi ya Magharibi, amesema mjadala huo umewaleta pamoja wadau mbalimbali kujadili vikwazo na fursa za kiutendaji zinazokabili biashara katika sekta hiyo.
Amesema mjadala huo umejikita katika namna ya kuunganisha rasilimali za bahari na masoko, huku jopo la kwanza likijadili uvuvi, mwani, jongoo wa bahari, uongezaji wa thamani, usimamizi wa baada ya mavuno na fursa za uchumi wa mzunguko.
Amesema maeneo hayo yanaweza kuongeza thamani inayobaki kwa wazalishaji na kupunguza taka kupitia ubora wa usindikaji, teknolojia, vifaa vya usafirishaji na viunganishi vya soko.
Kwagilwa amesema jopo la pili lilijadili fursa zinazoibukia za bioteknolojia ya buluu, kaboni ya buluu na utalii endelevu wa bahari na pwani, akieleza kuwa maeneo hayo yanaweza kuzalisha bidhaa mpya, huduma na vyanzo vya mapato.
Amesema utekelezaji wa fursa hizo unahitaji sayansi, viwango vilivyo wazi, teknolojia inayofaa, hifadhi na ushirikiano kati ya watafiti, jamii, wajasiriamali na wawekezaji.
Aidha, amesema jopo la tatu lilijadili ubunifu na ufadhili katika uwekezaji wa uchumi wa buluu, akisisitiza kuwa mawazo hayawezi kutimizwa bila utekelezaji.
“Biashara na waendelezaji wa miradi wanahitaji usaidizi ili kuwa tayari kwa uwekezaji. Wafadhili wanahitaji mifano ya mapato inayoaminika, uongozi bora, na hatari zinazoweza kudhibitiwa. Na serikali zinahitaji kutoa mazingira ya biashara yanayotabirika na kuwezesha,” amesema.
Amesema ufadhili mchanganyiko, dhamana, mtaji nafuu, ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi pamoja na mbinu nyingine za kugawana hatari zinaweza kusaidia kuziba pengo la ufadhili iwapo zitabuniwa vyema na kuoanishwa na vipaumbele vya kitaifa.
Kwagilwa amesema serikali za nchi wanachama zina wajibu wa kutoa mwelekeo wa sera ulio wazi, udhibiti thabiti, takwimu za kuaminika, michakato ya wazi, mipango ya spatial ya bahari, hifadhi za mazingira na jamii pamoja na uratibu kati ya taasisi.
Amesema sekta binafsi ina nafasi muhimu katika kuleta ubunifu, ufanisi, maarifa ya soko, mtaji wenye uwajibikaji na mifano ya biashara inayoweza kufanya kazi kwa kiwango kikubwa.
“Taasisisi za fedha lazima zisaidie kuunda bidhaa zinazofaa kwa biashara za uchumi wa buluu, ikiwa ni pamoja na biashara ndogo na za kati. Wakati taasisi za utafiti zinapaswa kusaidia kuhamisha maarifa na teknolojia kutoka maabara kwenda miradi ya mfano hadi kwenye matumizi ya kibiashara,” amesema.
Kwagilwa amesema kwa Tanzania Bara na Zanzibar, uchumi wa buluu ni sehemu muhimu ya ajenda ya maendeleo ya muda mrefu na umeelezwa katika Dira ya Maendeleo 2050, huku akikaribisha sekta binafsi kuchunguza fursa zilizopo.
Amesema wakati Mkataba wa Nairobi ukiingia katika miaka yake mitatu ijayo, ni muhimu kuimarisha uhusiano kati ya uongozi wa bahari, hifadhi, biashara na uwekezaji.
“Tujenge uchumi wa buluu wa Bahari ya Hindi ya Magharibi ulio na ushindani na ubunifu, lakini pia unaojumuisha wote, unaohimili mabadiliko ya tabianchi, na unaotegemea matumizi endelevu ya rasilimali za asili,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo na Uratibu wa Uchumi Buluu, Wizara ya Uchumi Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mondy Muhando, amewataka wadau wa Ukanda wa Bahari ya Hindi ya Kusini Magharibi kuacha kuzungumzia fursa za uchumi wa buluu kama uwezo wa rasilimali pekee, badala yake kuzibadilisha kuwa biashara endelevu zinazowekezeka na kuongeza thamani ya maliasili zilizopo.
Amesema changamoto iliyopo si kugundua rasilimali na fursa zilizopo katika ukanda huo, bali namna ya kuzigeuza kuwa biashara zinazoweza kuvutia uwekezaji.
Amesema ukanda huo una utajiri mkubwa wa maliasili, ukiwemo mwani, uvuvi, matumbawe, mikoko, bandari, rasilimali za utalii na njia za kimkakati za usafiri wa baharini.
“Kwa hiyo, changamoto yetu si kugundua kile tulicho nacho au uwezo tulio nao. Badala yake, changamoto yetu ni jinsi gani tutabadilisha vyote tulivyo navyo kuwa biashara endelevu na zinazowekezeka,” amesema.
Muhando amesema mwekezaji haangalii rasilimali pekee, bali huangalia mambo yanayoweza kujenga mnyororo wa thamani, ikiwemo masoko, miundombinu, vibali, vihatarishi na faida inayoweza kupatikana.
Amesema fursa za uchumi wa buluu katika ukanda huo zipo katika sekta mbalimbali, zikiwemo uvuvi na ukulima wa viumbe vya majini, mwani, uhafidhina wa viumbe vya baharini, utalii endelevu wa pwani, bandari na usafirishaji, ubadilishaji wa taka kuwa thamani pamoja na kaboni buluu.
“Hivyo tunapaswa kuacha kuonyesha tu fursa tulizonazo, badala yake tuzichukue fursa hizi pamoja na mifumo ya biashara, fedha, masoko, na utawala bora ili kutengeneza biashara zinazowekezeka,” amesema.
Aidha, Muhando amesema dhana ya uchumi mzunguko inapaswa kutumika katika kuendeleza uchumi buluu kwa kubadili namna rasilimali zinavyotumika, ambapo taka inaweza kuwa malighafi ya kutengeneza bidhaa nyingine yenye thamani.
Amesema uhifadhi wa mazingira haupaswi kuonekana kama kitu kinachoshindana na uwekezaji, bali vitu hivyo vinapaswa kwenda sambamba katika kuendeleza uchumi wa buluu.
.jpeg)



No comments:
Post a Comment